BAADA YA SIKU NYINGI!

Na Frank P. Seth

“BWANA akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. 2Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni. 3Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, 4Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. 5Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru. 6Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. 7Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote. 8Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, 9BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. 10Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote. 11Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia” (Yeremia 13:1-11).
Mungu aliamua kuonesha aonacho kwa watu wake BAADA ya SIKU NYINGI, ndipo akatumia mshipi/mkanda kama mfano. Kama alivyojifunga kiunoni mwake mshipi mpya, na kuona fahari yake, huku mshipi ukiwa umeshikilia vizuri kiunoni na akiusikia, ndivyo ilivyokuwa watu wake. Nini kimetokea baada ya miaka mingi? Mshipi UMEHARIBIKA na HAUFAI KWA LOLOTE!
Kama kuna jambo linanipa changamoto sana ni kitu kinaitwa UPENDO WA KWANZA! Laiti ningeweza kuishi upendo wa kwanza katika mambo yangu yote; kila jambo lingekuwa na thamani yake ileile. Baada ya miaka mingi, KILA kitu kimepungua thamani na uzito wake, ikiwemo na UHUSIANO na Mungu! Je! Umeona hilo na likakupa changamoto? Weka mikakati mwaka huu ya kurejesha THAMANI ya mambo yako ya muhimu ikiwemo na UHUSIANO wako na Mungu. 

Utapimaje kama umepungua au thamani ya mambo yako ya muhimu imeshuka? Angalia mambo haya:

1. MSUKUMO wa ndani wa kufanya yale mambo.

2. Kiwango cha FURAHA unachopata ndani yako ukifanya hayo mambo.


3. Ukipata UGUMU wakati wa kufanya hayo mambo, ustahimilivu wako ukoje sasa ukilinganisha na zamani?


4. Unatumia MUDA gani kufanya hayo mambo?


5. Katika KUWAZA au KUTAFAKARI, ni mara ngapi kwa siku unawaza/tafakari hayo mambo?


6. Unajisikiaje ukiambiwa UACHE kufanya hayo mambo? (linganisha reaction yako ya sasa na ile uliyokuwanayo mwanzo).


7. Ukiona mtu aliyekuwa anafanya kama wewe hapo MWANZO na sasa hafanyi tena (amerudi nyuma), unajisikiaje?


8. UKITOA pesa au MUDA wa kufanya yale mambo unajisikiaje?


9. MAZUNGUMZO yako yakoje kuhusu hayo mambo? (Linganisha zamani na sasa).


10. Nguvu yako ya kushawishi wengine wawe kama wewe (wafuate njia yako) imepungua kwa kiasi gani?


Kumbuka hayo mambo ni pamoja na uhusiano wako na Mungu. Ukiweza kujibu maswali hayo kumi, utajua thamani ya wewe kama MKANDA/MSHIPI mikononi mwa mwingine.
Frank P. Seth

Comments