![]() |
Askofu Boniface Kwangu |
Askofu huyo ni wa pili kutimuliwa na uongozi wa kanisa hilo baada ya mwaka 2007 aliyekuwa Askofu wa dayosisi hiyo, John Changae na yeye kufukuzwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kitendo ambacho kinaonesha taswira mbaya kwenye kanisa hilo.
Pia Askofu Kwangu aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi
cha miaka minane, katika uongozi wake alishawahi kutuhumiwa na waumini
wake kuwa anajihusisha na dini ya Freemasons huku wengine walikuwa
wakimtuhumu kwamba anatumia nguvu za giza.
Askofu Kwangu na wenzake wanne wanatuhumiwa na kanisa hilo
kwa ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni pamoja na kuendesha kanisa
hilo bila kufuata kanuni na taratibu za kanisa hilo kitendo ambacho
kimesababisha kutimuliwa kwake.
Askofu Kwangu, anatuhumiwa na upotevu wa Sh. 500 milioni ya
shule ya kimataifa ya Isamilo, kuuza gari la dayosisi hiyo, kufukuza
wafanyakazi wa kanisa hilo na kusababisha wadaiwe Sh. 60 milioni,
kujipatia kiasi cha zaidi ya Sh. 15 milioni kutoka kwa Mhasibu wa
kanisa, Sam Wisa, bila kibali.
Akisoma tamko la kumfukuza kazi, Mwenyekiti wa Nyumba ya
Wadumu kutoka DVN, Andrew Kashilimu, amesema askofu huyo ameisababishia
hasara kanisa hilo zaidi ya Sh. 600 milioni, kutokana na kufanya kazi
bila kufuata kanuni na taratibu.
Amesema kuwa askofu Kwangu amekiuka viapo vya uaskofu,
katiba ya jimbo, katiba ya DVN na amekiuka maadili na kanuni, kuendekeza
matabaka ndani ya wahudumu na waumini, kutoa ajira ndani ya DVN kinyume
na taratibu za kanisa.
Amesema katika kikao kilichoketi Septemba 1 mwaka jana,
kilithibitisha mambo hayo na kukubaliana kwamba Askofu huyo ajiuzulu kwa
afya ya kanisa la Mungu lakini alikaidi maagizo hayo mpaka kutoka kwa
tamko hilo.
“Askofu (Boniphace Kwangu) ametumia vibaya madaraka yake na
alikuwa anatumia vibaya mali na fedha za kanisa, kwa hali hiyo
tusingeweza kuwa na kiongozi wa namna hiyo,” amesema Kashilimu.
Mmoja wa waumini ambaye alikubwa na fagio la Askofu,
Kwangu, Edwar Kibiti, amesema kwamba kutimuliwa kwa kiongozi huyo wa
kiroho katika kanisa hilo kutasaidia kurudisha matumaini kwa waumini
walio wengi.
Kibiti ambaye pia ni Mchungaji amesema kuwa walipokuwa
wakijaribu kuhoji sababu za Askofu Kwangu kuuza mali za kanisa ikiwamo
gari alilochangiwa na waumini alikuwa akiwafukuza watu waliotaka
kufahamu suala hilo.
“Tulipokuwa tunahoji matumizi ya mali za kanisa tulichokuwa
tukiambulia ni kwenda polisi na wengine wafukuzwa, huyu (Askofu
Boniphace Kwangu) alikuwa anafanya kazi kwa majungu na mpaka anaondoka
alishafukuzwa wachungaji 19,” amesema Kibiti.
Amesema kuwa baada ya askofu huyo kuona wachungaji wazawa
wanaanza kumfuatilia alianza kutafuta wachungaji wengine kutoka nchini
mbalimbali hususani ni kutoka Rwanda, ili kuficha maovu yake
anayoyafanya.
Mmoja wa Waumini, Joycelyn Juma, amesema kilichomghalimu
askofu huyo ni upungufu wa mambo ya kiuongozi ambayo yamechangia
kusababisha kuwepo kwa mwanya wa wizi wa mali na fedha za kanisa hilo.
“Kiufupi nimefurahi sana kwa sababu mambo ya ufisadi ama
wizi wa fedha haviendani na mambo ya Mungu na nimefurahi kuona suala
hili limefikia mwisho na sasa tutakuwa na amani,” amesema Juma.
Sanjali na kufukuzwa kazi ya Uaskofu DVN, pia uongozi wa
kanisa hilo limemfungulia kesi Askofu Kwangu na wenzake wanne, Katibu wa
Bodi, James Mtaritinya, Mhasibu wa Shule ya Isamilo, Sam Wisa, Samson
Maganga na John Magawa.
Kesi iliyofunguli ni Januari 10 mwaka huu, Mw/Rb/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa.
Comments