KAZI SABA ZA MKRISTO DUNIANI.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mkristo ni yule mtu aliyempokea YESU KRISTO kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yake, kisha anaanza kuishi maisha matakatifu  siku zote.
Mkristo ni wa thamani sana na Biblia inasema hivi juu ya wakristo waliookoka kwamba
 '' Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini MUNGU, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa MUNGU.-1 Petro 1:18-21''

-Kila mkristo anatakiwa awe ni Mkristo anayeweza kupambanua rohoni.
 Hatuendi mbinguni kwa vyeo wala karama bali tunaenda mbinguni kwa sababu BWANA YESU ametuokoa na tumeenenda katika utakatifu wake.

Kazi saba za Mkristo akiwa duniani ni;

   1. Kuishi maisha matakatifu.

 Waefeso 5:8 '' Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika BWANA; enendeni kama watoto wa nuru,''

-Tuenende kama watoto wa nuru.
-Watoto wa nuru hawako gizani kamwe bali wako nuruni.
-Kuenenda nuruni ni kuishi maisha matakatifu.
-Ni wajibu wako kama mteule wa MUNGU kuishi maisha matakatifu siku zote.

   2. Kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU na kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

2 Kor 4:2 '' lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU.''

-Kuliishi Neno la MUNGU ndio kazi yetu tuliompokea BWANA YESU KRISTO.
- Ili  tulishike Neno la MUNGU atakavyo MUNGU inabidi  tuwe pia na ROHO wake na sio kuwa na ROHO wa MUNGU tu bali tuongozwe na ROHO wa MUNGU.
-ROHO wa MUNGU ndio muhuri wa MUNGU kwetu.
-ROHO wa MUNGU ndio hutufundisha, hutukumbusha na kutusaidia katika mengi sana .
-ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana kwetu Wakristo, na Biblia inasema kwamba  
'' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.-Warumi 8:14''

  3. Kuwashuhudia wengine Injili ya BWANA YESU inayookoa.

Zaburi 96:2-6 '' Mwimbieni BWANA, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.  Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake. ''

-Ni lazima tutangaze Wokovu wa BWANA Kama Biblia inavyosema.
- Ni lazima tuwahubiri watu wote ili waje kwenye wokovu wa BWANA ulio wa thamani sana na wa uzima.
-Kutangaza matendo ya MUNGU ni sehemu moja ya kushuhudia habari za MUNGU wetu.

Marko 16:15 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.''

- Ni kazi ya kila mkristo kuihubiri injili kwa watu wote wanaomzunguka iwe shuleni au kazini au majirani na popote pale.

  4. Kulitimiza kusudi la MUNGU la wokovu.

Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. '' 

-Wokovu ni mpango wa MUNGU kumuokoa mwanadamu.
-Wokovu ni kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
-Wokovu kwa mtu huanza pale anapompokea YESU KRISTO kama BWANA na Mwokozi wake.
Tukishaingia katika Wokovu wa BWANA YESU kuna kazi MUNGU hutupa na hiyo kazi inatakiwa kutimia kupitia sisi.
Ukiifanya kazi ya MUNGU huko ni kulitimiza kusudi jema la Wokovu.
Inawezekana kabisa MUNGU amekuokoa wewe kwanza ili kupitia wewe watu maelfu wampokee BWANA YESU.
 ukilala hakika utakuwa hujalitimiza kusudi la MUNGU la Wokovu. Kama ukitimiza wajibu wao huo hakika umelitimiza kusudi la MUNGU la Wokovu.


   5. Kutangaza shuhuda za matendo ya MUNGU.

1 Petro 2:9-10 ''Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.'' 

-Mojawapo ya vitu vya kutangaza ni jinsi ulivyookolewa na BWANA YESU.
-Ni jinsi ulivyoponywa na BWANA YESU.
-Neno la MUNGU limejaa shuhuda za matendo makuu ya MUNGU hivyo hata kusoma tu Biblia kwa watu wengine ni kutangaza shuhuda za MUNGU aliye hai.

  6. Kudhihilisha tabia ya uungu kwa ulimwengu.

2 Petro 1:3-4 '' Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.'

-Tabia za uungu wa MUNGU wetu ni nyingi sana na hizo tabia za MUNGU inatakiwa tuziishi wateule wa MUNGU wote.
-Kusamehe kwa wanaotubu ni tabia ya MUNGU hivyo na sisi tunatakiwa kuwa watu wa kuwasamehe wengine.
-Kutokuwa na upendeleo ni tabia ya MUNGU ambayo sisi tunatakiwa tuwe nayo pia.
Ziko tabia nyingi sana za MUNGU ambazo na sisi wateule wake tunatakiwa tuwe nazo. 

7. Kutawala dunia na kutiisha ili kila watu au mamlaka ipate kumtii KRISTO maana nje na KRISTO hakuna Uzima wa milele. 

 Mwanzo 1:28 ''MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.''

-Tumepewa kutawala na kutiisha.
-Kama kuna mchawi anawatesa watu basi wateule wa KRISTO wakiomba mchawi yule anaweza kukimbia mji, unajua ni kwasababu gani?
Ni Kwa sababu BWANA ametupa kutawala na kutiisha vitu vyote.
Adamu aliambiwa akatawale na kutiisha lakini shetani alipomzidi akili Hawa basi wanadamu wakaondolewa kutawala na kutiisha lakini BWANA YESU aliporudi aliturudisha kutawala na kutiisha vitu vyote rohoni na mwilini.
Nimewahi kushuhudia waganga wa kienyeji wakizikimbia tunguli zao baada ya maombi ya kanisa.
Kwa sasa hatutiishi ndege na wanyama bali tunatiisha hasa katika ulimwengu wa Roho na sio ulimwengu wa mwili.

2 Kor 10:3-5 '' Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO;''

-Tunatawala na kumiliki kwa maombi tu.
-Timiza kazi yako mteule wa MUNGU.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments

Asante kwa somo nzuri. Leo nitaliongeya kanisani na wateule wa Mungu kenye ibada ya jioni. Ubarikiwe!

Zaburi 199:9 Kwenye kazi ya pili