SABABU MOJAWAPO AMBAYO INAWEZA KUIFANYA KESHO IKAPIGA KONA: KUNA VITU VINAWEZA KUPANDWA NDANI YA MWILI WA MTU



ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA NA PASTOR YOSHIDA



-PASTOR YOSHIDA
Sisi tulio mpokea Bwana Yesu tunazo nguvu za Roho mtakatifu, Mungu ametupatia Baraka kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Tusiangalie maisha yetu kwa macho ya mwilini bali tunatakiwa tuangalie kwa macho ya Rohoni sababu Mungu wetu ni Roho na Baraka zetu tunazipata kuanzia ulimwengu wa Rohoni na kudhihirika kwenye ulimwengu wa mwilini.

“Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema.”
Luka 7:22

Neno la Mungu ni neno la Rohoni ndio maana linatenda kazi kuanzia Rohoni. Ukiliamini neno la Mungu unakuwa mshindi hata kama unaonekana hujapokea kile ulichokiomba, ukiomba jambo lolote unatakiwa uamini umeshapokea. Ukifanya hivyo lazima utafanikiwa na kubarikiwa sana.
Kuna binti mmoja alikuwa kipofu wa macho alikuwa anavaa miwani yenye lensI kubwa sana, siku moja alikuja kanisani kupata uponyaji, alimwamini Yesu akampokea na kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake akapona palepale baada ya maombi na kuacha kuvaa ile miwani. Kupitia uponyaji alioupata binti yule familia yake wote walimpokea Bwana Yesu kama mwokozi wa maisha yao wakawa wameokoka.
Ukimpokea Bwana Yesu kwenye maisha yako unatakiwa uwasaidie watu wengine wenye matatizo kwa jina na la Yesu kwa uwezo wa Roho mtakatifu na Mungu atakubariki na maisha yako hayatakuwa ya kawaida.
Tukiomba kitu kwa Mungu, Roho mtakatifu ambaye Yesu alituachia kama msaidizi wake anatusaidia jinsi itupasavyo kuomba na kukipata.
Kijana mmoja alikuwa mgonjwa ametoka jela. alikuja kanisani kupata uponyaji, Mungu alimponya ugonjwa wake na kuanza kumbariki. alikuwa anafanya kazi kiwandani na kulipwa mshahara mdogo lakini baada yakupata uponyaji alikuwa na ujasiri akaanza kufanya kazi kwa bidii na kupata kazi nyingine yenye mshahara mzuri, baada ya muda mchache alianza kufanya biashara ya magari na kuajiri rafiki zake waliokuwa naye jela na mpaka sasa ni mtu mzuri anamtumikia Mungu kwa bidii sana na biashara yake inaendelea kukua kila siku. Tunaona jinsi tukiwa na bidii kwa Mungu anatubariki na kutulinda dhidi ya maadui zetu kwa kuwa yeye ni mwaminifu.
Kijana mwingine alikuwa ana madeni mengi huku anatumia bangi na kuvuta sigara kwenye maisha yake ya kila siku. Siku moja alikuja kanisani kumpokea Bwana Yesu na kuombewa roho ya kutumia vilevi na kuvuta bangi na dawa za kulevya iliondoka ndani yake, akabarikiwa sana na kuanza biashara mpaka sasa amesha rudisha madeni yote aliyodaiwa na sasa ni mkurugenzi wa kampuni yake, ana wafanya kazi wengi sana. Familia yake ya watu hamsini wamempokea Bwana Yesu na wote wamebarikiwa sana.
Tunajifunza kwamba ukianza kubadilika rohoni na Mwilini pia utabadilika na kuwa mtu aliyebarikiwa.
Unatakiwa ufanye kitu chochote kupitia Imani yako, unatakiwa uombe uisikie sauti ya Mungu na kutii sauti yake. Kwa kufanya hivyo utabarikiwa sana. Ukiwa unaomba unatakiwa ukiri maandiko yanayoendana na hali yako uliyo nayo, mfano kama unaumwa unatakiwa ukiri "kwa kupigwa kwake nimepona", kwa kufanya hivyo kila siku Mungu atajidhihirisha kwako na kukubariki na kutimiza haja ya moyo wako maana sisi ni watoto wa Mungu hapa duniani na Mungu anatamani watoto wake wabarikiwe sana.


ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA


"SABABU MOJAWAPO AMBAYO INAWEZA KUIFANYA KESHO IKAPIGA KONA: KUNA VITU VINAWEZA KUPANDWA NDANI YA MWILI WA MTU"


Mungu anajua maisha yetu kabla hatujaanza kuishi na baada ya kuishi, ndiomaana anaitwa Alpha na Omega.
Mungu amekupa kesho yako kabla haijaanza kudhihirika uwe unataka kuwa Daktari, Profesa, Mwalimu, Mfanya biashara mkubwa, au mtu wa aina yeyote ile.
Unaweza ukaanza maisha yako na ukafika mahali ndoa haiendi tena, unaweza ukaanza kusoma ukafika mahali huwezi tena, unaweza ukaanza biashara ukafika mahali ikaharibika mambo yete haya yanaitwa [Kesho iliyopiga kona]
shetani amewapa watu akili kwamba pale wanapoona mambo yao hayaendi vizuri yameanza kuyumba wachukulie ni mapenzi ya Bwana kitu ambacho sio kweli.
Kwenye Biblia kuna mtu anaitwa Naomi alikuwa anaishi Bethlehemu, alihama pamoja na watoto wake kwenda sehemu nyingine kuishi na huko watoto wake walikufa wote akawa mwenye huzuni na akaamua kurudi Bethlehemu ambapo watu walipomuona walimkimbilia na kumuita Naomi [mbarikiwa] kitu ambacho alisema wasimuite bali wamuite huzuni maana amepatwa na matatizo. Kilicho mtokea Naomi kinaitwa kesho iliyopindishwa kona.
Mungu amesema katika siku za mwisho atatupa Mchungaji mwenye kuyajua maarifa. Maisha ya sasa tunayoishi ni maisha ya mtu anaishi kuendana na maarifa ya mchungaji.
Kama unaishi sasa hivi fahamu kuwa unalo kusudi linalokufanya uishi. Ndani yetu sisi Mungu ameweka maono ambayo tunatakiwa tuyatimize na lazima kila mtu atimize maono hayo ili turudi mbinguni tukiwa mashujaa kwa jina la Yesu.
Ukifika wakati Mungu ana haja na mtu, anasimamisha mambo mengine yote yasimame ili mtu huyo aende zake atimize kusudi lake.
Unatakiwa usiseme makosa yako uliyoyafanya ndiyo yamekufanya usifanikiwe au dhambi zako ndizo zimekufanya usifanikiwe sababu ukisema hivyo unamaanisha makosa yako na dhambi zako zina nguvu kuliko Mungu, Unatakiwa umfuate Mungu, uamini ukafanikishe maono yaliyoko ndani yako. Maono yanaweza yakawa maono ya Uchungaji, Uaskofu, Uraisi, Udiwani, bunge, Uwaziri, Ukurugenzi, Kusafiri kibiashara, Udaktari, Ualimu, Ukulima, ufugaji, au jambo lolote ambalo Mungu amekupa na kukuwezesha kulifanya
Pia Kuna vitu vimepandwa ndani yako kwasababu ya kubadili mwelekeo wako wa maisha yako ili usitimize maono ambayo Mungu amekupa.
Kwenye mambo ya Rohoni kuna vitu vya kutafsiri kiroho na kimwili, Mfano kimwili mtu na mke wake ni watu wawili, lakini kiroho mtu na mke wake ni mmoja, Tafsiri ya pili kimwili Mwili wa Mtu ni Nyama na tafsiri ya kiroho Mwili wa mtu ni udongo na unaweza ukapanda chochote kwenye mwili huu ambao ni udongo na kikaota ili mradi anayepanda awe yupo rohoni.
Kwa sababu hiyo chochote unachoweza kuufanyia udongo unaweza kuufanyia na mwili pia. Ndio mana Yesu akasema "lile pando ambalo Baba wa mbinguni hakulipanda litang'olewa".
Kwenye upande wa giza na wao nao wanaweza kupanda vitu vyao kwenye mwili wa mtu vikaota. Unaweza kumwona mtu analalamika mgongo unamuuma sana kumbe ndani yake amepandiwa kitu ambacho kinaufanya mwilini wake aonekane mgonjwa.

mchawi akiwa rohoni anakuona wewe kama udongo kwahiyo anakuja na vitu vyake na kuvipanda ndani yako na ukitaka kupita mahali unakwama sababu unakuwa kama pori lilojaa. Anaweza akatoboa mashimo ndani yako akaweka mapepo, mapepo nayo ni roho na yanaweza kujigeuza yakavaa umbo lolote.
UKIRI
"Kwa jina la yesu kama kuna chochote kilichopandwa ndani yangu kwa lengo la kubadilisha kesho Yangu ninaking’oa kwa jina la Yesu"
Kulikuwa kuna mpanzi mbaye alipanda mbegu kwenye udongo tofauti ambazo ni neno la Mungu, Mfano mwingine mtu alipanda kwenye shamba lake akalala na adui akaja usiku na kupanda magugu yakaota. Mungu aliamua magugu yale yaachwe yakue yote kwa pamoja na mvunaji akija kuvuna atajua avune nini na aache nini.
Yesu alisema adui ndiye aliyepanda usiku (shetani ndiye anayepanda) anaweza kupanda ujinga, uoga, chuki, magonjwa, mikosi, moyo usiokuwa wa kwako, magonjwa, akili bandia, tumbo la uzazi bandia, masikio bandia, laana, kukataliwa, ujinga, chuki, wivu, hasira, anasa, tamaa, uzinzi na uasherati, matusi, jazba, na mambo mengine mabaya kama hayo.
Ukilala shetani pamoja na mawakala wake wanakuja kupanda mambo yote hayo ndani yako, unatakiwa uwe mtu wa kuomba mwenyewe usitegemee kuombewa na Mchungaji bali ujifunze uwe mtu wa vita na maisha yako yatabadilika na utakuwa mmoja kati ya washindi.
UKIRI
"Kwa Damu ya Yesu ninang'oa kila kilichopandwa ndani yangu kwa jina la Yesu. Kila kilichopandwa ndani yangu ninaking’oa kwa jina la Yesu"
wengine kwenye familia zao kuna vitu vimepandwa na vimebadilisha mwenendo wa maisha yao na kuwa ya tofauti kabisa.
“Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.“ Yeremia 1:8
Kuna wakati Mungu aliuliza amtume nani aende kumdanganya mtu fulani duniani na pepo akajitokeza na kumwambia Mungu ‘nitume mimi nami nitakwenda na kugeuka kuwa pepo wa Uongo na kukaa kinywani mwake’. Tumeona mapepo yanaweza kugeuka na kuwa kitu chochote.
UKIRI
"Kwa damu ya Yesu nina ng'oa kila pando lilichopandwa ndani yangu kwa jina la Yesu, kila Pepo aliyegeuka na kuvaa umbo lolote na kuingia ndani yangu ninaamuru Ng’ooka kwa jina la Yesu"
Imeandikwa tumewekwa ili kung'oa, kubomoa, kuvunja, ili kujengana kupanda. Unatakiwa ungoe kila pando lililopo ndani yako kwa damu ya Yesu.

Comments