Somo:Usikurupuke kuoa au kuolewa, ukawa mtu wa Jahanum



Na Mtumishi Abel Shiliwa
"Usikurupuke kuoa au kuolewa, ukawa mtu wa Jahanum"
Najua wengi mnaweza kujiuliza, inakuwaje tendo la ndoa, ambalo Ni Takatifu lilioanzishwa na Mungu mwenyewe, liwe sababu ya watu kwenda Jahanum?

Naam kuoa au kuolewa, kunaweza kukupeleka motoni, kama Yesu asemavyo

Marko 10:11 Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

Katika andiko hilo, pameonyesha kwamba, mume akimuacha mkewe na kuoa mwanamke mwingine Azini, na mke pia akimuacha mumewe na kuolewa na mwanaume mwingine, Anazini.

Katika Mathayo Yesu akaanisha zaidi aliposema.
Mathayo 19:9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. 

Hapo Yesu anasema:- Mwanaume kama atamuacha mkewe bila chanzo cha Uasherati, akaoa mwanamke mwingine, hapo anakuwa anazini, na yule atakae muoa yule mwanamke nae pia anazini, na ikumbukwe katika Marko imesema, Mwanamke nae akiolewa na mwanaume mwingine, nae pia anazini, kwa hivyo panakuwa na wazinzi wanne.
1. Mume aliyemuacha mkewe.
2. Mke aliyeachwa, au aliyemuacha mumewe.
3. Mwanamke aliyeolewa na mume aliyemuacha mumewe, au aliyeachwa na mkewe.
4. Mwanaume aliyemuoa mwanamke aliyeachwa au kumuacha Mumewe.

Ndiyo maana Wanafunzi wa Yesu, wakasema kama ikiwa mambo ya mume na mke yapo hivyo, basi haifai kuoa, maana waliona ugumu wa kukurupuka, wakaona ni afadhali ukae bila ndoa, kuliko kudumbukia kwenye shimo la uzinzi.

Na Kibiblia Wazinzi Mbinguni hawaendi, sasa kabla hujaamua kuingia kwenye ndoa, kwanza Fanya uchunguzi, uelewe, huyo anaekuoa, au unaemuoa, aliwahi kuwa katika ndoa? Kama ndivyo, huyo mwanaume au mwanamke yu hai? Kama wapo hai, Usiingie kwenye ndoa, maana kama mwanamke ameachana na mumewe, na mumewe yu hai, mwanamke huyo hana ruhusa ya kuolewa na mwanaume ye yote.

1 Korintho 7:39 Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu. 
Sasa wewe mwanaume, ukimuoa mwanamke huyo aliyefungwa kwa sababu mumewe yu hai, basi wewe uoae na huyo umuoae nyote mnakuwa Wazinzi, hata kama ndoa yao imevunjwa na Mahakama, haimaanishi kwamba, inakupa kibali cha kumuoa, au kuolewa na mwanaume huyo, Hakimu ni mwanadamu tu ambae hana mamlaka ya kuitenganisha ndoa ambayo imeunganishwa na Mungu mwenyewe.

Mathayo 19:6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
Hata kama imetokea Mahakama imebatilisha ndoa ile kwa sababu ya Cheti cha ndoa, bado kwa Mungu inahesabiwa kuwa ndoa halali, Mke hana ruhusa ya kuolewa, wala mwanaume hana ruhusa ya kuoa mke mwingine.
1 Korintho 7:10 Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;
11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.

Sasa usikurupuke ndugu yangu, badala ya kwenda mbinguni ukaenda Jahanum kwa sababu ya dhambi ya Uzinzi, wewe unaweza kuwa unajizuia kuchepuka, ukiogopa uzinzi katika ndoa yako, na kumbe huyo unaeishi nae ni mzinzi mwenzio.

WAzinzi mbinguni hawaendi! Hata kama hapo ulipo unajiona kwamba, upo katika ndoa, anza kufanya uchunguzi, ujue, huyo ulienae nae, ni mke au mume wa mtu? Ukibaini chukua hatua.
Na kama bado hujaoa au kuolewa, fanya uchunguzi mpaka uhakikishe kwamba unaenda kwenye ndoa Salama! maana mwingine anakimbia kwa mumewe Mtwara, anakuja Dar anajifanya hajaolewa, au mwanaume anamkimbia mkewe kutoka mkoa fulani na kuhamia mkoa fulani, anakuongopea kuwa hajaoa, unauvaa Mkenge, mnakuwa Wazinzi, na MWISHO mnaenda motoni.

Comments