HAIWEZEKANI KUINGIA UZIMA WA MILELE BILA YESU KRISTO

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu huambiwa waokoke lakini hukataa bila sababu zozote.
Ingawa wanajua bila wokovu wa KRISTO hakuna uzima wa milele.
Kuna watu hukataa kuokoka kwa sababu tu ya kuwaridhisha wazazi wao.
Ukweli ni huu Sio Lazima Kumpokea YESU Lakini Haiwezekani Kuingia Uzima Wa Milele Bila Yeye.

Yohana 14:6 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. ''

Tangazo hilo la BWANA YESU katika Yohana 14:6 ni ukweli wa milele ambao wanadamu hawatakiwi kuwa na maono bali kuushika na kuutii.
Kila aliye mbinguni anajua kwamba nje na YESU KRISTO hakuna uzima wa milele.
Kila aliye kuzimu anajua kwamba bila YESU KRISTO hakuna uzima wa milele.
shetani na malaika zake wote wanajua kwamba bila YESU KRISTO hakuna uzima wa milele ndio maana wanafanya juhudi kila siku ili kuhakikisha wanadamu hawaingii uzima wa milele ambao wao waliukosa kwa sababu ya uasi wao.
Malaika wote mbinguni wanajua kwamba bila YESU KRISTO hakuna mwanadamu hata mmoja atakayeingia uzima wa milele.

Watakatifu wote waliokufa kabla ya BWANA YESU hajaja duniani miaka 2000 iliyopita walipata Neema ya kuhamishwa kutoka kwenye makazi manyonge na sasa wako mbinguni wakifurahi na BWANA.
 Mathayo 27:52-53 '' makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.''

Kitendo cha BWANA YESU mwili wake wa duniani kutengana na roho yake yenye utukufu kulipelekea Watakatifu waliofariki zamani kuhamishwa kutoka Kaburini na kupelekwa mji mtakatifu ambao ni mbinguni kwa MUNGU. Hivyo watakatifu walifariki kabla ya kuja kwa BWANA YESU mara ya kwanza wako mbinguni.
Watakatifu wote waliofariki baada ya Kalvari sana wako mbinguni wakifurahi kwa BWANA.
Watakatifu ni wale tu waliompokea BWANA YESU na kuishi maisha matakatifu siku zao za kuishi duniani. Wakimaliza safari duniani huenda mbinguni katika eneo la kungojea Siku ile kuu.
Mtume Paulo kwa sababu ya kulijua hilo la watakatifu kwenda  mbinguni kuna sehemu anasema kwamba anatamani ajumuike mbinguni na BWANA YESU ila bado hajaimaliza kazi. 
Ni muhimu sana kuokoka na kuishi maisha matakatifu ili baada ya kifo iwe mbinguni na sio kuzimu.

Watu huokokaje?
Biblia iko wazi ikisema 
'' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni BWANA wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka. -
Warumi 10:9-13''

Nje na KRISTO hakuna uzima wa milele maana wokovu wa MUNGU haukuja kwa njia nyingine yeyote ila njia ya YESU KRISTO.

Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ''

 Ndio maana Biblia iko wazi sana ikisema kwamba BWANA YESU akikuweka huru unakuwa huru kweli kweli.
Uhuru wa BWANA YESU unapatikana pale tunapompokea na majina yetu yanaandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni.

 Yohana 8:36 '' Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. ''


Jambo jingine la muhimu kila mwanadamu kujua ni hili.
Kila kitu katika ulimwengu ujao ni cha milele, Lakini kila kitu katika ulimwengu huu kitaisha.

2 Kor 4:18 '' tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. ''

Biblia inatoa ushauri mzuri sana kwamba ni muhimu sana kila mtu aangalie visivyoonekana yaani vya ulimwengu ujao katika uzima wa milele.
-Kuna watu wanaangalia mambo haya tu yanayoonekana hadi kwa hayo wamedumaa kiroho.
-Kuna watu wanataka mafanikio ya maisha haya lakini hawataki wala hawatafuti mafanikio ya maisha yajayo.
Ndugu zangu, naomba tujue kwamba;
=Ujana huisha.
=Uzuri huisha.
=Ajira hufika mwisho.
Hivyo vyote ni vitu vinavyoonekana na hatuhitaji kuvitumainia hivyo maana vyote vinavyoonekana vina mwisho.
Ni heri tushughulike na visivyoo
nekana sasa lakini vipo na hivyo ni uzima wa milele kupitia YESU KRISTO.


Biblia inatushauri hivi;
''Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.-Mathayo 6:33''


Njia ya utakatifu watapita wasafirio kwenda mbinguni pekee.
Msafiri ana tabia ya kujiandaa kwa ajili ya safari.
Msafiri husafiri kuelekea kule alipochagua kwenda.
Msafiri hudharau dharula zote ambazo zinaweza kufuta safari yake.
Wasafiri wa mbinguni huyahesabu sio kitu yote yanayoonekana ambayo kama wakiyafuata yanaweza kufuta safari yao ya mbinguni.
Wasafiri wa mbinguni ni waliookoka, wameokolewa na BWANA YESU. Japokuwa ulimwengu unaweza kuwaona washamba au waliopitwa na wakati lakini wao mambo hayo hayawezi kufuta safari yao ya kwenda mbinguni uzima wa milele. 
Wasafiri wa mbinguni hawatapotea kamwe maana wako na BWANA YESU, Duniani wanaweza wakaonekana washamba, wamepitwa na wakati au wanaweza wakaonekana kama wamepotea lakini hakika hawajapotea maana ROHO MTAKATIFU yu pamoja nao hadi uzima wa milele.
Tumefanyika wateule wa KRISTO kwa neema ya MUNGU hivyo ni lazima tuendelee na safari yetu ya kwenda mbinguni.
 Tunaye BWANA YESU na tumehakikika maana ni kamanda wetu na tutashinda vita vyote.

 1 Yohana 5:11-13 '' Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe(YESU KRISTO).
Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.''


 Wateule nakuomba tusonge mbele na BWANA YESU.
Hakuna haja ya kurudi nyuma tena sababu yale tumeshinda ndio mengi kuliko yale tunayo yaishi sasa
Wana wa MUNGU Tusongeni mbele sanaa


Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu. '' 

MUNGU wa mbinguni akubariki kwa kunisikiliza kwa njia ya maandishi.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments