DAWA IKO ULIMINI

Na Frank P. Seth.

“Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu. Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vyawapumbavu humwaga upumbavu. Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema. Ulimi safi ni mti wa uzima;Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo” (Mithali 15:1-4).

Ni kweli tumeambiwa "Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu" (Wafilipi 4:6). Lakini umejiuliza gharama unazolipa sasa zimekuja ni kwa sababu huombi au kwa sababu UMEHARIBU mwenyewe kwa UKOROFI wako (maneno na matendo yako kwa wengine)? Kwani hujui kwamba "Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake"? (Mithali 18:20).

Nimewaona watu wakiTUKANA au KUHARIBU kwa ndimi zao kisha kukimbilia kwa Mungu kuomba MSAADA bila kujali KUTENGENEZA walikoharibu wakidhani Mungu atawatengenezea! Ukiharibu, jifunze kutengeneza, na ndipo umuhimu wa neno, "Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao" (Waebrania 12:14) unakuja.

Unataka kumwona Bwana akikuinua hatua zingine? Basi tafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote (wajibika ipoasavyo kijamii) na sio unafanya FUJO halafu unajifungia chumbani na kuanza kukemea kwa Jina la Yesu, ukidhani kwa MAOMBI yako Mungu atawafunga watu lijamu kama punda ili wazidi tu kukutumikia wakati unawavuruga! Kaa kwa akili na adabu, utaona matunda yake. Ukiwa KOROFI, utaishi kwa maumivu mengi.
Kama tu SADAKA yako haikusaidii kumaliza mambo yako na jirani yako hadi ukapatane naye KWANZA; na BWANA Yesu anakushauri kabisa, acha kutoa sadaka, nenda kafanye SULUHU na jirani yako ndio uje KUTOA sadaka zako (Mathayo 5:23-26), sembuse maombi tu? Kwamba utaomba tu halafu basi! Acha kujifariji, umeharibu mahali kwa KINYWA chako? Katengeneze huko na sio kumkimbilia Mungu ukidhani umemaliza. Acha kiburi, omba msamaha na utaona Mungu akiingilia kati na kunyoosha mambo hata kama msamaha wako umekataliwa, wewe omba kwa dhati tu na utaona utakavyopata amani ya kusonga mbele.
Kwani hujui kwamba imeandikwa, "25Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ 26Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]" (Marko 11:25-26). Yaani hakuna namna UTAMVURUGA mtu halafu ukasema nitaenda kumaliza/kuzungumza na Mungu wakati hujatengeneza. Acha hiyo short-cut, omba msamaha na samehe wenzako ndipo uingine kwenye MAOMBI yako, kinyume na hapo, kama unaona shida, anza kushughulikia KIBURI ndani yako kwanza kwa sababu mara nyingi kinachokusumbua usiombe msamaha ni kiburi tu.
Soma:

"23Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, 24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. 25Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. 26Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho" (Mathayo 5:23-26).

Frank P. Seth.

Comments