Laana ya miungu

NA MCH. MAXMILIAN MACHUMU,UFUFUO NA UZIMA

1Samweli 17: 40 "Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti. Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli."
Goliati ni uzao wa wafilisti waliotokea duniani ambao na miili yao walikuwa wakubwa sana, ndio maana wale wapelelezi waliotumwa kuipeleleza nchi ya ahadi walipowaona walijiona wao kama panzi kwao. Watu wazima wa wamisri waliwaogopa sana lakini mtu mmoja mwenye macho ya tofauti hakuwaogopa bali aliamua kuwaongoza ili wakapigane nao na walifanikiwa kuwashinda. Tunajifunza kwamba ukiona Jitu kubwa kwenye maisha yako ya kawaida usiangalie jinsi uwezo wako ulivyo na ukubwa wake bali angalia Uwezo wa Bwana kwenye kukushindia vita dhidi yake.
Wana wa Israeli waliamua kumchagua mtu mmoja ili akapigane na Goliath. Sauli alipoambiwa aende kupigana naye hakwenda wala wanajeshi wake, aliamua kumtoa binti kuwa mke kwa mtu yoyote atakayejitokeza kwenda kupigana naye lakini hakuna mtu aliyejitokeza. Nchi nzima ya Israeli ilikuwa inamwamini Sauli kama kiongozi wao mkuu ambaye ndiye mwenye maamuzi makuu.
Ilipofika mahali vita hii imeshindikana kwa kuwa hakupatikana mtu wa kuwapigania wana wa Israeli, Daudi alitumwa kwenda kuwapelekea ndugu zake chakula ndipo akamkutiliza Goliath akiwatukana wana wa Israeli.
Daudi alipomsikia Goliath aliacha kila kitu akauliza kwamba atafanyiwa nini mtu atakayempiga. Sauli alipomwona Daudi alimdharahu lakini Daudi alimshawishi asimwangaliye mtu wa nje bali amwangalie mtu wa ndani. Akamwambia alikuwa akichunga kondoo wa Baba yake na siku moja akaja Simba amle kondoo wa Baba yake naye akapigana naye hadi akamshinda na kumwua. Daudi akamwambia Sauli kwamba kama anao uwezo wa kupigana na Simba na Dubu na huyo mfilisti asiyetahiriwa naye lazima ampige.
Ikafika asubuhi Goliath alijiandaa vizuri na silaha zake akaingia bondeni na Daudi naye.Goliath alijaribu kumtishia daudi kwa silaha zake lakini Daudi hakutishika, akaamua kumlaani Daudi kwa miungu yake.
Goliath hakuamini silaha zake za kivita na akaamua kutokubahatisha kupigana, akaamua hawezi kushinda vita yake bila kumlaani mpinzani wake. Goliath alimwaga laana yake kwa Daudi. Aliacha mambo ya mwilini akahamia rohoni akijua ushindi wa mwilini sio ushindi wa kubahatisha
Yapo makundi matatu yaliyopewa mamlaka na Mungu ya kulaani mtu akalaanika
1. Wazazi wamepewa mamlaka ya kulaani na mtoto akalaanika haijalishi Baba au Mama ni mchawi au mlevi akikulaani unalaanika. mzazi anaweza akatamka laana na mizimu ikayashikilia yaliyotamkwa mpaka yatokee.
2. Watumishi wa Mungu nao wanaouwezo wa kulaani na mtu akalaaniwa na wanauwezo wa kubariki na mtu akabarikiwa. Elisha aliwalaani watotot waliokuwa wakimdhihaki kwa sababu ya upara wa kichwa chake na laana yake ikavaa mwili akatokea simba akawala wale watu aliowalaani.
3. kundi la tatu ni mganga wa kienyeji. Mtu anaweza akawa hakupendi au umegombana naye na akaamua kukuendea kwa mganga ukalaaniwa. waganga hawa wanapotoa maneno kunakuwa na mapepo yanatoka na kuyasimamia yale maneno mpaka yatokee.

Laana sio kitu lakini kitu ni wasimamizi wa laana hiyo. Mtu anaweza akaenda kanisani huku ametumiwa mapepo na yakakemewa na kutoka. Kuna mizimu ambayo imejiungamanisha na damu ya ukoo na majina ya ukoo. mizimu hii unakuwa inafahamu damu yako ni damu yao na jina lako ni jina lao (jina la kitu ndio kitu chenyewe). Mtoto anaweza akawa analilia jina la Babu na mkimpatia tu ananyamaza fahamu mtoto huyo anamilikiwa na mzimu.
Laana zinazosimamiwa na mizimu zinakuwa ngumu kuvunjika sababu mizimu inakuwa ipo ndani ya mfumo wa maisha ya mtu. Hii ndio ngazi ambayo inawasumbua watu na ndio wanaoweza kusimamia laana isimtoke mtu.
Mwanzo 31: 24 "Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi. Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu. Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari."
Labani alikatazwa na Mungu asimlaani Yakobo wala asimbariki baada ya kugundua ameondoka na miungu yake. Mungu alijua kwamba Labani akitoa neno kwa Yakobo lazima angepata madhara.
Waliokulaani kwa mapepo na majini na mizimu tayari ulishafunguliwa lakini waliokulaani kwa miungu laana hiyo ni ngumu lakini utashinda kwa jina la Yesu. Daudi alipolaaniwa na Goliath yeye aliamua kumwambia atamjia kwa jina la Bwana wa Majeshi. Likitajwa jina la Yesu kristo mwana wa Mungu aliyehai hata miungu haitafanikiwa. Tunawaendea miungu yote kwa jina la Bwana Mungu wa miungu.
DALILI TATU ZA MU ALIYELAANIWA NA MIUNGU
1. Anakuwa na tatizo Sugu. Miungu humpatia mtu magonjwa sugu ambayo hata mtu akiombewa anakuwa haponi sababu inakuwa ina nguvu sana. Watu wengine wanaweza wakawa wanajua kwamba mtu wanayetaka kumlaani anakwenda kuomba sehemu fulani hivyo husafiri mpaka sehemu ambayo watapata miungu ya kufungia.

2. Kukosa jasiri wa kuchukua hatua. Goliath alikuwa anatukana matusi makubwa japo hatujaambiwa matusi gani alikuwa anatukana lakini ilikuwa ni laana ambayo aliwatukana wana wa Israeli kiasi kwamba wakashindwa kupigana naye hata mmoja kwa kujaribu.
Mungu ameweka ushndi ndani yako na ushindi huo unatokana na kuchukua hatua, Mungu hakutupa roho ya uoga bali ametupa sisi Roho ya Ujasiri na moyo wa kiasi. Unapokuwa na uoga wa kufahamu kwamba kuna laana imeachiwa juu yako. Uoga sio wa kibinadamu ni laana na unakuwa unamaanisha kila jambo litakalokufanya ufanikiwe usilifanye na kila jambo litakalokupeleka kwenye maangamizi ulifanye.
Daudi alipakwa mafuta ili aje awe mfalme lakini nchi haikumtambua na kulikuwa na laana iliyosababisha asitambulike lakini aliweza kuishinda laana ile kwa kumpiga Goriath. Ukichukua ujasiri Mungu anakutia nguvu njiani. Kilichomshinda Goliath ni ule ujasiri aliokuwa nao Daudi. Ujasiri ndio unaoleta miujiza kwenye maisha ya mtu.
Mungu hafanyi kazi kwa watu waoga bali anajidhihirisha kwa mtu yeyote mwenye ujasiri, ukiyahifadhi maisha yako ili Mungu atukanwe na wewe ukae kimya fahamu kwamba maisha yako yatakuwa sio salama kabisa, lakini ukijihatarisha maisha yako ili Mungu asitukanwe maisha yako yatakuwa salama. miungu inakufanya uogope lile eneo ambalo unatakiwa ubarikiwe kwalo.
3. Kushindwa na kufa. Balaki alikamwita balaamu akamwambia kwamba tumesikia habari za hawa watu hivyo naomba uje unilaanie watu hawa. Balaamu aliitwa alaani ili jeshi la Israeli lishindwe kabla ya vita, Goliath alimlaani Daudi ili ashindwe kabla ya vita. Mtu yeyote aanyeshindwa mara kwa mara huyo anaelekea kufariki. Maisha yamejaa mashindano kila siku usiku na mchana na jinsi vile ulivyo ndivyo matokeo ya mashindano uliyowahi kushindana kule. Kushindwa kwa mtu hakutokei kwa bahati mbaya kila mtu anatamani kushinda lakini kama una laana ya miungu huwezi kupata tuzo ya ushindi. Unatakiwa ujue kinachoitwa laana ndio kushindwa kwenyewe huko. Ukiona mtu ameshindwa muulize kilichomfanya mpaka ashindwe utafahamu kwamba ameshindwa kwenye maamuzi sehemu nyingi kwenye maisha yake mpaka kumpelekea kufikia hapo alipo.
simama upigane kwa jina la Bwana wa Majeshi ili kuvunja laana za miungu zilizokufikisha hapo ulipo, fanya vita vya kiroho bila kichoka kuharibu laana za wachawi na washirikina waliokutumia laana kwenye maisha yako kwa jina la Yesu Kristo Amen.

Comments