KUSHIKA MAAGIZO YA MUNGU NI JAMBO LA MUHIMU SANA.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kushika maagizo ya MUNGU ni jambo la muhimu sana.

Malaki 3:7 ''Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?''

''Mmegeuka mkayaacha maagizo yangu asema BWANA''

Kuna wanadamu wengi waliogeuka na kuyaacha maagizo ya MUNGU. 
Neno ''maagizo'' maana yake ni  maelekezo yatolewayo na mkuu kwa anayemuongoza.
Neno ''Maelekezo'' ni muongozo wa kufanya jambo.
Maagizo ya MUNGU ni muongozo wa MUNGU uliotolewa na MUNGU kwa ajili ya wanadamu wote kuishi kwa kufuata muongozo huo.
Muongozo wa MUNGU ambao wanadamu wote wanatakiwa kuufuata ni mmoja tu yaani Biblia takatifu.

Zaburi 112:1 ''Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake.'' 

Kila agizo la MUNGU juu ya maisha ya kila mtu liko katika Biblia takatifu ambalo ni Neno hai la MUNGU kwa watu wote.
Katika Biblia utapata muongozo wa jinsi ya kuishi ukimpendeza MUNGU na wanadamu.
Kutokufuata Neno la MUNGU ambalo ndilo muongozo ni kumdharau MUNGU aliyeutoa.

Yeremia 47:7a  ''Utawezaje kutulia, Ikiwa BWANA amekupa agizo?  ''

Kuna maagizo mengi ya MUNGU kwetu.

=Agizo la kwanza  nikuokoka kwa kumpokea YESU kama Mwokozi wako.

Yohana 3:16-19 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. ''


=Agizo la pili ni Kutubu dhambi zote.

 Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.-Mathayo 3:2

=Agizo la tatu ni kuacha dhambi zote na kuanza kutenda mema yanayoagizwa na Biblia.

Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''

=Agizo la nne ni uwe mtakatifu siku zote.

1 Petro 1:14-16 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. ''

Kuna madhara makubwa sana kwa mtu anayeenda kinyume na maelekezo ya MUNGU.
Maelekezo ya MUNGU ni wanadamu waishi maisha ya Wokovu ambao maisha hayo yako pekee katika KRISTO YESU.
=Kumkataa YESU KRISTO ni kumkataa MUNGU.
=Kuukataa Wokovu wa BWANA YESU ni kuukataa uzima wa milele.
Kila mtu amehubiriwa injili lakini sio wote waliitii injili ya KRISTO japokuwa waiijua kwenye fahamu zao kwamba injili hiyo ndio muongozo pekee wa uzima wa milele kwao.
 Biblia inasema hivi huwa kuna wakati wa MUNGU kuwaacha waasi ili wafuate wanachokiamini kilicho nje na Wokovu wa KRISTO lakini mwisho ni hukumu ya kutisha.

Warumi 1:21-25 ''Kwa Sababu, Walipomjua MUNGU Hawakumtukuza Kama Ndiye MUNGU Wala Kumshukuru; Bali Walipotelea Katika Uzushi Wao, Na Mioyo Yao Yenye Ujinga Ikatiwa Giza. Wakijinena Kuwa Wenye Hekima Walipumbazika; Wakaubadili Utukufu Wa MUNGU Asiye Na Uharibifu Kwa Mfano Wa Sura Ya Binadamu Aliye Na Uharibifu, Na Ya Ndege Na Ya Wanyama, Na Vitambaavyo. Kwa Ajili Ya Hayo MUNGU Aliwaacha Katika Tamaa Za Mioyo Yao, Waufuate Uchafu Wao, Hata Wakavunjiana Heshima Miili Yao. Kwa Maana Waliibadili Kweli Ya MUNGU Kuwa Uongo, Wakakisujudia Kiumbe Na Kukiabudu Badala Ya MUUMBA Anayehimidiwa Milele, Amina''

Kuna watu hupotoshwa na viongozi wao wa dini.
Kiongozi akianguka dhambini ni rahisi kuwaangusha waumini.
Kuna ambao wameangushwa na viongozi wao wakuu wa kikanisa ngazi ya dunia.
Kama askofu mkuu wa kanisa lenu ataanguka ni rahisi pia maaskofu wadogo kuanguka.
Ni rahisi kwa wachungaji kuanguka.
Ni rahisi zaidi kwa waumini kuanguka na kuiacha kweli ya KRISTO.


Ndugu Yangu, Ni Hatari Mtu Akufundishe Uongo Na Wewe Unasema "amina Kubwa". 
-Ni Hatari Mtu Akuhubiri Maagizo Yake Wewe Uyashike Huku Mmeacha Maagizo Ya MUNGU. 
-Ni Hatari Kwako Uliyemjua JEHOVAH MUNGU Wa Kweli Ambaye Anapatikana Katika KRISTO YESU Pekee, Lakini Kwa Tamaa Ya Pesa Au Kushawishiwa Umeamua Kumwacha. 
-Ni Hatari Kwako Unayesujudia Sanamu Za Wanadamu Au Wanyama Na Kuziabudu. 
BWANA YESU Kwa Sauti Kali Anasema Geuka.
 ''Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, MUNGU wenu-Walawi 19:4''

Mwenye sikio la kusikia na kuacha mabaya na asikie leo.
 
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments