NI RAHISI NGAMIA KUPENYA TUNDU LA SINDANO KULIKO TAJIRI KUINGIA UFALME WA MUNGU.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Marko 10:17-25 '' Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? YESU akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye MUNGU. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. YESU akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. YESU akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa MUNGU! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. YESU akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa MUNGU! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa MUNGU. ''

BWANA YESU alimjaribu huyu tajiri maana alimjua rohoni mwake. BWANA alitambua kwamba roho ya huyu tajiri ilikuwa kwenye mali na sio kwa MUNGU.
Japokuwa tajiri alionekana anautaka uzima wa milele lakini alikuwa anapenda zaidi mali kuliko huo uzima wa milele.
Tajiri anayezungumzwa kibiblia sio lazima awe wa mali tu bali yeyote  aliyeridhika na hahitaji msaada wa kiroho huyo ni tajiri wa kidunia ambaye hahitaji mambo ya MUNGU.
Wengi hawajaokoka na hawahitaji kuokoka hata kama wanaambiwa kila siku waokoke, hao ni matajiri na wanajiona wako kamili hawahitaji msaada wa MUNGU wa uzima wa milele.
Kuna wengi sana wenye sifa kama za huyu tajiri, yaani wanapenda zaidi mali au vitu vya dunia kuliko kupenda uzima wa milele japokuwa wanautaka uzima huo.
Mali imekuwa muhimu kwa watu wengi kiasi cha kuabudiwa kabisa.
Mali imewafanya wengi kuwa watumwa wa mali.
Mtumwa wa kitu ni yule anayekitumikia kitu hicho.
Mtumwa wa mali  ni yule anayependa mali kuliko MUNGU.
Anapenda mali kuliko Ibada, anapenda mali kuliko mambo ya MUNGU.
Yuko tayari kwenda jehanamu akiwa tajiri kuliko kwenda mbinguni akiwa maskini, japokuwa hakuna mwanadamu hata mmoja  atakayeondoka duniani na mali zake.

1 Timotheo 6:7 ''Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ''

Kuna watu wanaweza wakatumia miaka 30 kutafuta mali na kufanya kila uovu na dhambi ili tu watajirike, watu hao hata kabla hawajafaidi mali zao wanakufa katika dhambi na kwenda upotevuni. Cha ajabu baada tu ya kuondoka watu hao ambao hawakuwa hata na dakika moja na BWANA YESU enzi za maisha yao lakini wakiondoka tu mali zile walizozitafuta kwa miaka 30 zinatumiwa ndani ya mwaka mmoja na wale waliowaachia mali hizo. 
 ''BWANA anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.-Zaburi 94:11''  
na ndio maana BWANA anasema  ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.-Mathayo 3:2''

Na mwanadamu mmoja mwenye hekima aliyatazama mambo ya dunia na kuona kuwa ni ubatili tu tena hakuna jipyachini ya jua na yote ni ubatili tu.

Mhubiri 1:2-9 '' Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake.  Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. '' 

Wengi wametafuta utajiri lakini kabla ya kuupata wakaondoka duniani, huo hakika ni ubatili mtupu.
Unakosa yote kwa sababu ya kutafuta mali.
unakosa mali unazozitafuta na unakosa uzima wa milele kwa sababu ya mali ulizokuwa unatafuta.
Mtumwa wa mali ni yule anayependa mali kuliko uzima wa milele, lakini Biblia inasema hatuwezi kutumikia MUNGU na mali.

Mathayo 6:24 ''Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia MUNGU na mali.''

 Sifa za tajiri anayezungumziwa kwamba ni vigumu kuingia katika uzima wa milele.

   1.  Anapenda pesa kuliko MUNGU.
1 Timotheo 6:10 ''Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.''

  2.   Ameridhika na ufahamu wa dunia.
1 Yohana 2:15 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.'' 
-Mtu kama huyo hata akilisikia Neno la MUNGU, Kwa sababu ya mali na mambo ya dunia Neno hilo halizai matendo mema kwake.
Mathayo 13:22 ''Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.''

 3.  Anajifanya hana uhitaji wa kiroho wa kuokoka.
Mathayo 5:3 '' Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.''
-Maskini wa roho ni wale ambao wanaachana na mambo ya dunia na kumpokea YESU ili awape uzima wa milele. Tajiri anaweza kulidhika na alivyo hata asihitaji mambo ya roho ambayo ni Neno la MUNGU la uzima.
-Huwa tunaenda kanisani kwa sababu sisi ni maskini wa roho yaani tunauhitaji wa rohoni. tajiri hawezi kuacha kazi zake ili akamwabudu MUNGU.
-Tunatubu na kulia mbele za MUNGU kwa sababu tunahitaji BWANA atutakase lakini tajiri ni ngumu kwake kunyenyekea mbele za MUNGU ili atubu.

  4.  Hutumia pesa zake kwenye dhambi.
 1 Timotheo 6:9 '' Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.'' 

  5.  Pesa ni kila kitu kwake hivyo hahitaji msaada wowote maana anajiona amekamilika.
Mathayo 6:24 ''Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia MUNGU na mali.'' 
-Pesa inakuwa kila kitu kwake maana anapata kila akitakacho cha dunia kiwe ni kibaya au ni kizuri lakini Biblia iko wazi ikisema kwamba kuna hukumu mbeleni. 
Mhubiri 11:9  '' Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote MUNGU atakuleta hukumuni. ''

  6.  Pesa imempa kiburi na kinga feki.
 1 Timotheo 6:17 ''Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini MUNGU  atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha''
Tena Biblia inaendelea kusema 
''BWANA asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; -Yeremia 9:23''

   7.  Pesa imemtungea na watu wa kumsaidia kiroho.
1 Timotheo 5:20 ''Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.''
-Anayeagizwa kuwakemea wenye dhambi ni mtumishi wa MUNGU ambaye atakemea dhambi kanisani madhabahuni lakini huko kanisani tajiri kumpata ni jambo gumu sana maana wakati wengine wako kanisani yeye tajiri yuko busy kwenye mishemishe zake. Wakati wengine wakimpokea YESU jumapili kanisani tajiri yeye yuko kwenye biashara zake hivyo mali zake huyo zinamtenga na watu ambao wangemsaidia kiroho hata akaifikia toba ya kweli katika KRISTO YESU mwokozi wa watu wote.

Yakobo 5:16 ''Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.''

-Kuongozwa sala ya toba ni kwa wanyenyekevu tu na ambao wanafika ibadani, tajiri yeye wakati wengine wakiongozwa sala ya toba kanisani na kupatanishwa na MUNGU wao matajiri watakuwa busy muda huo na mambo yao.

Kama ndugu umezongwa na mambo ya dunia na mali zako zimekuweka mbali na BWANA YESU nakuomba ugeuke leo.
Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments