SOMO: KIFO CHA GHAFLA

Na ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA, Ufufuo na uzima.


Tulijifunza kwamba kifo sio tukio bali kina uhai ambao unafanya kazi, hatukuongelea habari ya vifo vya kawaida bali tunaangalia vifo vya kutengenezwa vinavyo wapata watu kabla ya wakati wao.
Tumeona kifo kinaweza kupanda farasi, kifo kina kamba ambazo zinaweza kukuzunguka, tumeona kwamba kuna njia ya kutoka kwenye kifo Zaburi 68:20 inavyosema, tumeona kuna njia ya kuelekea mautini kwenye Mithali 2:18, tuliona pia kila mahali inapotajwa mauti imetajwa na kuzimu, Kwenye Mithali 16:14 tumeona kumbe wapo wajumbe wa mauti.

Kati ya mambo ambayo yametugusa sana tulipojifunza ni kifo kupanda farasi na kuingia ndani ya sufuria, tumeona adui wa mwisho ambaye ataingia kwenye ziwa la moto ni mauti kwahiyo kwasababu hii tukafahamu kwamba kifo sio tukio. Ufunuo 20:14, Pia tuliona kuna ugonjwa wa mauti na ambao sio mauti Yohana 11:4. Sisi tuko juu ya mauti kwa jina la Yesu.
Mungu anaweza kuzuia kifo kisimpate mtu wake mpaka kile alicho mwahidi kitimie kwenye maisha yake, Mfano mzuri ni Simeoni ambaye alizuiliwa na Mungu kwamba hatoona mauti mpaka amwone Bwana Yesu.
Imeandikwa:- Yoshua 14: 6-15 "Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu."
Kalebu aliahidiwa na Mungu kwamba atairithi nchi ya ahadi yeye na watoto wake. Tuone alifanya nini kabla hajairithi hiyo nchi...
Imeandikwa:- Hesabu 13:25 Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi."
Walitumwa watu 12 kuipeleleza nchi na walipofika huko watu 10 walileta habari kwamba nchi ile ni nzuri ina vyakula vingi lakini kuna majitu makubwa mno yanakaa ndani na tukijilinganisha sisi na wao, tunajiona kama mapanzi, lakini akina kalebu walikuja wakawaondoa wasiwasi kwamba japo kuna majitu lakini wataweza kuwapiga na kuichukua ile nchi, Kutokana na zile taarifa za watu 10 watu wakaanza kuhuzunika mioyoni mwao bora warudi Misri jambo lililomfanya Mungu amwambie Musa kwamba atawaangamiza watu wote sababu wamedharau, unapokumbana na magumu leo kumbuka magumu yako yaliyopita ambayo Mungu alikupigania ukapita salama na hili nalo lita pita usikate tamaa kwa jinsi linavyoonekana.
Wana wa Israeli walipoanza kukata tamaa Musa aliingilia kati na kumwomba Bwana awasamehe ndipo Mungu akamjibu hivi.
Imeandikwa:- Hesabu 14:20 "Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa Bwana; kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki."
Inashangaza sana wale walioleta habari halisi walifariki lakini wale walioleta habari za uongo kwa macho ya kibinadamu waliishi. wale kumi walimshangaa kalebu kwa vile alivyosema uongo kwenye habari ya kurithi nchi japo Mungu alitenda maajabu kwenye bahari ya shamu, wao hawakukumbuka mambo yote lakini kina Kalebu waliyakumbuka yale maajabu ya Mungu na wakaongea kwa Imani.
Leo usiogope kwasababu ya mambo yanayokupata kumbuka Mungu kwetu ni Mungu wa kuokoa na njia za kutoka mautini zi na yeye. Mara nyingi unapofika mahali pagumu kumbuka Mungu alipokuokoa kule nyuma atakuokoa na hapo ulipofikia tena. Wanaweza kukuhamisha na kukuweka kwenye milima ili wakupige. Kabla hujasema "siwezi" angalia kule nyuma mambo mangapi yalitokea Mungu akakusaidia ukashinda.
Mungu amesema unapokwenda vitani ukakutana na adui amekuzudi usiogope maana mimi nipo pamoja na wewe. Ukiyaona yaliyo mbele ni magumu kabla hujawaza kumbuka Mungu aliyokupigania. Unaweza kukumbuka ya nyuma ukarudi nyuma zaidi na unaweza kukumbuka ya nyuma ukaenda mbele zaidi.
Wana wa israeli walipovuka mto Jordan Mungu aliwaambia waweke mawe kumi na wawili mtoni ili vizazi vijavyo wakumbuke kwamba wana wa Mungu waliugandisha mto wakavuka. Mungu aliwaambia wana wa Israeli wachote mana kidogo wakaiweke kwenye hekalu la Bwana ili iwe kumbukumbu kwamba Mungu anaweza kulisha wakati wa njaa.
Kalebu aliingia kwenye nchi ya ahadi kama tulivyoona mwanzo, na aliambiwa watakapoingia atapata kile alichoahidiwa na Bwana. Mungu alimwambia kwasababu alileta habari njema yeye na wana wake waliambiwa watapewa ile nchi ya ahadi. lakini wakati huo kalebu yupo kwenye nchi ya ahadi bila kujua. kalebu alijiuliza mbona Yoshua mwenzangu kapata kile alichoahidiwa na Bwana wakati walikuwa wote walioleta habari njema. Kalebu alikua anasubiria bure pasipo kuchukua uamuzi wa kuifuata ahadi aliyoambiwa, baada ya miaka arobaini kalebu alimfuata Yoshua na kumwambia ile nchi ambayo walienda kuipeleleza bado hajaipata hivyo anaomba aende kuimiliki ile nchi kwa kupigana vita na wale manefili waliokuwa wakiishikilia.
Imeandikwa:- Yoshua 14:14 "Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu. Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma."
Tumeona Kalebu alikuwa anaingojea ile nchi ya ahadi kama alivyoambiwa na Bwana bila kupigana na alipofika miaka 85 ndipo alifahamu kwamba anatakiwa kwenda kupigana vita ili amiliki. kalebu aliambiwa atamiliki akiwa ana miaka 40 lakiini alikuja kumiliki akiwa na miaka 85.
Kwa kawaida Mungu akikuahidi jambo, huwa anatunza jambo hilo mpaka litimie, anweza kuifunga mauti. Inawezekana Mungu alikuwa anamwambia kalebu aende kuimiliki nchi yake kwa kupigana vita lakini kalebu hakulitambua hilo ambapo Mungu alimtunza mpaka akiwa na miaka 85 ndipo aliposhtuka na kuamua kupigana na lile kusudi lake likatimia .
"Ukimili unamiliki wewe na watoto wako na inawezekana wewe haumiliki kwasababu Baba yako hakumiliki"
Kalebu alipoona miaka inazidi kwenda aliamua kwenda kwa Yoshua wake akampa ruhusa ya kwenda kupigana ili amiliki. Wewe unatakiwa umfuate Yoshua wako ili akupe ruhusa ukapigane na kumiliki lile uliloahidiwa na Bwana.
Mauti ya kalebu ilishikwa na Mungu ili asife kwasababu alikuwa anaahadi aliyopewa na Bwana hivyo Bwana aliishikilia mauti isimpate mpaka pale atakapoimiliki.
kusudi linalotokana na Ndoto
Kwenye Biblia kuna tafsiri ya ndoto. ndoto ya kuota yale mambo yanayotokana na shughuli za kila siku, kuna ndoto ambazo huwa ni kiashiria cha mambo yale yajayo. Mungu anaweza akakuonyesha kusudi alilokupa kupitia ndoto kama kiashiria cha kutokea siku zijazo. Jukumu lako ni kupigana ili uje uitimize ndoto hiyo, inaweza ikawa ndoto ya kuchunga anisa la maelfu, ndoto ya kusafiri, ndoto ya kupanda cheo, ndoto ya kufanya biashara, ndoto ya uongozi n.k
Unapokuwa huoni yale mambo ambayo Mungu alikuahidi unatakiwa uamke upigane na kuanza kuomba kama ulikuwa haufungi uanze kufunga na kupigana mpaka ile ndoto yako itimie.
Mauti ilifungwa isimguse Kalebu na alichukua hatua kwenda kwa Yoshua na kusudi lake likatimia.

Dunia nzima haijajua kwamba mautini ni ni mahala unaweza kuingia na unaweza kutoka. Kabla Yesu hajarudi mara ya pili na Jehanamu ya moto haijafunguliwa yeyote anaweza kuingia na kutoka mautini. Sisi hatusemi kwamba waliokufa ni wajinga bali tunasema Yesu alikufa mautini akafufuka na anayo nafasi ya kuwafuata walioonewa na kuwekwa mautini akawatoa huko. Yesu alimfuata Lazaro alipokufa siku nne akamwita njoo naye akatoka mautini. Sisi pia tuliomwamini Bwana Yesu tunao uwezo wa kuwaita wote walio mautini wakatoka huko kwa Jina la Yesu.
Kufa ni kuhamishwa kutoka duniani kwenda mbinguni au kuzimu, kila aliyekufa anapatikana ama mbinguni ama kuzimu ama juu ya dari ama kwenye chupa ama shambani, wengine kwenye vibuyu, wengine maofisini, wengine chini ya bahari, wengine maofisini,kila aliyekufa ana patikana kwa jina la Yesu.
Jambo litakaloyaleta mataifa yote Duniani msalabani ni Ufufuo wa wafu sababu leo watu wote wanapambana na kifo bila kupata ufumbuzi.
tulijifunza kwamba kuna mashetani ambayo yanamweka mtu kwenye hali ya kutokuonekana. Watu hao unapokuwa unatembea wanakuona wewe lakini wewe huwaoni. mfano mtu anapoanguka ghafla na kufa anachukuliwa na shetani aliyejigeuza akawa kama huyo.
kuna ulimwengu ambao umewaficha watu waliokufa ambao wanatumika kwenye shughuli za kufanya kazi za watu. Watu hao wanaitwa watu walioibiwa na kutekwa, wamefichwa mashimoni, wamekuwa mawindo lakini sauti ya Ufufuo na Uzima imepatikana na inawarudisha wote.
Hii ndiyo itakayotikisa dunia kwa kuujaza utukufu wa Mungu. alipokufa Bwana Yesu makaburi yalifunguka na wafu walifufuka wakaenda manyumbani mwao, hii inamaana mauti ya Yesu msalabani ndiyo iliyowatoa watu waliokuwa kuzimu wakafufuka. Biblia inasema mauti ikawatoa wafu iliyokuwa imewameza na bahari ikawatoa wafu waliokuwa ndani yake, hii inamaana wafu wanatoka.
Kuna viumbe wanaitwa majini ambao ni malaika wa giza wanaoweza kugeuka na kuwa kitu chochote sababu na wenyewe ni malaika waovu. Mganga wa kienyeji au mchawi anaweza kuyatuma mashetani yaende kwa mtu anayetakiwa achukuliwa msukule, Jini hili linaambiwa liwe na sura ya mtu yule vilevile alivyo. mtu aliyechukuliwa msukule huwa anaakili zilezile lakini hawezi kuuliza maswali wala kuongea huko alikochukuliwa. Watu wengi wanaofanya haya mambo ni wafanya biashara sababu huwatumia kuita wateja kwenye biashara zao na kutumia nyota zao za utajiri.
Imeandikwa:- Ufunuo 18: 11 Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena; bidhaa ya dhahabu, na fedha, na kito chenye thamani, na lulu, na kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na hariri, na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, na kila chombo cha pembe, na kila chombo cha mti wa thamani nyingi, na cha shaba, na cha chuma, na cha marimari; na mdalasini, na iliki, na uvumba, na marhamu, na ubani, na mvinyo, na mafuta ya mzeituni, na unga mzuri, na ngano, na ng'ombe, na kondoo, na farasi, na magari, na miili na roho za wanadamu."
Mtu anayewachukua watu hawa msukule ukimgusa huwa anakuwa ni mkali sana sababu anajua ukiwarudisha watu hao ule utajiri wake alioupata kwa kutumia msukule utaisha na atakuwa masikini, Tunatakiwa tuende mpaka kule ambapo watu wamewekwa msukule na kuwatoa kwa jina la Yesu. Kanisa lina nguvu za ajabu sana, kama likiamua kuishi maisha matakatifu linaweza kutenda matendo makuu ya ajabu ambayo yataitetemesha dunia.
Shetani huwa hawezi kutengeneza kitu ni mwizi, huiba na kutumia mali za watu waliopewa na Mungu ili akatumie kwa shughuli zake, kila mtu amebarikiwa eneo fulani ili kupitia eneo hilo awe tajiri. Mungu amebariki kila mtu kwa eneo lake. Kuna watu wanamacho ya kuona utajiri wamechukuliwa msukule na macho yao yanatumika na mtu fulani kutafutia utajiri sehemu fulani na ukimnyanganya mtu huyo msukule anayetumia macho yake, anafilisika.
Uaweza kumwona mtu anatembea lakini akili yake inatumika mahali au nyota yake inatumika mahali na ameibiwa na kutekwa. kuna jini ambalo hutumiwa na wachawi linajibadilisha na kuvaa sura ya mtu wakati mtu huyo akiwa bado yupo hai. Jini huyo anaweza kutenda kosa la kufungwa jela na akaja akamatwa mtu asiye. ndiomaana kuna watu wengi wapo jela ambao hawajafanya makosa waliyofungwa kwayo. jini hili hutumika mtu akiwa hampendi mtu fulani.
kuna msukule ambao mwanao yupo hai na unamwona lakini siku moja anabadilika na kuanza kufanya vitu vya ajabuajabu kumbe sio yeye wa asili. Mara nyingi wachawi huwa wanafanya hii aina ya msukule sababu anakuwa yupo hai na wewe hujishughukishi na maombi unabaki unasema mwanangu siku hizi amebadilika kumbe sio yeye.Wachawi huwa wanaogopa kuaibika, hutumia kuwachukua watu wa aina hii msukule, ili wasijulikane kwamba wamemchukua msukule.
Wengine wamebarikiwa kwenye vinywa vyao wakisema kitu kinakuwa na utiisho wa kimungu.
Mungu ni Mungu wa kuokoa na kurudisha na njia za kutoka mautini zi na yeye, lazima watu wote walioibiwa warudishwe kwa jina la Yesu.

Comments