KANISA LA KIROHO LIKOJE?

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kanisa la kiroho likoje?
Kanisa ni kusanyiko(kundi)la watu walioitwa kutoka dhambini na kumwamini BWANA YESU. Kanisa ni mwili wa KRISTO Yaani watu watu waliookoka miaka yote iliyopita   na watakaoendelea kuokoka hadi siku ya unyakuo wa kanisa.
Kanisa la kiroho ni mtu au ni kundi  la watu au dhehebu la watu ambao  wanamwabudu MUNGU katika roho na kweli.

Yohana 4:24 '' MUNGU ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''

MUNGU ni ROHO maana yake unaweza ukasema MUNGU ni ROHO MTAKATIFU na kama unataka kumwabudu basi ni muhimu kumwabudu katika roho .
Kwenye andiko hapo juu Biblia inasema MUNGU ni Roho na sio roho maana yake Neno ''Roho'' ni nafsi kamili ni jina ndio maana limeanza na herufi kubwa.
MUNGU ni ROHO na nguvu zake hutokea rohoni na sio mwilini.
Baraka zake hutokea rohoni na sio mwilini.
Ushindi wake kwetu huanzia rohoni na sio mwilini.
Kama tunataka kumpendeza MUNGU ni lazima tuwe watu wa rohoni na sio mwilini.
Waabuduo halisi wanatakiwa wamwabudu MUNGU katika roho na kweli.

Mithali 20:27 Biblia inasema ''Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake. ''

MUNGU najua yote anayotenda mwanadamu hivyo hatuwezi kumficha kitu chochote hivyo kama tunataka kumwabudu basi ni lazima tumwabudu katika roho na kweli.
Kama kweli ndani yako haimo MUNGU atajua, kama unaigiza tu kumwabudu MUNGU bado yeye atajua.
Ni lazima tuwe kanisa la kiroho na linalomwabudu MUNGU BABA katika roho na kweli.
Tukimwabudu MUNGU katika roho na huko hatuna hiyo kweli yake bado tutakuwa hatujatimiza kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.

Yohana 17:17 ''Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.''

-Neno la MUNGU ndio kweli.
Kuanza kumpendeza MUNGU huanzia pale tunapolitii Neno lake.
Kwa Kulitii Neno la MUNGU ni lazima kwanza tumpokee BWANA YESU kama mkombozi wa maisha yetu.
Kuokoka ndio mwanzo wa kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.

Warumi 8:5-9 ''Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.  Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya MUNGU, kwa maana haitii sheria ya MUNGU, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza MUNGU. Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake.''

Kuna sauti nyingi duniani, kuna nguvu nyingi duniani.
Sio kila sauti ni ya MUNGU na sio kila nguvu ni ya MUNGU.

Tumepewa Neno la MUNGU ili kuthibitisha kile ambacho ni cha MUNGU na kile ambacho sicho cha MUNGU.

 1 Yohana 4:1-3 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. ''


-Tumepewa ROHO MTAKATIFU ili kutujulisha kile ambacho ni cha MUNGU na kutupa taarifa kuhusu kile kisichofaa.
=Kuokoka ni hatua ya kwanza ya kuanza kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.
=Kuishi maisha matakatifu ni hatua ya pili.
=Kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU ni hatua inayokuthibitisha kwamba hakika wewe ni mwanafunzi wa YESU KRISTO.

 Mkristo aliyeokoka anatambulikana kwa matendo yake na sio maneno yake
Kuokoka ni jambo la lazima kwa mtu anayetaka kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Kuokoka ni Kumpokea YESU KRISTO kama BWANA na Mwokozi wako, Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. ''

Katika uhalisia naweza kusema kwamba KUOKOKA ni kufumba macho ya ndani ili usiviangalie na kuvitendea kazi vile vinavyoweza kukurudisha kwa shetani.

1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA(MUNGU), bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.'

 Ukijua thamani ya wokovu wako utajithamini ili utimize yale yanayowapasa watakatifu wa KRISTO.
Moja ya mambo muhimu yawapazayo watakatifu ni kumwabudu MUNGU katika ROHO na kweli.

 Wagalatia 5:25 "Tukiishi Kwa ROHO, Na Tuenende Kwa ROHO".  

 Jambo jingine naomba niseme ukweli huu kwamba Kila Mwanadamu asiyemwamini YESU KRISTO kama Mwokozi wake amepotea.
Kumkataa YESU ni kuukataa uzima wa milele.

Najua unatamani kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Ngoja nikuulize swali hili.
Je umekimbilia kwenye hema(Kanisa) ili kuyafanya mapenzi ya MUNGU aliye hai?
Ni swali ambalo kila mtu anatakiwa kujiuliza na kujijibu.
Kama umejiunga na kanisa ili uyatimize mapenzi ya MUNGU basi kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli ni moja ya mambo ya muhimu kwako.

Nimesema hapo juu kwamba Mtu pia anaweza akawa kanisa.
Kanisa sio jengo bali ni watu.
Kanisa ni mwili wa KRISTO hivyo wewe kama kanisa unatakiwa uwe kanisa la kiroho na unatakiwa umwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Kanisa la kiroho ni watu wale ambalo ni masikini wa roho.

 ''Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao-Mathayo 5:3.''
 
-Masikini Wa roho ni watu ambao wanauhitaji Wa mambo ya rohoni.
Rohoni Kuna MUNGU na neno lake.
Tunapomhitaji MUNGU na uzima wake Wa milele basi tutampata rohoni. Hivyo ni vizuri sana kuwa masikini Wa roho au muhitaji Wa mambo ya rohoni maana ukiyaishi ya rohoni kwa kumtii KRISTO hakika ufalme Wa mbinguni ni wako.

Tunaenda kanisani kwa sababu sisi ni wahitaji wa vitu vya rohoni.
Tunahudhuria maombi na mikesha kanisani kwa sababu sisi ni wahitaji wa rohoni.
Kama wewe sio masikini au mhitaji wa rohoni hakika hutaweza kuacha biashara yako ili uende kanisani.
Kanisa la kiroho ni wale wanaomwabudu MUNGU katika roho na kweli, ni maskini wa roho maana wanahitaji mambo ya rohoni.

Kanisa la kiroho ni ushirika wa watakatifu waliookoka na wanaishi maisha mataktifu.
Ushirika ni neno linalotokana na kushirikiana.
Tulipompokea YESU tulizaliwa katika familia ya MUNGU hivyo ni lazima tuwe na ushirika na wakristo wenzetu waliompokea YESU.
Yohana 1:12-13 Biblia inasema " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. "

=Waliookoka wote ni familia ya MUNGU hivyo wanatakiwa kuwa na ushirika kama familia moja ya MUNGU.
=Tunaitwa watoto wa MUNGU kwa sababu tuna ushirika na MUNGU.
Ndugu, naomba ujue kwamba ukipoteza ushirika na MUNGU unakuwa nje na ufalme wake.

Tu viungo katika mwili mmoja.
Tu askari katika jeshi moja.
Tu wenye uraia katika taifa moja liitwalo wateule wa KRISTO.
Sisi ni ushirika.

Tukiwa kama ushirika basi huwa tunakutana na kumwabudu MUNGU katika roho na kweli tukiwa kundi lake takatifu.

1 Kor 12:27 ''Basi ninyi mmekuwa mwili wa KRISTO, na viungo kila kimoja peke yake.''

Tuna ushirika na MUNGU.
Tuna ushirika na BWANA YESU aliyetuokoa.
Tuna ushirika na ROHO MTAKATIFU anayetuongoza na kutufundisha.
Tuna ushirika sisi kwa sisi kama timu moja yenye malengo mamoja yaitwayo uzima wa milele.
Ushirika wetu unahusisha kukutana ibadani ili kujifunza neno La MUNGU pamoja.

Tunatakiwa tumwabudu MUNGU BABA katika roho na kweli.
Tunatakiwa pia Kuonyana ili asitokee wa kutoka nje ya mstari wetu uitwao wokovu wa KRISTO.
Nawapenda wateule wote haijalishi wanatoka kanisa gani.
Wote ni watoto wa MUNGU kama wanaliishi neno La MUNGU.


1 Timotheo 3:15 ''
Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya MUNGU, iliyo kanisa la MUNGU aliye hai, nguzo na msingi wa kweli.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments