MAMBO (10) MUHIMU KUYAJUA KIONGOZI WA KANISA

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU asifiwe.
Namshukuru MUNGU kwa kunilinda na namshukuru MUNGU kwa ajili ya marafiki zangu ambao wanasoma jumbe zangu ambazo MUNGU ananipa kwa ajili yangu na kwa ajili ya rafiki zangu na ndugu zangu wote.
Natarajia kuwa na masomo mengi sana maana kila iitwapo leo napewa ujumbe wa kufundisha.
Ubarikiwe wewe unaekula Neno la MUNGU ili upate afya na kiroho.
 Mathayo 5:6 '' Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. ''

Ubarikiwe wewe ambaye ni udongo mzuri uliopandwa mbegu njema ambayo ni Neno la MUNGU aliye hai.

Luka 8:8 na 15 ''Nyingine(Mbegu) zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie. .... Na zile penye udongo mzuri, ndio wale(Watu) ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia. ''
 
Naomba uyajuae mambo haya wewe uliye kiongozi kanisani kwako na wewe unayetamani kuwa kiongozi kanisani ili yakusaidie kuongeza ufahamu na kuijua nafasi yako.

1.  Chanzo cha kumtiii MUNGU ni kulisikia Neno lake.

Kulisikia Neno la MUNGU ndio chanzo pia cha wewe kuitwa na MUNGU.
Kuipokea Imani ya KRISTO ni kutii kuitwa kwako na MUNGU.

 Warumi 10:17  '' Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''

-Wewe umeitwa na MUNGU kwanza uokoke kisha utumike.
MUNGU amekuita hapo ulipo na utakuwa hapo mpaka MUNGU atakapokupangia majukumu mengine,
Jitahidi sana kushirikiana na viongozi wenzako mahali hapo mlipo  ili muifanye kazi ya MUNGU vizuri. Kumbuka umoja ni nguvu hivyo usikubali kujitenga na viongozi wenzako kanisani.

 Mithali 18:1 ''Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema. ''


 2.   Kuna gharama katika kuitii sauti ya MUNGU lakini kuna faida kuu kama utaitii sauti ya MUNGU.

Faida ya kuitii sauti ya MUNGU huwa ni kubwa kuliko gharama za kuitii.
MUNGU anaweza kukuweka chini ya mchungaji wako ambaye unamzidi Elimu na uelewa. Kumtii Mchungaji inaweza kuwa gharama kubwa kwako lakini MUNGU anaweza kumtumia mchungaji wako huyo huyo ili kukufanya ukamilike katika utumishi mkubwa zaidi wa baadae.
Mtumishi mmoja wa marekani aliambiwa ampe mtumishi mwingine mali zake zote na aende akawe chini yake, ilimshumbua mtumishi yule lakini alipotii MUNGU alimtengeneza kupitia mtumishi yule wa pili na sasa huyo aliyetii sauti ya MUNGU ni mmoja wa watumishi wakubwa sana duniani, yaani huduma yake imeinuliwa sana na MUNGU. Lakini chanzo cha kukua kwa huduma yake ni utii wake.
 1 Samweli 15:22 ''Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. ''

-Kutii ni bora kuliko dhabihu.

 3. Kuna watumishi wa MUNGU na kuna watumishi wa watumishi wa MUNGU. 

Inawezekana kabisa wewe kwa sasa ni mtumishi wa MUNGU lakini kiutumishi wewe ni mtumishi wa mtumishi wa MUNGU bado. ukijua siri hii itakusaidia na utakataa roho ya kiburi na kudharau wale ambao MUNGU amewaweka juu yako.

Yoshua alikuwa anaitwa mtumishi wa Musa hadi Musa alipofariki ndipo tunamuona Yoshua akiitwa mtumishi wa MUNGU.
-Yoshua alikuwa mtumishi wa Musa kabla ya kuwa mtumishi wa MUNGU.
Kama hujaitwa rasmi na MUNGU katika utumishi, wewe utabaki mtumishi wa mwenye wito kanisani kwenu hadi utakapoitwa rasmi wewe kama wewe.

Usijiite bali subiri uitwe na MUNGU ndipo utatumika vizuri.
Mfano ni huu; Sio kila mtanzania ni mtumishi wa serikali, lakini kila mtanzania ni muhimu sana katika Tanzania.
Elisha kabla ya kuwa mtumishi wa MUNGU alikuwa mtumishi wa Eliya. Ajabu ni kwamba kuna watumishi wenye watumishi lakini hawawasaidii watumishi wao ili baadae wawe watumishi wa MUNGU wazuri.

Yatafakari haya niyasemayo ili utengeneze vizuri utumishi wako.

 ''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.-2 Timotheo 2:15''



 4.  BWANA MUNGU anapomchagua mtumishi wake, hamchagui kwa sababu ya uelevu wake bali anamchagua kwa sababu ni mali yake.

1 Samweli 16:7 ''Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. ''

Kama MUNGU amekuita katika utumishi basi ni muhimu sana kujua kwamba MUNGU amekuita sio cha sababu ya elimu yako au ujanja wako bali kwa sababu tu wewe ni mali ya MUNGU kama walivyo wengine.

 Mtumishi aliyeitwa ni lazima sana aitii sauti ya aliyemuita.
Wewe Mteule wa YESU umeitwa ili uwe mtumishi wa kazi ya MUNGU duniani hivyo itii sauti ya MUNGU aliyekuita.
Ukiwa chini ya mchungaji bado timiza utumishi wako bila manung'uniko na dharau hata kama unajiona una upako kuliko mchungaji.

2 Kor 9:13-15 '' kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya KRISTO, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote. Nao wenyewe, wakiomba dua kwa ajili yenu, wawaonea shauku kwa sababu ya neema ya MUNGU iliyozidi sana ndani yenu. MUNGUashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo. '' 

 5.  Mtu akikua huonekana kwa umbo lake, na imani ikikua huonekana kwa matunda yake.

Ni Muhimu kula Neno ili ukue.
Kama kiongozi wa kanisani hakikisha unakuwa kiroho sio kudumaa kiroho.
Kila mtu anatakiwa ajifunze Neno la MUNGU ndipo atakuwa mtumishi mzuri.
 Ili ukue kiroho ni lazima sana ujifunze sana Neno la MUNGU na kulitendea kazi.


1 Petro 2:2-3 '' Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili. ''


6.  Unaweza ukawa kiongozi lakini usiwe na uwezo wa kuwasaidia unaowaongoza kusonga mbele.

Kiongozi mzuri ni yule amefaulu kuwa muumini mzuri.
 Huwezi kuwa kiongozi kama bado hujawa muumini.
Kiongozi mzuri kanisani ni yule ambaye ni muumini mzuri.
Haya ni ya muhimu sana kuyajua na kuyaishi na kuyatendea kazi.
Wachungaji wengi leo ni wale waliokuwa wazee wa kanisa zamani, ni wale waliokuwa mashemasi zamani, ni wale waliokuwa viongozi wa vijana, kwaya, wamama na watoto zamani.
MUNGU aliwaona wamefaulu huko ndio maana akawapa uchungaji kwa sasa.
Kama kiongozi hakikisha unawasaidia unaowaongoza kusonga mbele katika utumishi wa injili.
Kama kiongozi humtii BWANA YESU hakika utakuwa chanzo cha kupeleka watu jehanamu na sio mbinguni maana unaowaongoza watakuiga kutokumtii BWANA YESU na kujiletea uangamivu mkuu.
 Jichunge sana na jifunze sana maana wewe unahitaji Neno la MUNGU siku zote.

Waebrania 5:12 ''Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya MUNGU; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. '' 

7. Madhabahu ni daraja kutoka ulimwengu wa roho kwenda ulimwengu wa Mwili.

Ufunuo 16:7 '' Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, BWANA MUNGU Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.'' 
 

MUNGU hupitishia Neno lake kwenye madhabahu.
Madhabahu inatakiwa kuheshimiwa, kulindwa na kuombewa.
Kama kiongozi yajue hayo ili MUNGU akikupa baade madhabahu ili uhudumu basi hutasema uongo madhabahuni maana unaiheshimu madhabahu ya BWANA.




8.  Jiamini kama YESU amekuamini hata kukupa uzima wake baada ya wewe kumpokea.

Yohana 1"12-13 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;
waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''


Jikubali kama YESU amekukubali hata kukupa neema yake ya ukombozi.
Kiongozi aliyeokoka na hatendi dhambi ni lazima ajiamini.
Kama kiongozi hajiamini hakika na anaowaongoza watakuwa hawajiamini.
Kiongozi ni mtatuzi wa shida za watu hivyo tumia muda mwingi katika maombi na kujifunza kwa watumishi walio juu yako ili ikusaidie katika uongozi wako kanisani sasa na baade utakapokuwa Mchungaji au Askofu.

9. Kuna nguvu katika umoja.

Zaburi 133:1 ''Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. ''
 
Nyumba haijengwi kwa tofali moja bali tofali nyingi.
Mwili hauna kiungo kimoja bali vingi.
Kanisa pia halijengwi na mtu mmoja bali watu wengi.
Kanisa likiwa na umoja ni faida kubwa.

Kama kiongozi linda umoja kanisani sio kuiharibu umoja huo.
Inawezekana kabisa ulipo hapo ni sehemu MUNGU amekuweka ili ujifunze hivyo hakikisha unaongezeka katika kujifunza na kuwa na umoja na viongozi wenzako.


10.  Uwe na Hekima

Kuna hekima za aina 2.

=Kuna Hekima ya kibinadamu.
=Na Kuna hekima ya Ki MUNGU.

  Mithali 2:6 ''Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;''

Jifunze sana kuhusu hekima, na pambanua hekima ili ikusaidie baade katika utumishi wako.
Jihoji pia je una hekima ya MUNGU au una hekika tu ya kibinadamu inayokufanya kila siku uzozane na Mchungaji wako?

Wakolosai 4:5 '' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.''

Hekima ya Ki MUNGU ndio muhimu kwa wanadamu.
Mfano wa hekima ya Ki MUNGU ni pale ambapo Mtume Paulo aliposikia kutoka kwa KRISTO Kisha Paulo akamsikilizisha Timotheo na Timotheo naye akawasikilizisha wengine na wengine hao wakawasikilizisha wengine hata injili ikaenea. Hiyo ndio hekima ya Ki MUNGU.
Je unaipenda hekima ya Ki MUNGU?
Basi ukisikia Neno hai la MUNGU wapelekee na wengine ili wengine hao wawapelekee wengine.


 2 Timotheo 2:2 ''Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.  ''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments