MAARIFA KATIKA KUTENDA MEMA

Na Frank P. Seth

"Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa" (Yeremia 4:22).

Hebu tazama maana ya "kuwa na akili katika kutenda mabaya", kisha tafakari.
Tena angalia "maarifa katika kutenda mema", kisha tafakari.
Angalia jambo hili, ni GHARAMA, BIDII na AKILI kiasi gani mtu anaweka katika kutenda uovu? Na, tazama tena, ni GHARAMA, BIDII na AKILI kiasi gani mtu anaweka katika kutenda mema?
Niliposoma msitari huu katika Yeremia nikaona, kumbe, Mungu analinganisha! Lakini kumbuka jambo hili, kutenda mema kuna hitaji NGUVU nyingi kuliko kutenda mabaya kwa sababu ya NIA. Penye nia siku zote patakuwa na njia, ndio maana vita dhidi ya UOVU ni ngumu kwa sababu atendaye mabaya ameamua katika nia yake; hadi NIA ibadilike ndipo ataacha uovu wake. Je! Umenuia nini? Nguvu ya nia ni kubwa, ukiweza kuidhibiti, utakuwa mtu tofauti.

Paulo alipotazama jambo hili la kutenda wema, akasema, “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” (Wagalatia. 6:9-10).

Mambo ya kuzingatia, katika Wagalatia 6:9-10: 

1. Kuna KUCHOKA kutenda wema


2. Kuna KUVUNA faida kwa sababu ya kutenda wema


3. Kuna WAKATI ambao utatenda wema ila MATUNDA hayaji utakavyo, ila huja kwa wakati wake.


4. Kuna NAFASI ya kutenda wema


5. Ukikata tamaa (KUZIMIA ROHO) ni kikwazo cha kuvuna matunda ya wema wako uliotenda. 


6. Wema unatendwa kwa watu WOTE ila angalia sana watu wa nyumbani kwako (usipojali watu wa nyumbani kwako unalinganishwa na mpagani) na waaminio. Ukiweza kutenda SAWA kwa wote umefanya jambo jema zaidi.


Sasa katika mambo haya 6, nitasema ziadi hili la 3 & 4. Fikiri unafanya MEMA halafu unalipwa MABAYA. Kuna hatari ya kuzimia roho. Fikiri unataka kutenda wema ila huna NAFASI (muda, mwenye shida haji kuomba msaada, mwenye shida ni wa kutafuta, mwenye shida yuko mbali, UTARATIBU hauruhusu, unayetaka kumtendea wema ni MKOROFI, umetenda wema lakini unatukanwa, nk). Nilipotazama haya mambo mawili (3&4) ndipo nikaona kwanini imetupasa kuwa na MAARIFA ili tuweze kutenda wema.

Basi nilivyozidi kutazama, nikaona jinsi ambavyo TUMEJIFARIJI kwa kutokutenda wema, eti, kwa sababu hatujaulizwa, hatujaombwa, hatukujua, mhusika yuko mbali, mhusika ni mkorofi, mhusika hana shukrani, nk. Je! Umeona jinsi ambavyo inatupasa kuwa na BIDII na MAARIFA ili tuweze kutenda wema? Basi Mungu alipotazama akaona kumbe jitihada zetu kwenye kutenda uovu zimezidi zile za kutenda mema; hata kama tuna sababu za msingi za kutokutenda wema, bado imetupasa kutenda wema tu.
Frank P. Seth

Comments