MIPANGO YA MOYO WAKO KWA MWAKA 2016 NI IPI?

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze.
Ni Neema ya MUNGU kuishi katika mwaka mwingine wa nyongeza. 
Mipango ya moyo wako kwa mwaka 2016 ni ipi?
Biblia inakushauri hivi 
'' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.-Yakobo 4:7 ''
-Kuna watu wanapanga mipango mbalimbali katika mwaka mpya ujao lakini Neno Hili nilipewa nimwambie kila mwanadamu kwamba katika kila analolipanga mwaka ujao  ahakikishe anamtii MUNGU katika yote na wakati huo ampinge shetani na kuzikataa kazi zake zote.
-Kama ndugu yangu unawaza mwakani kwenda kwa mganga wa kienyeji ili akusaidie, mimi nakuomba usiende huko bali okoka na fuata maombezi kanisani.
Vinavyoonekana vyote ni vya muda mfupi tu.
Inawezekana kabisa mwakani unapanga kupunguza ratiba za kwenda ibadani kwa sababu tu ya biasahara yako, lakini mimi nakuomba hakikisha unamtiii MUNGU na hakikisha unajifunza sana Neno la MUNGU kanisani.

 Isaya 55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. ''

Inawezekana wewe umeokoka, hakika umefanya vyema kuokoka lakini napenda ujue kwamba;
Watu wengi waliosongwa na mambo ya dunia inakuwa ngumu sana kwao kulitimiza kusudi la MUNGU la utumishi.
Kwa sababu kila mtu anautaka uzima wa milele basi ni muhimu sana pia kujua kwamba;
 Kuonyesha uko safi nje haitakusaidia kama ndani yako ni kuchafu.
Safisha ndani yako ndipo na nje patakuwa safi.


 Mathayo  23:24-26 ''Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. ''

-Safisha ndani yako ndipo na nje patakuwa safi.
-Usikubali kufuga dhambi bali itubie.
-Dawa ya dhambi ni moja tu yaani damu ya YESU, Na hiyo damu ya YESU itatenda kazi kipindi ambacho utatubu na kuacha uovu.

 Yuda alimsaliti YESU.
Mtu yeyote aliyeokoka akitenda dhambi naomba ajue kwamba na yeye anamsaliti YESU kama Yuda alivyosaliti.

Mwaka ujao usikubali kuwa msaliti kwa BWANA bali mtii na kataa shetani na kazi zake zote.
Kama Mwaka huu ulitenda dhambi na uovu mwingi basi hakika mwaka ujao unabadilika mfumo wa maisha yako na anza kuishi maisha mataktifu yanayompendeza MUNGU aliye hai.

1 Petro 1:13-18 '' Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake YESU KRISTO.
Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita BABA, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO.
  ''


Kwanini MUNGU anaitwa BWANA?
Maana ya MUNGU kuitwa BWANA ina maana kwamba anakutawala yeye na anakuongoza yeye, ana msaada wa mwisho kwako na ana kalenda ya maisha yako kama ukiamua kuongozwa na ROHO wake Mtakatifu huku ukiishi maisha safi ya Wokovu katika KRISTO YESU.

Zaburi 16:2 '' Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu; Sina wema ila utokao kwako.'' 

 Kila mteule wa KRISTO ameitwa katika kusudi fulani katika kazi ya MUNGU.
MUNGU anaweza kumweka mtu fulani katika mahali fulani kwa wakati fulani ili kulitimiza kusudi lake fulani.
Kila mteule ana zamu yake katika utumishi mbele za MUNGU.
Ndugu, timiza zamu yako ya utumishi kwa wakati ulioitwa na BWANA YESU.

Utumie Mwaka wa nyongeza aliokupa BWANA katika matendo mema na sio dhambi.
 Wakolosai 2:6-7 '' Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, BWANA, enendeni vivyo hivyo katika yeye;  wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.''


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments