NINI MAANA YA KUJITWIKA MSALABA!?

Na Mwl Nickson Mabena
Bwana Yesu asifiwe Mtu wa Mungu, karibu wakati huu tujifunze Neno la Mungu,
Karibu!
"Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate" Marko 8:34
Yesu amezungumza mambo mawili kwa mtu anayetaka kumfuata, mambo hayo ni KIJIKANA na KUJITWIKA Msalaba.
Katika somo hili ntazungumzia KUJITWIKA MSALABA,
Kama andiko hilo tungetakiwa kulitafsiri kama lilivyo, basi ingetulazimu kuingia Misituni kwenda kutafuta Miti kwa Ajili ya kutengeneza Misalaba ili tumfuate Yesu!.

Kupitia Somo hili utahifunza nini maana ya kubeba Msalaba kama alivyomaanisha Yesu.
Yesu alizungumza Maneno hayo kwa mtu yeyote anayetaka Kumfuata Yesu, lazima akae chini ahesabu gharama kwanza kabla hajamfuata Yesu!. Gharama zenyewe ni Kujitwika Msalaba!
KUJITWIKA MSALABA MAANA YAKE NI KUKUBALI YAFUATAYO:-
a) Kukubali AIBU
".... ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau Aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu" Ebr 12:2b

Mtu aliyeamua kumfuata Yesu lazima, akubali Aibu wakati mwingine.. Mfano Kuhubiri injili ni kukubali aibu, maana yake wengine watakuona kama unapoteza muda tu, na utakuwa Tayari kuaibika kwa ajili ya BWANA.
Sio kuhubiri tu, wakati mwingine katikati ya rafiki zako, yakupasa uidharau Aibu, Na ujivike ujasiri wa kusema kwamba wewe umeokoka, na haupo tayari kushirikiana nao kwenye dhambi!
b) Kukubali KUKATALIWA.
"Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima" 1Petro 2:4
Watu wengi baada tu ya kuamua kuokoka, wakajikuta wanakataliwa na Ndugu, jamaa na marafiki. Na wanashindwa kuelewa ni kwa nini, ila hiyo ni ishara moja wapo wa kuubeba msalaba, wengine wamerudi nyuma kwa kuwaogopa wanadamu.
Yesu alikataliwa, ila kwa Mungu alikuwa mteule!!.
Hata mwanadamu anaweza kukataliwa lakini kwa Mungu akawa ni Mteule.

c)Kukubali KUTUKANWA.
"mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana" 1Petro 4:4
Matusi ni kawaida ya wafuasi wa shetani, wakiwatukana watu wa Mungu, si ajabu kwa hata Yesu mwenyewe alikubali kutukanwa. Ninamshukuru Mungu kwani nimewahi kutukanwa kwa ajili ya Injili, sikurudisha kitu kwa sababu najua ndio kuubeba msalaba wa Yesu, mara nyingi watu wa dunia hii huwatukana watu wanaohubiri injili...
d)Kukubali KUDHIHAKIWA.
"Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema" Math 27:39
Yesu wakati amekubali kuubeba msalaba, watu walimtukana, pia walitikisa-tikisa vichwa vyao kama ishara ya kumdhihaki. Najua mtu baada ya kuokoka watu lazima waanze dhihaka, lengo kuu la shetani katika hili ni uuache wokovu, dhihaka lazima ziwepo tena toka kwa watu wa karibu sana. LAKINI SONGA MBELE YESU ANAWEZA YOTE na amekuita kwa kusudi maalumu.
e)KIFO KWA AJILI YA BWANA.
Ni rahisi sana kulitaja hili, lakini ni ngumu sana katika utendaji, Yesu pia walimtundika, wakamuua. Wapo watu waliuawa kwa ajili ya YESU, hii yote ni kukubali kuubeba msalaba. mfano kina stefano katika biblia. Lakini pia hata nyakati hizi wapo, nmesika kwenye shuhuda mbalimbali, wapo waliofungwa magerezani kwa ajili ya YESU sasawa na UFUNUO 2:10, lakini bado YESU aliwatetea!
Mdo 10:39..
Tunajua dunia inapita, tujitoe kwa YESU kikamilifu, tukubali kuubeba msalaba hadi mwisho, naye atatupa taji ya UZIMA.
Hiyo maana ya KUJITWIKA MSALABA, na sio kubeba Mti na kusema umejitwika Msalaba!!!
Mwambie Mungu akufundishe zaidi kuhusu haya, maana ni muhimu sana kwa maisha ya Mkristo.
Baada ya kulikumbuka somo hili, nimedhamiria Kujipanga zaidi, na zaidi katika kuwa karibu na Mungu!.
nikutakie mafanikio mema katika Kristo
UBARIKIWE NA BWANA KATIKA JINA LA YESU.
Mwalm Nick.
0712265856
(Whatsapp#)

Email: mabenanickson@gmail.com

Comments