ILI KUJENGA na KUPANDA (1)

Na Frank P. Seth
"Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda" (Yeremia 1:9, 10).

Mwaka huu 2016 unapoanza, watu wengi sana wameweka maazimio ya kubadilika au kufanya mambo fulani mapya au kuendeleza mambo fulani lakini kwa kasi na ari mpya. Umewahi kujiuliza ni kwanini sio wengi sana watafanikisha malengo yao? Ni asilimia kidunchu tu ya watu wanaopanga huweza kufanikisha mambo YOTE sawa na mipango yao, wengi sana huishia kupanga. Umejiuliza ni kwanini?

Nataka ujifunze mambo matatu katika kitabu cha Yeremia. Kwanza kuna NENO ambalo Mungu huliangalia juu yako ili ATIMIZE malengo yako. Je! Unalijua? Hili ni kusudi la Mungu kwa maisha yako. Kisha imekupasa kujua kwamba Mungu hutenda au kuumba mambo kwa Neno lake.

Pili, kuna hatua ya msingi ya KUBOMOA, KUNG'OA, KUHARIBU na KUANGAMIZA mambo fulani katika maisha yako au mahali unapotaka kufanya mabadiliko. Uko tayari kupata hasara? Uko tayari kulipa gharama katika kuangamiza?
Na, tatu, kuna hatua ya muhimu ya KUJENGA na KUPANDA. Sasa usidhani kujenga na kupanda ni maneno sawa, au yametumika kwa bahati mbaya. Kuna mambo utajenga na mengine utapanda. Vyote viwili vinatakiwa ili uweze kuwa na mabadiliko. [somo linalofuata tutaangalia haya mambo kwa kina]

Katika sehemu ya kwanza ya somo hili, fanya yafuatayo:

1. Andika mambo yako ya muhimu unayotaka kuanzisha au kufanya katika mwaka huu 2016. Haijalishi kama ni mambo ya kudumu zaidi ya mwaka huu, andika tu.


2. Angalia mambo unayodhani ni vikwazo vya hiyo kazi yako au jambo unalotaka kufanya.


3. Anza kumwomba Mungu akufundishe yakupasayo kujua kwa habari ya mapenzi yake juu ya hiyo kazi unayotaka kufanya.


4. Weka mkakati wa kusoma Neno kila siku na mfululizo kwa mwaka mzima. 


5. Omba Mungu akuinulie watu wa kufanya hayo mambo unayotamani kufanya.


Zingatia hili, haya maombi sio ya siku moja, utaendelea kuomba kwa muda wa mwaka wote, hata utakapokuwa umeanza kufanya udhaniyo ni yamuhimu kufanya.
Frank P. Seth

Comments