SADAKA NI YA NANI NA YA NINI?

Na Frank P. Seth

“na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.”
ISA. 58:10-11 SUV

Kuna mambo mawili na makundi matano ya watu ambayo huwezi kuacha kuangalia utoapo sadaka zako.
Mambo mawili: 1. Kazi ya huduma (kwa ajili ya agano) 2. Watu (kiwemo chakula)
Kazi ya huduma ni pamoja na kujenga makanisa, kugharimikia kazi za injili, nk.
Watu ni katika makundi haya makubwa matano: wajane, yatima, masikini, mgeni na Walawi. Lengo ni "ili kiwemo chakula" kama lengo kuu, japo mengine yapo ila ni madogo.
Angalia makundi haya matano ya watu, wote hawana urithi (kipato kutokana na biashara au kazi zao), wanaupungufu kwa namna kwamba wanahitaji kanisa liwasiadie, etc. kwa lugha nyingine, tukiamua kuwaweka wote kwenye kundi moja tungewaita maskini.
Kwa mtazamo huu, kwa haraka sana utagundua kati yetu (kwenye kizazi hiki) hakuna Walawi, na kama wapo ni kidogo sana, na kundi la mgeni sio dhahiri sana kwa muktadha wa dunia ya sasa. Ila tazama makundi haya matatu, WAJANE, MASIKINI na YATIMA. Je! wapo kati yetu na sadaka kiasi gani inaelekezwa kwao? Au kwa vile wao sio viongozi na hawana mtetezi?
Sasa angalia tena, sehemu KUBWA ya sadaka katika kizazi hiki cha ULAFI kinakwenda wapi? Je! Ni mara ngapi umefundishwa kwa msisitizo utoaji wa KUPELEKA kwa WAJANE, MASIKINI na YATIMA na sio mafundisho ya LETENI?
Zingatia jambo hili, ni LAZIMA utoe sadaka uendapo hekaluni, usiende mikono mitupu, ila angalia usitoe KILA MAHALI UONAPO kwa sababu umeshawishiwa kutoa. Jifunze kujua MAHALI pa kutoa na KIASI cha kutoa bila kupuuza MUDA wa kutoa sadaka zako.
Usisahau jambo hili, thamani ya sadaka sio sawa na thamani ya pesa au kitu (market value/price) ila moyo utoao. Na, angalia sana maana ukitoa ILI waone, umechakachua sadaka yako kwa sababu lengo ni IFIKE MBINGUNI sio kwa hao ulikopeleka.
Jiulize, nani anahesabu sadaka zako? Nani anajua umetoa nini? Zaidi sana, jiulize, KUSUDI lako la kutoa ni nini, au ukishatoa UNAJISIKIAJE moyoni? (kwamba "wanajua mchango wangu", "wameona ninavyojitahidi", "hata mimi nilichangia", "kama isingekuwa mimi wasungefika hapo walipo", nk.)

"Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo" (Luka 10:30-37).
Katika mfano huu wa Msamaria (mmataifa) mwema, wakati Kuhani na Mlawi (watumishi wa Bwana) wanapita kando ya JIRANI yao mwenye uhitaji (yamkini wanawahi kwenye huduma makanisani mwao, au wanafuata SHERIA ya kujiepusha na unajisi wa damu imtokayo mtu/majeruhi), ndivyo ilivyo na sisi ambavyo tunawaacha masikini, wajane, na yatima mitaani mwetu wakiwa na njaa, uchi, wagonjwa na wahitaji huku tukikimbilia hekaluni na mahela kumwaga miguuni pa watumishi tukidhani tutapata baraka zaidi!
Usiache kutoa sadaka hekaluni kila ukusanyikapo kuabudu, wala usiende mikono mitupu. Usiache kuwakirimu watumishi wa Mungu na wala usiache wakapungukiwa, LAKINI Kumbuka siku zote, hao wajane, yatima na masikini mlangoni pako, ambao hawana AHADI ya kukupa kwa sadaka zako, wanahusika sana kwa mafanikio yako kuliko hao *wakuuziao* baraka au uponyaji kwa sadaka zako.
Soma Matendo ya mitume mlango wa 10.
Frank P. Seth

Comments