NANI MWIZI?

Na Frank P. Seth

"Maana mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele" (Isaya 61:8).

Katika mazungumzo mafupi na ndugu mmoja baada ya ibada, liliibuka swali moja, "nani anastahili kuitwa mwizi/fisadi/mbadhirifu?"
Kwa maelezo ya huyu ndugu ambayo yalinipa changamoto sana, kuna kosa zaidi pale watu wanaponyooshea wenzao vidole kwamba ni wezi ilihali wao pia ni wezi! Sasa basi nani ni mwizi (mwivi)?
Bila shaka kila ajuaye maana ya msamiati huu atasema mwizi ni mtu achukuaye kitu cha mwingine bila ruhusa iwe kwa siri au wazi-wazi.

Sasa huyu ndugu akaendelea kunipa mifano, Je! Ni mara ngapi tunaiba muda wa waajiri wetu kwa sababu ya utoro au utegaji? Je! mbona ni rahisi kuchukua rimu ya karatasi za ofisi na kupeleka nyumbani kwako bila shida? Mbona kujichukulia vifaa au vitu vidogovidogo ambavyo vilinunuliwa kwa matumizi ya ofisi na wewe unapeleka nyumbani kwako? Mbona wachukua vitu vya wengine bila hata kuwaambia na kisha kukaa navyo bila kujali huku wenyewe wanasumbuka? Au kwavile ni kalamu tu?
Nilipotazama sana, nikajiuliza, hivi kumbe BWANA aliposema habari ya "kuona KIBANZI kwenye jicho la mwenzako wakati kuna BORITI kwenye jicho lako" ni rahisi tu? Ni rahisi sana kumwita mtu fisadi/mlarushwa/mwizi/mbadhirifu, nk. Jikague kwanza ndugu, weka mambo yako vizuri ndipo utaweza kufumbua kinywa kwa mwingine, japo hukumu sio kazi yako.

Sasa angalia, kuna tofauti ya KIBANZI na BORITI. Hivi kuchukua rimu ya karatasi ofisini kwa mwana wa Mungu si BORITI na kuiba mabilioni kwa wamataifa ni KIBANZI tu? Zingatia hili, mara nyingine ukubwa wa KOSA unaweza kupimwa na AFANYAYE kosa kuliko hata kosa lenyewe. Ndio maana mchungaji akizini watu hushangaa kuliko kondoo wake akizini. Au mtoto akitukana hadharani ni vyepesi zaidi kuliko baba yake akifanya hivyo. Je! Umeona maboriti tuliyonayo kwa sababu ya jina yetu japo kwa wengine ni vibanzi tu?

"Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako" (Luka 6:41,42).
Frank P. Seth

Comments