JE! WEWE NI MTU WA MUNGU?

Na Frank P. Seth

"Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao. Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia" (Isaya 65:19-24).

Hii ni ahadi kwa watu ambao Mungu anawaita "watu wangu". Swali, Je! Mimi ni mtu wa Mungu? Kuna tofauti gani kati ya mtu wa Mungu na watu wengine?
Mara nyingi hili wazo la "watu wa Mungu" limesumbua sana kwa maana kwa urahisi unaweza kujiuliza, "inamaana kuna watu ambao sio wa Mungu?" Sasa nitajuaje kama mimi ni mtu wa Mungu au sio?
Je! Dini tu au dhehebu tu linaweza kuwa tofauti baina ya makundi haya? Je! Cheo chako kanisani kinaweza kukuweka kwenye kundi la watu wa Mungu? Bila shaka jibu lake ni HAPANA. Kama sio dini, dhehebu au CHEO, basi tofauti yake ni nini?
Kwa kutafakari zaidi, angalia mambo haya halisi:
1. Wakati Mungu anasikia kilio cha wana wa Israel kule Misri, na anamfuatilia Musa ili akawatoe utumwani, hakuna aliyemjua Mungu wala jina lake! Ila Mungu aliwaita "watu wangu". Kwa hiyo sio dini yao iliwasaidia kuwa watu wa Mungu.
"7BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao" (Kutoka 3:7)
2. Watoto wa Ibilisi na watoto wa Mungu
"39 Wakajibu (wenye dini za Kiyahudi), wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. 40Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. 41Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. 42Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. 43Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. 44Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo" (Yohana 8:39-44).
Hao ni wenye dini (Wayahudi), lakini kati yao bado kuna wana wa Ibilisi! Kwa sababu "wanatenda mambo ya baba yao" japo wapo kwenye dini zao!

3. Wakati Mungu anamwona Korinelio, kati ya maelfu ya watu, achilia mbali Wayahudi na dini zao NZURI, Korinelio alikuwa mmataifa! (Matendo ya Mitume 10 - soma mlango mzima).
Mitume hawaamini kwamba hata "wamataifa nao wanapokea kipawa cha Roho Mtakatifu" kama wao, na sio hivyo tu, "wamataifa wanafanya mambo MAKUU kuliko wao" ambayo Mungu anayaona na kuyahesabu!
Swali ni Je! Wewe ni mtu wa Mungu? Kumbuka ahadi za Mungu haziendi JUMLA JUMLA tu. Kila ahadi inakundi lengwa, Je! Kundi lako ni lipi na UNASTAHILI ahadi zipi?
Frank P. Seth

Comments