SOMO: SIRI YA KIFO CHA GHAFLA

NA ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA


Kutoka 11
Imeandikwa "Bwana akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya "Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa. Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu. Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake. Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri; na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa. Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi Bwana anavyowatenga Wamisri na Waisraeli. Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu. Bwana akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri. Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake."

Musa alimwambia Farao Mungu anataka wape ruhusa Wana wa Israeli waende zao lakini Farao alikataa kuwapa ruhusa. Kutokana na ugumu wa moyo wa Farao Ndipo Mungu akasema atatoka usiku wa manane auwe mzaliwa wa kwanza wa kila kiumbe wa misri lakini kwenye kambi ya wayahudi hawatakufa hata mmoja iwapo watamchinja mwana kondoo na kuinyunyizia damu yake kwenye kila kizingiti cha milango yao. Tunapata picha kumbe Mungu naye anauwa lakini kwa sababu maalum.
Kutoka 12:5-13
"Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri."

Wana wa Israeli walimla mwanakondoo wa Pasaka wakiwa wameshajiandaa kuondoka. Wakati wanamla Mwanakondoo Malaika wa kifo alipita juu akaiona ile damu walioipaka kwenye vizingiti vya milango yao akaacha kuwapiga kwa pigo lile la wamisri.
Kutoka 12: 23-25
Imeandikwa:- "Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi."

Tumeona kwamba Bwana amesema atapita juu aharibu nchi ya Misri lakini si yeye aliye haribu bali alimruhusu mwenye tabia ya kuharibu aharibu nchi hiyo.
Mungu akisha kuonya sana ukazidi kukaidi anauondoa ulinzi wake juu yako na anamruhusu shetani akushambulie huku yeye akikuangalia, anakuwa amemruhusu shetani akuumize mpaka utakapoamua kutubu na kuacha kosa ulilolifanya.
Mungu huuondoa ulinzi wake kwako pale unapokuwa umetenda dhambi. Ukiwa umetenda dhambi unaanza kushambuliwa na magonjwa na matatizo mengi huku balaa na mikosi inakufuata sababu ile neema ya Mungu na ulinzi wake juu yako inakuwa imeondoka mpaka Pale utakapoamua kusema kwamba Mungu nimefahamu mahali nilipokosa naomba msamaha sitarudia tena. Ukishatambua kola sako na kulikiri na kutubu hapo Mungu atakusamehe na kukurudishia ulinzi wake juu yako.
1 Samueli 16: 14,15,16,23
Imeandikwa:- "Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. 23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha."

Hiyo roho mbaya iliyomwingia Sauli haikutoka kwa Mungu moja kwa moja. Ni shetani anakuwa amemfuata Mungu kukushtaki kwamba umetenda dhambi na mshahara wa dhambi ni mauti, kwakua shetani anaijua Biblia hivyo anamwambia Mungu aje kwako maana umemtenda kosa na Mungu anamruhusu na kuuondoa ulinzi wake kwako ndipo mashambulizi yanaanza kukufuata kwenye maisha yako. Unatakiwa uangalie kwenye maisha yako nini umekosea mpaka Mungu aruhusu mabaya yakupate.
Unaweza ukawa unakemea sana, unaomba sana, unafunga na kutoa sadaka sana lakini bado mambo yako hayaendi vizuri kumbe kuna mahali umekosea. Mfano unafanya mapenzi kabla ya ndoa(Unazini) au nje ya ndoa(uzinzi) na unaomba kwa jina la Yesu, unaenda kanisani na kupiga majeshi wakati ni mwenye dhambi, unawasema watu wa Mungu vibaya..nk.
Kuna watu wanasumbuliwa na matatizo kwasababu kuna milango ya dhambi wameifungua kwenye maisha yao na hiyo ndiyo inayowatesa hivyo wanatakiwa wasahihishe na kutubu.
Kama hujamtii Mungu usimwombe kitu mpaka utubu.

Hata kama una maagano ya kifamilia ambayo ni chukizo kwa Mungu unakuwa hutaki kuyaacha, hayo yanaweza kuondoa ulinzi na neema ya Mungu kwenye maisha yako unatakiwa uyaache mara moja kwa jina la Yesu.
Ukiri:
"Kwa jina la Yesu maagano yote ninayoyafuata ninayavunja kwa damu ya Yesu"

hatufanyi dhambi kwasababu ni ngumu kuifanya bali ni kwasababu Mungu amesema tusiifanye.
Imeandikwa:
Malaki 3:10
Imeandikwa "Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi."

Mungu amesema tupeleke zaka nyumbani mwake naye atamkemea yeye alaye na hataharibu mazao ya ardhi wala hayatapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake. Kumbe njia moja wapo ya kupata ulinzi wa mali zetu ni kumtolea Bwana zaka kamili nyumbani mwake.
Unakuta mtu anaomba na kufunga lakini hatoi zaka ghalani mwa Mungu, kwa kufanya hivyo unakuta yule alaye haachi kumfuata kwenye biashara zake, kazi zake, mazao yake na kuyala.
Mungu amesema yeye anipendaye atalishika neno langu na Mimi na Baba tutakuja kwake na kufanya makao.
Siri mojawapo ya Mungu ni kwamba ukimpenda Mungu sana Mungu anakukemea sana pale unapokuwa umekosea. kuna watu ambao wakikosea kidogo tu Mungu anawakemea sana lakini kuna wengine hata wakikosea Mungu hawakemei anawaacha hivyohivyo sababu anawajua hawampendi na ni wakosaji wa kudumu.
1 Wafalme 22: 20 - 22
Imeandikwa "Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo."

Bwana alimtafuta wa kumdanganya mfalme ahabu lakini hakumpata mbinguni sababu kila mmoja alisema kivyake lakini alitokea pepo akasema anaweza kwenda kumdanganya mfalme Ahabu na Mungu alikamfanyia interview kwamba atamdanganyaje na akamruhusu aende kumdanganya. kumbuka Mungu yupo mbinguni na jopo la mbinguni limemzunguka amesema kuna mtu anawatesa sana watu wangu duniani lakini ili mtu huyu afe anatakiwa adanganywe ndipo yule pepo akatokea na kujifanya pepo wa uongo kwenda kumdanganya Ahabu.
Tunajifunza kumbe wakati mwingine shetani anaweza kwenda kutenda jambo fulani kwasababu ameruhusiwa aende.
Kwahiyo tumeona kifo sio tukio bali ni roho ya mauti inayoweza kuruhusiwa.

Ufunuo wa Yohana 6:8
Imeandikwa "Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi."

Hapa tunaongelea kifo cha kutengeneza ambacho kinawapata watu kabla ya wakati ulioamriwa na Bwana.
Ufunuo wa Yohana 1:18
Imeandikwa " nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu."

Akimaanisha anaouwezo wa kuwafungulia watu waliomezwa na mauti na kuhifadhiwa kuzimu wawe huru.
Ufunuo 20:14
Imeandikwa "Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto."

Hii ni maana nyingine kwamba kifo sio tukio, kinaweza kukamatwa na kutupwa kwenye ziwa la moto, kama ilivyoandikwa siku za mwisho mauti na kuzimu itatupwa kwenye shimo la moto.
Ukiri:
"Kwa damu ya Yesu ninatoka ndani ya tumbo la aliyenimezakwa jina la Yesu, mauti tapika biashara yangu uliyoimeza kwa jina la Yesu, Tapika Ujasiri wangu ulioumeza kwa jina la Yesu, tapika elimu yangu, tapika kazi yangu, tapika ndoa yangu, tapika maisha yangu, tapika safari zangu kwa jina la Yesu,"

Ayubu 20:15
Imeandikwa "Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake."

Mithali 7:27
Imeandikwa "Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti."

Wakorintho 15:26
Imeandikwa "Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti."
Daudi mwana wa Yese alitoka vitani, aliporudi nyumbani akakuta wameibiwa vitu vyote na askari wake wakataka kumpiga kwa mawe, ndipo akaamua kumuuliza Bwana kwamba awafuate na atawapata? ndipo Bwana akamjibu kwa dharura akamwambia wafuate na utawapa na kurudisha vyote.

Unatakiwa uache kulia uchukue hatua kuwafuata waliokuibia na utavichukua vyote.
Ukiri:
"Kwa msaada wa Bwana nitatenda mambo makuu maana yeye amewakanyaga watesi watu"

Kifo kwetu sisi tuliookoka tunaita ni kulala mauti. mtu anapolala kwa umri mzuri tunakuwa hatuna shida naye, lakini mtu akifariki kwa kuibiwa na kutekwa huyo tunamrudisha kwa jina la Yesu.
1Wathesalonike 4: 13, 15
Imeandikwa "Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti."

Kwa asili mtu huonekana mwili wake wa nje lakini yeye wa asili aliye ndani yake huwezi kumwona na huyo ndiye anayelala na huyohuyo ndiye huibiwa na kufichwa mashimoni kuwa mateka (Misukule).
Mtu anapokuwa amekufa anakuwa ametoka nje ya mwili na kujiona yuko nje ya mwili wake na huwaona malaika ambao huwakumbuka kama alishawahi kuwa pamoja nao zamani. kulala kwetu sisi watakatifu ni kitendo cha kuhama kutoka duniani na kurudi mbinguni, ni zawadi ambayo tunakuwa tumeisubiria inakuwa imewadia kwa wakati uliopangwa na Bwana.
Nini kinatokea wakati wa kufa ukifika.?
Luka 16:19
"Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa."

Kwa wenye dhambi ambao hawajaokoka mtu ukiwa unataka kufa dakika chache kabla hujafa macho yako ya rohoni yanafunguliwa unaona mahali unapokwenda na wengine wakiyaona midomo yao inafungwa wasiseme kile wanachokiona sababu mashetani yanakuwa yanamfuata kumchukua akiyaona, mtu huyu wakati mwingine anapiga mateke na kuhangaika ili arudi duniani na kuwakwepa mashetani yale. mashetani hayo yanamchukua mtu huyo na kwenda naye kuzimu.
kuzimu ni mahali ambapo wanawekwa watu walikuofa kwa dhambi, Imeandikwa Jehanamu imeandaliwa kwaajili ya shetani tu na sio wanadamu, na mbinguni wataingia watu wengi sana wa lugha zote na rangi zote.
Mungu hapendi hata mtu mmoja apotee bali watu wote waokolewe, Neema ya Mungu iwaokoao wanadamu wote imefunguliwa, Hapo kwanza Mungu alijifanya kwamba haoni lakini sasa anataka watu wote waokolewe. Hii ni saa ya Ufufuo na Uzima Duniani.
Mlokole anapokufa na yeye anakuwa hasikii maumivu ya uchungu wa mauti (Bwana Yesu alipata maumivu ya mauti msalabani ili sisi tumwaminiye tusipate maumivu hayo). Mtu huyo anakuwa anawaona malaika watakatifu wanakuja kumchukua na kusikia vinanda na nyimbo nzuri zikiimbwa, anakuwa anaiona mbingu nzima ndio maana mtu wa Mungu anapokuwa anafariki(analala) huwa anapata afya na nafuu nzuri kama alikuwa anaumwa na baada ya hapo hufariki kimya bila kuhangaika.
Kifo cha kutengenezwa huwapata watu kwa njia ya Hofu ya mauti kifo kiwachukue watu kiurahisi kwasababu ya hofu zao.
Waebrania 2:15
Imeandikwa "Awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa."

Ukiri:
katika jina la Yesu nabatilisha hofu ya mauti juu yangu, mauti ya aina yeyote niliyotegewa naibatilisha kwa jina la Yesu, mauti ya biashara iliyopandwa kwangu naibatishisha kwa jina la Yesu"

2Timotheo 1:10
Imeandikwa "na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili"

ndugu zetu waislam wanakiita kifo ni roho Israeli sababu wanamwogopa Mungu wa Israeli kwasababu ya mambo ambayo waisraeli waliwafanyia kwenye vita walizopigana mpaka wameamua kuita kifo roho israeli. pia waarabu wanakiita kifo ni jini makata (muuwaji).
""Kwa jina la Yesu mauti iliyoshikilia biashara, ndoa, kazi, naishinda kwa jina la Yesu. Mambo yote yanawezekana kama ukishinda hofu ya kifo"
Roho kubwa mbili ambazo zinawazuia watu ni mauti na kuzimu. kazi ya mauti ni kuuwa watu na kazi ya kuzimu ni kuwatunza waliouwawa na mauti.
Samsoni alikuwa na nguvu akakatwa na kufanyishwa kazi ya kusaga ngano, ndivyo lilivyo kanisa la sasa na la zamani sababu kanisa la zamani lilikuwa na nguvu na miujiza ya kupita kawaida lakini kanisa la sasahivi imefanywa kama maudhurio ya kila siku bila kuwepo nguvu za Mungu au limebakia na nguvu za kutoa pepo tu bila kuponya wagonjwa na kufufua wafu. lakini saa imewadia ambapo kanisa la Mungu limesimama imara na kufanya mambo makubwa na ya ajabu kupita akili za wanadamu kwasababu mauti na kuzimu tayari zimeshakamatwa na kufungwa, kazi moja iliyobaki ni kuwarudisha wote walioibiwa kwa jina la Yesu Kristo. Amen
"HII NI SAA YA UFUFUO NA UZIMA DUNIANI"

Comments