ANGALIA MWISHO!

Na Frank P. Seth.

"11Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. 12Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote, (Yeremia 29:11-13).
Pamoja na kwamba unapita mahali pagumu sasa, mawazo ya Mungu sio wewe uangamie ila kuna jambo JEMA mbele yako. Usikate tamaa. 

Fikiri habari za Yusufu na Mariam, wazazi wa Yesu huku duniani; wanakwenda safari yao na mama anapata uchungu wakiwa safarini. Wanakosa mahali pa kulala (hoteli nzuri) wanaishia kulala kwenye banda la ng'ombe. 

Kwa hali ya kawaida, huyu mama (Mariamu) angeanza kumlaumu mumewe kwamba anafanya mambo bila utaratibu mzuri hata anapata shida yote hiyo. Labda hata anaweza kuwaza haikuwa mpango wa Mungu kuolewa na Yusufu maana mambo yake yanaenda kombo tu. Hajui hata itakuwaje maisha yake kama mume mwenyewe hata kupanga safari vizuri hajui, nk.
Sasa angalia tena upande wa pili. Mungu ameandaa jeshi la malaika huko mbinguni na kuna kundi la Mamajusi wako njiani wanataarifa kwamba Mfalme amezaliwa. Mamajusi wanakuja na zawadi zao mkononi. Yamkini huku moyoni Yusufu anakemea mpango wa adui. Labda kuna hatari ya mtoto kufa kwa maana ilikuwa ni majira ya baridi (winter), kumbe hajui, katika HAYO YOTE Mungu alikuwepo!

Hakuna mahali utasogea hatua bila gharama kutumika, aidha utembee au ulipe gharama ya usafiri fulani, lazima gharama ipo amasivyo utabaki ulipo tu. Ukiona mtu anataka kupanda tu, kusogea hatua tu, na hataki kabisa kuhesabu au kulipa gharama, mwangalie tena, hataweza kuishi hizo baraka hata akizipata kwa maana safari ni maandalizi ya kumwezesha mtu kumudu kitakachozaliwa mbele. Usiangalie shida za safarini, angalia mbele unakokwenda. 

Siku zote kumbuka, BWANA hakutuahidi njia laini tu, wala wepesi wa safari. BWANA amesema habari ya wembamba wa njia na kusonga kwakwe. Kuona hiyo njia ni shida achilia mbali kuipita; lakini huko mbele kuna Uzima wa milele na mambo mengi mazuri tu. Angalia mbele!

Mambo unayopitia ni maandalizi ya mambo mazuri mbele yako, jipe moyo mkuu. Mungu anakuwazia mema na wala hataacha mguu wako usogezwe. Jina lake ni MLINZI wa Israel, hatasinzia wala hatalala mchana na usiku. AMEN.
Frank P. Seth.

Comments