UACHE MABAYA UKATENDE MEMA

Na Mtumishi Peter Mabula.
 BWANA YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
karibu tujifunze neno hai la MUNGU aliye hai.

Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''

Ni agizo la MUNGU kwamba kila mwanadamu aache mabaya na atende mema siku zote.
Kinyume cha mema ni mabaya.
Kama mtu hatendi mema basi huyo atakuwa anatenda mabaya.
MUNGU kupitia neno lake anatutaka wanadamu wote kuacha mabaya na kuanza kutenda mema.
Huu ni ujumbe niliopewa leo ili nimwambie kila mtu kupitia somo hili muhimu kabisa.

Zaburi 37:3 '' Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. ''
BWANA YESU anapendezwa na mema ya wateule wake.
BWANA anataka tuishi maisha mema yanayoambana na matendo mema tu.
Kuna watu huchanganya matendo mema na mabaya kwa wakati mmoja na kudhani kwamba wao wana nafuu fulani mbele za MUNGU, kumbe hapana nafuu yeyote maana MUNGU anataka tutende mema tu na sio michangayo.
Mtu akiyachanganya matendo mema na mabaya katika maisha yake inatakiwa ajue kabisa kwamba Matendo yake mema hayatakuwa na faida kwake  kama mema hayo yanafanyika kwa kuunganishwa na matendo mabaya, matendo mabaya yana hasara kubwa hata kama yamechanganyikana na matendo mema kidogo, hasara kubwa zaidi ya matendo mabaya ni ziwa la moto.
Matendo mabaya ni mengi na yote hayatakiwi kutendwa na mwanadamu.

Mithali 3:29 ''Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.''

=Matendo mema ni yapi?
Matendo mema yanaanza kipindi mtu anapompokea YESU KRISTO kama mkombozi wake kisha mtu huyo anaanza kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na MUNGU kupitia neno lake hai Biblia takatifu.

=Matendo mabaya ni yapi?
Matendo mabaya ni yale yote ambayo MUNGU kupitia Biblia takatifu anayakataza.

Matendo mabaya hayatakiwi kutendwa na mteule wa KRISTO.
Uwe unayajua matendo mabaya au huyajui lakini ukiyatenda bado hayo yatahesabika ni mabaya mbele za MUNGU.

Amosi 5:15 ''Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, MUNGU wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.''

Kuisoma Biblia ili ujue MUNGU hataki nini na anataka nini ni jambo jema na ni jambo la lazima kwa kila mtu, maana ukitenda mabaya hata kama hujui kama ni mabaya bado hayo mabaya yatabaki kuwa ni mabaya tu.
-Kusudi la MUNGU kwa mwanadamu  lote liko katika Biblia.
-Mpango wa MUNGU kwa mwanadamu ; jinsi ya kuishi na kutenda, vyote viko katika Neno lake Biblia.

Mika 2:1 ''Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. ''

FAIDA SABA(7) ZA MATENDO MEMA.

 1.  Uzima wa milele.
 2.  Kukubaliwa na MUNGU.
 3.  Kumpendeza MUNGU
 4.  Kuwa mwenye haki mbele za MUNGU.
 5.  Kutumiwa na MUNGU kihuduma.
 6.  ROHO wa MUNGU kuwa ndani yako.
 7.  Utakuwa mwanafunzi wa Kweli wa YESU KRISTO.

HASARA SABA(7) ZA MATENDO MABAYA YASIYOTUBIWA.

1. Jehanamu ya milele.
2. Kuwa upande wa shetani na sio wa MUNGU.
3.Kukataliwa mbele za MUNGU.
4. Kuteswa na kutawaliwa na nguvu za giza katika maisha yako.
5. Kujitenga na uzima wa Milele.
6. Kujitenga na kusudi jema la MUNGU kwa maisha yako ya duniani.
7.Kuwa mtumwa wa dhambi zinazozaa mauti.
-Mfano; 
Anayefanya dhambi ya uasherati  na uzinzi anaweza kupata ukimwi na kufa mapema kinyume na wakati wa MUNGU kwake.
Mwizi anaweza kuiba na kukamatwa na kuuawa na wananchi wenye hasira kali hivyo dhambi yake ya wizi inakuwa imezaa mauti. hiyo ni mifano michache katika ile mingi ambayo dhambi huzaa mauti mapema kinyume na mpango wa MUNGU.

Yohana 3:16-21 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee(YESU), ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.'' 

Neno la MUNGU linamkataza kila mwanadamu kufanya matendo mabaya na linamtaka kutenda mema tu siku zote.

-Kwa mema tu ndani ya Wokovu mtu atalipwa uzima wa milele.

-Kwa mema tu mtu atabarikiwa na BWANA.

Matendo mabaya yote yanaitwa dhambi.
-Dhambi ni uasi kwa MUNGU .
-Watenda dhambi hawana nafasi hata moja  katika ufalme wa MUNGU.
-Watenda dhambi hawana nafasi hata moja katika uzima wa milele wa KRISTO YESU.
Dawa ni kutubu na kuacha dhambi zote hata kama ulizipenda kiasi gani.

Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''

Hakuna dawa ya dhambi ila ni kumpokea YESU na kutubu.
-Dhambi haifai na ni mbaya sana.
-Dhambi ni barabara pana  sana lakini inaelekea jehanamu.

Neno la MUNGU leo linatuambia tuache mabaya na tutende mema tu.

Warumi 12:17-21 ''Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.''


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments