NI MUHIMU SANA KUKUA KIROHO.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mtu aliye amua kukua kiroho hakika ni lazima akue kiroho.
-Kwa nini tunasinzia makanisani wakati kwenye ma-baa kabla hatujaokoka tulikuwa tunakesha? 
Kwanini imekuwa vigumu kuzungumzia habari za MUNGU, lakini ni rahisi kuzungumzia watu wengine? (umbea ).
Kwanini imekuwa hata vigumu ku-post status za kumtukuza MUNGU lakini tuna-post vitu sawasawa na wapagani? 
Na Mtumishi Peter Mabula
2 Petro 3:18 '' Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua BWANA wetu na Mwokozi YESU KRISTO. Utukufu una yeye sasa na hata milele.''

Biblia kwenye maandiko hayo juu imesema ''KUENI''
-Kumbe ni muhimu sana kukua.
-Hakuna ambaye huzaliwa akiwa mtu mzima bali huzaliwa akiwa mchanga kisha anaanza kukua taratibu kulingana na chakula anachokula.
Hata mtu anayeokoka, kibiblia ni mtoto mchanga kiroho hivyo anatakiwa akue kiroho ili awe mtu mzima. 
ili mkristo akue kiroho inategemea na chakula cha kiroho anachokula kila siku. 
Chakula cha kiroho ni Neno la MUNGU analofundishwa kila mara.

Mkristo halisi ni yule ambaye kila siku ana kiu ya KRISTO.
Mathayo 5:6 ''Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.''
-Kiu inayozungumzwa hapa ni kiu ya uhitaji wa rohoni.
-Watu kila siku wanaomba toba kwa sababu wana kiu ya kupata uzima wa milele.
-Huwa tunaenda kanisani kila siku kwa sababu tu tuna kiu ya kupokea kitu kutoka kwa MUNGU.

BWANA YESU anasema juu ya wenye kiu ya uzima wake kwamba '' Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.-Ufunuo 21:6 ''
-Mkristo Lazima awe na kiu ya kujua mambo ya MUNGU ndipo ataona umuhimu wa ibada na maombi.
-Tunahitaji lishe sahihi ya kiroho katika maisha yetu ya kiroho.
-Kama huna muda wa kula kiroho hakika kuna kitu utapungukiwa kiroho.
-Ili ukue kiroho unatakiwa ukifanyie kazi chakula cha kiroho unachopokea kila iitwapo leo.

Chakula cha kiroho ni neno la MUNGU.
Neno ni chakula kisichoharibika bali neno ni uzima na ushindi.
Yohana 6:27 ''Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na BABA, yaani, MUNGU. '' 



Watu wengi wakiwa wanafundishwa mambo ya kidunia huhakikisha wanaelewa na sio kukariri tu.  Lakini watu hao hao wakiwa wanafundishwa neno LA MUNGU hutamani mfundishaji amalize hata kama  ndio ana dakika 5 tu tangu aanze kufundisha.
-Hayo ni matokeo ya watu kukosa kiu ya Neno la MUNGU.
-Hayo ni matokeo ya watu kuipenda dunia huku wakichukia mambo ya MUNGU ambayo ni ya uzima wa roho zao.
1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.  ''


Ndugu, Kufungulia moyo wako ili upokee ya MUNGU ni muhimu zaidi kwako kuliko kung'ang'ania ufahamu wa mambo ya duniani.


Utaendelea vizuri katika maisha ya kiroho ukiyafuata mashauri yafuatayo kila siku:

=Uwe mwombaji .

Yohana 15:7 ''Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.''

=Jifunze na kulitafakari Neno la MUNGU.

Matendo 17:11 ''Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. ''

=Tii Neno la MUNGU siku zote.

Yohana 14:21 ''Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na BABA yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. ''

=Washuhudie wengine injili ya KRISTO ili waokoke.
 Mathayo 4:19 ''Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.'' 

 =Nyenyekea kwa MUNGU siku zote..
 1 Petro 5:7 ''Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;  huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. ''


=Umruhusu ROHO MTAKATIFU akutawale na kukuongoza siku zote.

Wagalatia 5:16-18  ''Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
''


Ukikua kiroho kuna faida nyingi sana kwako.
 Hata mtu akudharau mpaka akurushie na kinyesi usoni usiogope wala kuchukia jua kwamba ipo siku Baraka zako zitamiminika tu na kwa macho yake atashuhudia baraka yako. songa mbele tu na MUNGU wa wokovu wako
Ni maombi yangu kwamba;
 MUNGU ashughurike na wanaokuwazia mabaya ili mipango yao isifanikiwe na kwa macho yao washuhudie ushindi wako maana mawazo ya maadui zako siyo mawazo ya MUNGU
.MUNGU anakutakia mema siku zote

Yakobo 4:7-8 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.  '' 


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments