KIU YAKO YA KUTAKA KUINGIA KATIKA NDOA NI?

 
Peter Mabula na mkewe Scholar Mabula.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe sana.
Nakukaribisha katika neno LA MUNGU
Kuna vitu Leo kuhusu uchumba hadi ndoa nitavigusia.
Nitatumia zaidi Neno ''vijana'' hata kama hiyo itakuwa inawakirisha yeyote ambaye hayuko kwenye ndoa ila anatarajia kuingia katika ndoa.


1 Kor 7:9 '' Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.'' 

-Biblia inasema ikiwa kijana hawezi kujizuia basi aoe.
-Ikiwa Binti hawezi kujizuia basi aolewe.
-Ni heri kuoa/ Kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
Tamaa ya ngono ni dhambi na haifai kuwepo kwa watoto wa MUNGU.
Suala la Kijana kuoa au Binti kuolewa ni muhimu sana kwa wanadamu na ni agizo la MUNGU.

Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''

Binafsi mimi Peter Mabula Naitambua kiu inayokuwa ndani ya vijana wakati Wa kutafuta ni yupi Wa kuwafaa Kwa ajili ya kuchumbia au kuchumbiwa.


Kuna ambao hutafuta lakini kuna ambao hutafutana kabisa.
Kila MTU hutaka kuingia kwenye ndoa Kwa malengo yake. 


=kuna ambao huingia kwenye ndoa Kwa sababu tu wamechoka kuwa wapweke.


=Kuna ambao huingia kwenye ndoa Kwa sababu tu marafiki zao wameoa au kuolewa.


=Kuna ambao huingia katika ndoa Kwa sababu tu umri umekwenda sana


=Wengine huingia kwenye ndoa Kwa sababu tu wanahitaji watoto.


Zote ni sababu za MTU kutaka kuingia kuingia kwenye ndoa Kwa spidi kubwa, Lakini mimi napenda nikupe ushuhuda wangu kwa ufupi juu ya jambo la kuoa maana Kwangu kidogo ilikuwa tofauti.



Je kiu yako wewe unayesoma somo hili juu ya kuingia kwenye ndoa ni nini?
Ukiulizwa swali kwamba ''Kiu yako ya kutaka kuingia kwenye ndoa ni nini?''
utajibuje?

Mimi Peter kabla ya kumwoa Scholar sept 20 Mwaka 2014 kuna mambo ambayo nilikuwa najiuliza kwamba kwanini huo ndio ulikuwa muda sahihi wa mimi kuoa?
Kuna sababu ambazo humfanya mtu kutaka kuoa au kuolewa, Kwangu nilitaka sana kuingia kwenye ndoa Kwa sababu ya andiko Fulani ambalo nilikuwa nikilisoma nakosa confidence kabisaaaaaaaaa
Andiko hill linasema "Apataye mke afanya kitu chema, Naye ajipatia kibali Kwa BWANA"

Andiko hilo ndilo lilokuwa linataka kuniliza kila kila nikisoma Biblia.
Nilikuwa naweza kuongea mengi lakini nikikumbuka tu kwamba sijajipatia kibali Kwa BWANA maana sina mke nilikuwa naishiwa pozi lote.

Andiko hilo ni Mithali 18:22 ''Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA.''

Nilitamani kujipatia kibali Kwa BWANA maana imeandikwa apataye mke afanya kitu chema, naye ajipatia kibali Kwa BWANA.
Nilikuwa nasikitika kwanini hadi wakati huo sikuwa na kibali Kwa BWANA?

Neno kibali ni upendelea wa kiMUNGU kwako juu ya jambo fulani kwa ukukufu wa MUNGU.
Inawezekana kabisa wewe una kibali katika mambo mengi lakini bado hujapata kibali cha ndoa.

Kuna ndoa hazina kibali mbele za MUNGU kwa sababu ya dhambi ya wana ndoa.
Hapo juu nimeuliza je kiu yako ya kutaka kuingia katika ndoa ni nini?
Kwa sababu ya dhambi kuna watu kiu yao ya kuingia kwenye ndoa ni kwa sababu wamebebeshana mimba hivyo kiu yao ya sasa kuingia katika ndoa ni kwasababu wanataka kuficha aibu ya mimba. Hawajatubia uzinzi wao na kwa kukwepa kuwaeleza wachungaji ili wawaombee, wao sasa wanataka kukimbilia ndoa ili kuficha uovu wao.

Waefeso 5:3-5 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU.  Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya MUNGU huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao.'' 

=Hasira ya MUNGU huwajilia wenye kuasi.
waasherati ni wenye kuasi hivyo kukimbilia kufunga ndoa bila kutengeneza kwanza uhusiano wao na MUNGU hapo sidhani kama kutakuwa na kibali cha BWANA cha ndoa, bali hadi watakapotubu na kurejea.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; ''
Kwa ambao walichachukuana kabisa naomba baada ya kujifunza somo hili mtengeneze na MUNGU. Watumishi wa MUNGU wako kila mahali, okokeni kama hamjaokoka na anzeni upya na BWANA YESU.

Je, kiu yako ya kutaka kuingia katika ndoa ni nini?
Inawezekana kabisa unataka kuoa/kuolewa kwa sababu tu unataka kuwaridhisha wazazi. Ndugu, usioe/kuolewa ili tu uwaridhishe wazazi.
Ndoa ni jambo nyeti na linahitaji umakini mkubwa kuliendea.
Kuna tatizo kwa sasa kwa vijana wengi juu ya yupi anafaa ambaye ni mpango wa MUNGU. 
Vijana wengi ili wajue kwamba binti fulani au kijana fulani ni mke/mume mwema wake basi lazima waote ndoto ndipo watathibitisha kwamba wamepata mke/mume mwema kumbe wakati mwingine sio kweli maana sio ndoto zote ni za kweli.
Ni kweli kabisa MUNGU husema kwa ndoto lakini MUNGU pia anasema na watu wake kwa njia zaidi ya 7 nje na ndoto. 
Na kwa njia rahisi zaidi ambayo MUNGU husema na watu wake ni kitu muhimu sana kinaitwa ''Amani ya KRISTO kuamua moyoni''

Wakolosai 3:15 ''Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.''

=Amani ya KRISTO huongea na kuonyesha kabisa jambo kama ni zuri au baya, kama jambo ni la baraka au ni la laana, huonyesha kama jambo ni la haki au sio la haki.
Lakini amani ya KRISTO huamua ndani ya wateule wa KRISTO tu.
Amani ya KRISTO husimamiwa na ROHO MTAKATIFU.
ROHO MATAKTIFU huliona jambo mwisho kabla ya mwanzo hivyo kama binti aliyeokoka atatamkiwa na kijana kisha binti amani ikaondoka maana yake jambo lile sio sahihi.
Kama kijana aliyeokoka atashawishiwa kuoa binti fulani lakini rohoni mwake kukawa hakuna amani basi hata kama binti yule ni mzuri kiasi gani inabidi aache kwanza au aombe mpaka amani itakapokuja.
Kama amani itakuja maana yake BWANA YESU ameweka matengenezo  na mtu yule sasa atafaa.
Japokuwa MUNGU anasema nasi kwa kutumia Amani ya KRISTO kuamua mioyoni mwetu lakini pia kuna baadhi ya vijana hujipotosha wao wakiisingizia amani ya KRISTO.
-Unakuta binti anataka kuchumbiwa lakini mchumbiaji hana kazi na anatoka familia maskini hiyo yule binti anadanganya kwamba hana amani moyoni kumbe ni kuogopa umaskini.
Huo ni mfano mmoja tu katika mingi ambayo watu hutumia Amani ya KRISTO mioyoni mwao vibaya.

Kiu yako ya kutaka kuingia katika ndoa ni nini?
Ndoa ni nzuri sana kama ukimpata mtu sahihi kutoka kwa MUNGU kisha wote mkawa ni wacha MUNGU mliookoka na mnaongozwa na ROHO MTAKATIFU katika maisha yetu.

Mithali 5:18 ''Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.''

-Hakika huwa kuna furaha katika ndoa kama ndoa hiyo kiongozi wake ni MUNGU.
-Huwa kuna furaha sana katika ndoa kama kila mmoja atakaa vyema kwenye majukumu yake yanayoagizwa na Biblia takatifu.
-Ni baraka kuwa katika ndoa takatifu, sio zile ndoa za kuchukuana kama kuku au bata.
Je kiu yako ya kutaka kuingia katika ndoa ni nini?

Mithali 12:4 '' Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake. '' 

-Je, wewe mama ni mke mwema kwa mmeo hata umekuwa taji kwa mmeo.
-Je, wewe mke ni taji kwa mmeo au ni balaa kwa mmeo?
Mke mwema  anatakiwa awe taji nzuri ya kung'aa kwa mmewe.

Je kiu yako ya kuingia kwenye ndoa ni nini?

Waefeso 5:28-29 ''Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama KRISTO naye anavyolitendea Kanisa.'' 

-Je, wewe mume ni mume mwema kwa mkeo.
Mume mwema humpenda mkewe kama nafsi yake.
-Mume mwema humpenda mkewe kama anavyojipenda yeye. Kama yeye hapendi kutukanwa basi hakika na yeye hatakiwi kumtukana mkewe.
Kama hapendi kunyanyaswa basi na yeye hatakiwi kumnyanyasa mkewe.
Kama mume hapendi kupigwa basi na yeye hatakiwi kumpiga mkewe hata siku moja. Mume mwema sifa yake ni kumpenda mkewe kama anavyojipenda yeye.
Nimekupa changamoto nyingi leo lakini naamini umejifunza kitu na sasa kiu yako ya kuingia katika ndoa itakuwa kiu sahihi na sio kiu kupelekeshwa na mwili au dhambi.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments