NYAMBIZI (SUBMARINE)

Na Frank P. Seth

"Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika;
Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili. Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa" (Ufunuo 3:1-6).

Nimetazama mistari hii ambayo nimeizoea sana lakini leo nikiitazama naona NYAMBIZI. Nyambizi ni chombo cha KIVITA cha majini chenye uwezo wa kupita chini ya maji (vilindini) au juu ya maji kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano, kama ni maeneo ambayo nyambizi haitakiwi kuonekana na watu basi hujizamisha chini ya maji na HUWEPO KAMA HAIPO, kumbe ipo. Na mara nyingine, nyambizi ikitaka KUSHAMBULIA adui, huibuka juu na kufanya shambulizi kisha kurudi vilindini isikoonekana na mtu.
Nimetazama mistari hii katika Ufunuo 3:1-6 nikaona tofauti ya mtu AKESHAYE na NYAMBIZI. Kuna maana nyingi za kukesha, ila kwa maana ya msitari huu ni kuwa (in sync) vizuri na Mungu wakati wote. Sasa, angalia, sijamaanisha kuwa malaika, ila kuishi maisha ya UTAKASO na KUTENGENEZA kama kuna mahali hapako vizuri. Ndio maana Roho anasema "Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu".
Msisitizao katika somo hili ni pale ambapo wakati wa SHIDA au UHITAJI utaona kila mtu yuko juu akitupa makombora dhidi ya adui kwa HASIRA, shida au uhitaji ukiisha, mara, huoni tena ile KASI na HASIRA kinyume na adui; NYAMBIZI hurudi vilindini kuendelea na maisha ya GIZANI kama vile haikuwahi kuelea na kufanya vita na adui wazi wazi.

Je! Utaona tofauti kati ya dawa za kutibu magonjwa na nyambizi? Nikatazama wala sikuona tofauti. Naam, ndivyo wengi tunavyomtumia Mungu kama dawa tu, yaani anahitajika wakati wa MAUMIVU kisha huwekwa kando na maisha kuendelea kama ilivyo kwa nyambizi vilindini mwa bahari.
Basi, "kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako".
Frank P. Seth

Comments