SOMO: SABABU ZA KIFO CHA GHAFLA.

NA ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA, UFUFUO MA UZIMA


Biblia inasema Mungu hawezi kutenda jambo bila kuacha maelekezo kwa watu, inakuaje ufariki kabla hujaandaa mambo yako, Mungu alimwambia Hezekia aandae mambo ya nyumbani kwake kabla hajafa, Yesu alisema anaona siku zake zimekaribia, Paulo naye aliona siku zake zimekaribia na akasema amekaribia kumiminwa. Tunajifunza kwamba Mungu anatenda mambo kwa kuwaambia watu wake kwanza.
Kifo sio tukio bali ni roho kamili yenye macho, masikio na akili. Kuna vitu vitano kuhusu kifo au mauti.
1. kifo kinaweza kupanda gari kwenda na mtu.
"Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi." Ufunuo6:8

Yohana ameonyeshwa maono ameona farasi mwenye rangi ya kijivu na juu yake amepanda mauti. Tunaona kifo kinaweza kupanda ndege, gari, baiskeli, pikipiki nk, sio tukio lakini kinaweza kutembea na mtu. Kifo kinaweza kupanda farasi kwenda kuharibu Taifa lakini kimeshashindwa kwa jina la Yesu.
2. kifo kinaweza kuwa ndani ya sufuria/chakula
"Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii. Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua. Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula. Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani." 2 Wafalme 4:38
Hawa wana wa manabii ambao ni watumishi wa Mungu walipiga kelele na kusema kifo kimo sufuriani. Inamaana kifo sio tukio bali ni roho na inaweza kuingia kwenye chakula au maji, kwenye gari, kinaweza kwenda sehemu yeyote na kuingia ndani yake.
3. Kifo kina chanzo chake, kabla Adam na Eva hawajatenda dhambi kifo hakikuwepo, lakini walipotenda dhambi ndio kifo kiliingia duniani
"Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza." 2 Wafalme 2:19
Mtumishi wa Mungu alifika kwenye mji unaoitwa Yeriko na watu wa mji ule wakamwambia maji ya mji huo yanaleta kifo na kuzaa mapooza. Mbuzi wao walikuwa wakinywa maji yale na kuharibu mimba, wanawake kabla watoto tumboni hawajakaribia kukua mimba zao zilikua zinaharibika, mazao yao walipokuwa wakipanda yalikuwa yanaharibika kabla hayajakomaa kwasababu ya maji waliokuwa wanayatumia yalikuwa yana mapooza. Elisha aliwaambia watu wa mji ule wampatie chombo kipya chenye chumvi ndani yake na akaenda mahali ambapo maji yalikuwa yanaanzia na kuyaponya na roho ya mauti ikafutika watu wakastawi na mifugo yao na mazao yao.
4. Kifo kinaweza kupitia dirishani
"Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu." Yeremia 9:21
Mauti inaweza kupanda dirishani na kuingia ndani ikimfuata mtu iliyetumwa imwingie.
5. Mauti inaweza kuzungumza
"Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu." Ayubu 28:22
Mauti ina masikio na inaweza kutumwa iende kwa mtu ikakae nyumbani mwake, mauti inaweza kuingia kwenye taifa ikakaa na kuongoza mambo ya taifa hilo. Kifo sio tukio na siku ya mwisho kitakamatwa na kutupwa motoni.
"Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti." 1wakorintho15:25
"Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake." Mithali 18:21
Mauti ni roho inayoweza kumwingia mtu akafa ghafla.
"Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa." Waebrania 2:14-15

Hofu ya mauti, inaweza kumwingia mtu akapatwa na mauti. unaweza ukaingiwa na wasiwasi wa kufa kabla hujafika miaka hamsini. kuna aina ya uoga wa aina mbalimbali duniani na moja wapo ni hofu ya mauti.
Ukiri
"kwa jina la Yesu nakataa hofu ya mauti"

Mungu hakutupa roho ya uoga bali ametupa roho ya ujasiri na moyo wa kiasi.
Tumeona kifo kinaweza kuwa ndani ya chakula, kinaweza kuzungumza, kinaweza kuingia ndani ya maji, kinaweza kupanda usafiri, kinaweza kuingia ndani ya nyumba kwa kutumwa na mtu fulani. Habari njema ni kwamba Bwana Yesu ameshinda kifo na kuzimu sababu anazo funguo zake.
Binadamu ni kama mashine na kifo kinaweza kutumwa kwake bila yeye kujua. Pia kifo kinaweza kumwingia mtu akamua kujinyonga au kufanya jambo la kuondoa uhai wake bila yeye kujitambua.
Ukiri
"kwa jina la Yesu mahala popote alipotuma mtu roho ya kifo ninaamuru itoke kwa jina la Yesu."

Kifo kinaweza kuingia ndani ya mtu halafu mtu yule akaamua kutembea kwenda mahali akafariki sababu kinamwongoza.
kuna kifo cha wakati wa mtu kuishi duniani ukifikia mwisho, sio kifo hicho tunacho kizungumzia bali ni kifo kinachotumwa na watu kumwingia mtu na kumuua kiakili, kinaingia ndani ya kinywa, unaongea maneno ya kujiangamiza, kinaingia ndani ya tumbo unakosa kizazi, kinaingia ndani ya ndoa ndoa inakufa, kinaingia ndani ya biashara, biashara inakoma, kuna wakati mwingine mauti inaweza kupandwa ndani ya akili ya mtu na kila anachokiwaza kinakuwa hakina maana.

Ukiri:
"kifo chochote kilichopewa siku kinipate ninakifuta kwa jina la Yesu. mimi kwenye kifo cha ghafla simo kwa damu ya Yesu, jini makata, subiani ninawashinda kwa damu ya Yesu."

kifo cha ghafala kinaweza kutumwa kama pepo likamuingia mtu na kukaa ndani yake. kuna watu kifo kimetegwa ndani yao tangu wakiwa tumboni, kimeshindwa kutimia sababu wanakwenda kanisani lakini bado kinakuwa hakijatoa.
kuna watu ambao wanalima shamba lakini hawawezi kula mazao yake, wanachumbia lakini hawawezi kuoa/olewa, wanajaribu kufanya biashara lakini hawawezi kifanikiwa. sababu ya roho ya mauti na kuzimu ipo ndani yao na hawajaweza kuitoa ndiomaana unakuta wanashindwa kufanikiwa na kupiga hatua.
ukiri
"kwa jina la Yesu kama vile Yesu alivyoshinda mauti na mimi leo naishinda mauti kwa jina la Yesu, kwa jina la Yesu mauti iliyopandwa ndani yangu naifuta kwa jina la Yesu"

Nguvu kubwa kuliko zote duniani ni kifo na Bwana Yesu alikuja kutukomboa duniani kwa njia ya mauti na amemharibu mwenye nguvu ya mauti, kifo kilichaharibiwa msalabani na mwenye nguvu ya mauti ameshindwa.
Ukiri:
"kwa njia ya mauti Yesu amemharibu aliyeweka ngvu ya mauti ndani yangu kwa damu ya Yesu"

Damu aliyoimwaga Bwana Yesu akiwa hai inaitwa damu ya ukombozi ndio imetununua na kututoa dhambini na kuingia nuruni, imetutoa kwenye magonjwa na mateso
Aina ya pili ya damu ya Yesu ni ile damu aliyoitoa pamoja na maji ubavuni wakati anakata roho na kwa damu hiyo tumeshinda mauti.
Ukiri
Damu ya Yesu inashinda mauti, kwa damu ya Yesu mauti yeyote iliyopandwa moyoni, akili ni naing'oa kwa damu ya Yesu, nimeshinda mauti kwa jina la Yesu.

AMEN

Comments