KUTEMBEA GIZANI

Na Mtumishi Frank P. Seth

"Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi? Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa. Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu" (Isaya 57:11-13).
Kuishi maisha ya imani ni sawa na kutembea gizani. Yaani, unaenda, sio kwa sababu unaona kwa macho haya ya nyama, bali unaona kwa macho ya ndani kwamba uko salama. Na, Imani yako izidipo kukua sana, ndipo UJASIRI wako huongezeka na kukuwezesha sio kutembea tu gizani ila kukimbia gizani, tena unakuwa salama. 

Sasa, ona jambo hili, yeye asiye na imani hukushangaa kwamba unawezaje kukimbia gizani wakati hakuna nuru? Wewe pia humshangaa asiye na imani kwa kuwa anashindwa kusogeza mguu wake kwa sababu "anaSABABU za kutosha" za kufanya hivyo. Kwanza, ni hatari sana kutembea gizani mahali ambapo hujui kama kuna shimo au laa, ukijikwaa je? (logic inagoma). Pili, kama Mungu alitaka nifanye jambo, kwanini haliweki wazi sana hadi mwisho? nk. Hizi ni dalili za "kwenda kwa kuona, sio kwenda kwa imani".
Hakuna aliyeona safari nzima hadi mwisho kabla ya kuianza, naam, hata manabii wakuu. Kila aliyepiga hatua, alianza kwa imani, katembea kwa imani na kumaliza kwa imani. Ukisubiri uone kila kitu ndio uanze safari, huo sio utaratibu wa Mungu huyu nimjuaye. Ona habari za Musa, kabla ya kuanza safari hakuwahi kufikiri kuvuka baharini kwa mguu, ila alivuka kwa imani. Ona Ibrahim, hakujua njia nzima aendako, ila aliondoka na kuanza safari kuhamia nchi asiyoijua, alifika kwa imani, nk.

Angalia jambo jingie, asemaye uongo, husema uongo kwa sababu anadhani asemacho KIMEFICHIKA (kiko gizani). Kwa hiyo, kwa sababu macho ya nyama hayaoni, basi husema uongo akijua hakuna aonaye! Ndipo mwenye imani huona hata gizani, kwa maana macho yake ni zaidi ya haya ya mwilini. Je! Imani haiji kwa Neno la Kristo? Je! Lipo jambo lililojificha mbele ya Neno? Angalia, hatusemi kweli kwa sababu WATU WANAONA, ila tunasema kweli kwa sababu HATUWEZI KUMFICHA MUNGU kitu. 

Ndipo BWANA akauliza, Je! "ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?" Yaani, kwa sababu Mungu amejificha mahali usipomwona, humwogopi! na kwa sababu hao watu unawaona, unawaogopa zaidi ya Mungu! 

Sasa ona jambo hili, amwaminiye Mungu sana, uwepo Wake ni dhahiri sana kuliko wa hao awaonao kwa macho, ndipo hatawaogopa wala kutimiza MATAKWA yao, japo yuko gizani, atasema kweli. Kumbuka akina Shedrack, Meshak na Abednego, mbele yao kuna mfalme na jeshi lake, ila wanamwona Mungu ambeye hakuna amwonaye kwa macho haya, na wanasema kweli tu bila kujali sana MADHARA yake kwa sababu japo wapo GIZANI, wapo wazi sana mbele za Mungu na wako SALAMA sana mikononi mwake, japo ni gizani. Hao watapiga mbio na wala hawatajikwaa wala kuanguka, japo ni gizani.
Frank P. Seth

Comments