Oliver Zakaria. |
Mimi ni msichana wa miaka ishirini na nane, niliokoka na miaka ishirini na tatu, kabla ya kuokoka nilikuwa dhehebu moja sitapenda kulitaja, ndani ya dhehebu langu hilo nilikuwa muumini mzuri tu niliyekuwa nimeshika mapokeo yote yaliyokuwa ya dini yangu kwa kipindi kile.
Lakini cha kushangaza nilikuwa nikivutiwa sana na mahubiri na mikutano ya watu waliookoka na nilikuwa nahudhuria ,ila nilikuwa sipendi kuokoka.
Siku moja nilikuwa nimelala nikamwona muhubiri mmoja kwenye ndoto ambaye ni muhubiri mkubwa sana kwa hapa Tanzania ila kwa sasa amesha tangulia mbele ya haki.
Muhubiri huyu nilikuwa nikipenda sana mahubiri yake. Sasa baada ya kumwona akihubiri, nlianza kumdhihaki huku nikisema maneno haya "HAWA WALOKOLE WAONGO SANA,HAKUNA WOKOVU" Ghafla wakati naongea maneno hayo,nikaanguka chini nikaona mgawanyiko wa giza upande wake na nuru upande wake.
Kisha nikasikia sauti ikisema "TAZAMA WA MUNGU WALIVYO WACHACHE NA WATU WA SHETANI WALIVYO WENGI" Nakweli nilipo tazama katika giza kulikuwa na watu walikuwa wengi mno, ila katika nuru kulikuwa na watu wachache kweli,Ghafla nikashtuka kutoka usingizini,
Niliposhtuka toka usingizini nilitafakari sana juu ya ile ndoto niliyoiona ila sikupata jibu.
Baada ya muda kupita niliendelea kuhudhuria mikutano mbalimbali,ila siku moja nilikaa na kutafakari maisha yangu nikaona laiti ningekuwa karibu na baba yangu mzazi huenda ningekuwa na maisha mazuri.
Baba yangu ambaye alipotea katika familia yetu nikiwa mdogo na hakuna mtu aliyefahamu mahali alikuepo. Siku moja nilipata wazo kichwani nikiwa na umri wa miaka ishirini na tatu kwamba nimtafute baba yangu mzazi kupitia media, kweli nilianza taratibu za kutuma ombi langu katika radio fulani hapa nchini. Na wakati huo nilikuwa bado sijaokoka ila nikamwambia Mungu "kama kweli Mungu upo, na wokovu upo naomba unifanikishe nimpate baba yangu mzazi". Kweli Mungu akawa Mwaminifu kwangu nikafanikiwa kumpata baba yangu , Na baada ya kumpata tu Mungu akanikumbusha ahadi yangu niliiyoiweka kwake.
Nami nikatimiza ahadi yangu kwa kuokoka.
Safari ya wokovu ikaanza, niliendelea kumwona Mungu akitenda maajabu ndani yangu. Nikaendelea kuwa na kiu ya kumjua Mungu zaidi na Mungu alipoona kiu yangu akaniinua viwango vya juu zaidi. Siku moja niliota ndoto ya ajabu iliyonishtua sana . Nilisikia watu wakiimba chumbani kwangu usiku ila sikujua ni akina nani, na sauti zile sikujua kama ni wanaume au wanawake ila zilikuwa ni nzuri sana na walikuwa wakiimba wimbo niliokua nikiufahamu unaoitwa "KIJITO CHA UTAKASO"
Wakati wakiendelea na wimbo ule nilishtuka nikaamka nizisikilize sauti zile zilikuwa ni akina nani wanaimba usiku ule, niliposhtuka sikuona mtu nikajaribu kuangalia labda niliacha radio on, lakini ilikuwa imezimwa nikajaribu kujishika mwili wangu labda nikafikiri sikuwa katika hali ya kawaida nikajikuta ni mimi, nikajaribu kuamka pale nilipo nakutembeatembea chumbani sikuona mtu wala chochote. Basi nikatazama saa ilikuwa saa 8 za usiku, .ikabidi nianze kuomba,niliomba kama saa moja hivi kabla sijamaliza maombi ulikuja tena kama usingizi mzito kisha nikaanza kuzisikia zile sauti zimerudi tena ila wakati huu walibadilisha wimbo wakawa wanaimba wimbo mwingine unaitwa "TWAKWABUDU MAANA NDIWE BWANA.. X3 TUKWITAPO BWANA UNAASHUKA"
Nikataka tena nijiamshe kama nilivyofanya mwanzo ili niwaone waliokuwa wanaimba nikashindwa. Ghafla niliona roho yangu inachomoka taratibu kutoka katika mwili ikavaa mabawa mawili ikaruka mpaka juu ya paa kisha nikasikia sauti ikisema tazama mwili wako pale ulipo kweli niliposhusha macho pale nilipolala nikauona mwili wangu umelala pale kitandani. Nikajua kwa vyovyote Mungu anataka kuchukua roho yangu nikamwambia Mungu naomba kurudi nikaifanye kazi yako, naweka nadhiri mbele zako nitakutumikia maisha yangu yote. Ghafla ile roho yangu ikaruka ikaurudia ule mwili na sauti ile iliyosema mwanzo ikasema tena." NIMEKURUDISHA KWA KUSUDI MOJA TU UKANITUMIKIE KWA KUHUBIRI INJILI YA YESU KRISTO"
Nikashtuka toka kwenye yale maono huku nikistaajabu sana. Niliendelea kumtumikia Mungu kwa nguvu nyingi na vile nilivyotumika kwa wingi ndivyo Mungu alikuwa akinipandisha viwango vya kiroho. Nilikuwa nikipita masokoni, madukani, mashuleni na njiani nikihubiri injili ya Yesu, watu walikuwa wakinishangaa sana kwa mara ya kwanza kumwona mwanamke tena binti akihubiri injili. Wengine walikuwa wakinihurumia sana wanasema masikini huyu dada sijui kakosa nini mpaka anakuja kushuhudia habari za Mungu tena kwa mji kama Dar es salama uliojaa ufuska na uasi wa kila namna ila kwangu nilifunikwa na nguvu za Mungu nisiukaribie ule uasi zaidi ya kumtangaza Mungu. Nilikuwa nikihudhuria shule tatu za msingi kwa siku nikihubiri watoto habari za Yesu Kristo na kuwafanyia maombi na ndipo niliona jinsi mapepo yakioneo watoto mashuleni nikianza maombi tu watoto hata kumi walikuwa wakidondoka na kukimbia hovyo hovyo huku nikiwa peke yangu sina msaidizi kwa hiyo ikiwa kama fujo shuleni walimu wakasema tunaomba huyu mwalimu wa dini ya kilokole azuiliwe kuja hapa shuleni hivyo wakanizuia.
Nikaingia kwenye maombi ya kumwita tena Mungu kwaajili yao walionizuia kwakuwa Mungu ndiye aliyenituma sikuwa nalipwa mshahara bali kwa Bwana hatimaye wakaniruhusu nikaendelea na huduma bila kuzuiliwa nikamwona Mungu akiponya na kuwaweka huru wanafunzi wote walioonewa na ibilisi na kupanda roho ya injili ya Yesu Kristo ndani mwao.
Niliendelea kumtafuta Mungu sana na kutaka kuona uweza wake maishani mwangu. Lakini ilifikia mahali nikawa nafanya huduma kwa upinzani mkubwa sana nikawa sipendezwi na ile hali ikabidi nikaadhimia kufanya maombi ya siku arobaini lakini ya masaa kumi na mbili yaani kula jioni tu. Wakati nikiendelea na maombi siku ya ishirini na moja nilivamiwa na kundi la wachawi maelfu kwa maelfu nikawa kwenye maono nikaonyeshwa vijana wanne wanene weusi sana na kwa namna walivyokuwa wamejazia kwa lugha ya kisasa unaweza kuwaita mabaunsa. Wakanishika mguu wa kulia kwenye goti huku wanaubana kwa nguvu sana, nikawa nasikia maumivu makali sana huku nalia na kukemea toka kwa jina la Yesu. Jinsi nilivyokuwa naendelea kukemea ndivyo walivyokuwa wakinibana zaidi na zaidi. Baadae nilijikuta nikiita Mungu naomba unirehemu na watu hawa. Ghafla nikasikia kama mtu amechukua msasa akaanza kusafisha na kuusugua mwili mzima, kisha alipomaliza nilisikia kama mtu ananidondoshea matone makubwa ya maji kichwani, wakati anaangusha yale mateno ya likuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba wakati wakudondoka kwake mpaka mwili ulitikiswa mpaka nyumba na vyombo vilivyokuwa ndani ya nyumba vilikuwa vinatikisika. Kifupi kulikuwa kama na tetemeko kubwa kila baada ya kudondoka kwa tone moja, na matone yale yalikuwa yakinidondokea usawa wa kichwa utosini. Na kila tone lilokuwa linadondoka nguvu zilitofautiana, lilianza la kwanza, la pili, na tatu nguvu za yale matone ziliongezeka toka moja hadi jingine. Baada ya kumalizika tone la tatu tu ile nguvu ilininyanyua kutoka chini mpaka juu kabisa na nikaona nagusana na wingu, huku chini niliona watu wengi kama mchanga na wote walishika vitambaa vyeupe wakipepea upande huu na upande huu kwa pamoja, Kisha mimi nilikuwa nikiwaimbisha wimbo mmoja aliimba mtumishi wa Mungu John Lisu unasema" JEHOVA YU HAI" kisha wale waliokuwako chini waliungana na mimi niliyekuwa juu tukauimba ule wimbo pamoja na kwa sauti moja huku wakishangilia. Wakati ule ikatokea sauti kule kule juu mawinguni ikasema nami ila sijui kama wale wa chini nao waliisikia ikasema hivi " NIMEKUPA KIBALI KISICHO CHA KAWAIDA HAKUNA ATAKAYEWEZA KUSIMAMA MBELE YAKO WAKA KUKUPINGA" Ghafla nikashtuka kutoka kwenye maono yale.
Kweli niliendea kumwona Mungu kwa namna ya tofauti sana, nikaendelea kumtumikia Mungu. Ila kwa kawaida ukimtumikia Mungu kwa karibu ni sawa na kutangaza vita na shetani kwenye ulimwengu wa roho, anakuwa na hasira kama dubu jike aliyejeruhiwa. Siku moja nikiwa jikoni napika kama saa tano asubuhi, nikasikia sauti inasema nami maneno haya "HIVI UKIJARIBIWA KAMA AYUBU UTAWEZA" nikaijibu ile sauti maana ilikuwa kama iliniuliza swali. Ghafla baada ya siku kadhaa nikaanza kuugua kila nikienda hospitali wanasema mara malaria, mara taifodi nikahangaika kwa muda mrefu bila kupona wala kupata nafuu..nilikuwa nasoma ilibidi niache maana nilikuwa siwezi kuhudhuria shuleni. Niliendelea kuugua kwa muda mrefu sana mpaka nikawa mtu wa kitandani tu siwezi kwenda popote, nikakakonda nilikuwa na kilo 65 nikabaki na kilo 49 kwa hali ya kawaida ungeweza kusema ni kama muathirika wa ukimwi. Lakini sikuwa na uathirika, ndugu walikata tamaa yangu ya kuishi na wakajua muda wowote naweza kufa. Hakika nikikumbuka mateso yale niliyoyapata na jinsi hali yangu ilivyokuwa mbaya nafika mbaaali mbali sana,Nilikuwa naona niko mbali sana na wanadamu kama vile mtu anayeishi katika sayari nyingine na mauti ilikuwa ikinizungukazunguka ooh ashukuriwe, Mungu wa israel muumba wa ardhi mbingu na nchi. Madaktari Walifika mwisho wa akili zao maana joto la mwili likuwa 40 nyuzi joto na lilikuwa halipungui, walinichoma sindano za kila aina mpaka nikawa siwezi kukaa wala kusimama nikulala tu mchana na usiku, nikawa nikiendelea kumsihi Mungu aniponye, na chakushangaza moyoni nilikuwa nikisikia amani,watu walikuwa wakilia kwa uchungu na kunihurumia ila mimi nakumbuka nilikuwa nikimwaambia neno hili mara kwa mara"ijapo haribika mwili huu nitapata mwingine kwa Baba, kuishi ni . Kristo nakufa ni faida..nikiishi ni kwaajili yake na nikifa ntakwenda kukaa nae".
Wakawa wanashangaa sana maneno yangu na kusema,"mtu mwenyewe umebaki mifupa mitupu hata hujihurumii"
mimi niliendelea kumwabudu na kumtukuza Mungu nikiwa kitandani ndani ya miaka miwili.
Siku moja walikuja vijana wenzangu toka kanisani kwaajili ya kuja kuniona sitakanisahau siku ile, nilipofungua mlango tu wakaniona walilia sana huku wakigaragara chini vijana wakiume na wa kike wakatokwa machozi siku ile nikasikia wakisema " ee. Mungu mkumbuke mtumishi wako ukamtoe katika maangamizo haya, kumbuka alivyotumika mbele zako''
walipomaliza wakaondoka zao. Siku moja nilikuwa kwenye maombi nikasikia sauti ikisema nami.
"NITAKUPONYA KWA MAKUSUDI YANGU MWENYEWE ILI NITUKUZWE NDANI YAKO UKAIFANYE KAZI YANGU YA KUWAAMBIA HABARI ZA YESU"
Kwa kweli baada ya kusikia sauti ile nikasikia amani moyoni na furaha ya ajabu. ndipo baada ya miezi michache nikaanza kujisikia kupona, nikainuka kitandani ambapo nililala ndani ya ya miaka miwili, mara afya ikarudi mauti ikavulika ndani yangu nikawa hai tena. Familia na ndugu walifurahi kweli ikaandiliwa sherehe kubwa kwaajili yangu maana nalikuwa nife sasa ni hai. Nikafanya ibada ya kumshukuru Mungu kanisani kwangu na nikasimama mbele ya umati wa watu zaidi ya elfu moja kutoa ushuhuda huu ambao Mungu alinitendea watu wakatokwa na machozi siku ile wakashindwa kabisa kujizuia, maana kabla ya ugonjwa walinifahamu nilivyokuwa na afya,na baada ya ugonjwa waliniona wakati nilipokuwa kama skeletoni, na baada ya ugonjwa macho yao yakashuhudia Mungu akiniinua kutoka kitandani kwa muda wa miaka miwili
"Hakika Mungu wewe ni wa ajabu sana njia zako hazichunguziki pale akili zetu zinapoishia ndipo wewe unapoanzia,sitaacha kukutumikia maisha yangu yote maana umenipa kama nyara ndani yangu,"
nikikumbuka rehema za Mungu na fadhili zake, na upendo wake ndugu msomaji wa ushuhuda huu nafika mbaaali sana najiona si kitu mbele za Mungu. Nikikumbuka ule utukufu wa Mungu niliouona na raha ya kuwa naye dunia hii naina kama jalala, dunia hii naiona kama mavi.
Baada ya kupona nikaendelea kumtumikia Mungu aliye hai nikasema asante Jehova nimevuka majaribu haya mazito, kumbe safari bado inaendelea. Siku moja nilikuwa nimelala nikaona joka kubwa lilikuwa chini ya ardhi na watu walikuwa wakipita juu yake bila kumwona ila mimi nikiwa napita katika barabara ile aliyokuwepo nikamwona yule joka nikaanza kukemea kwa jina la Yesu Kristo, baadae nikashangaa watu wengi wakaanza kufurika lile eneo tukasaidiana nao tukamwua.Nikashangaa mimi nikawa na shukuru Mungu kwa joka yule kufa kwa namna isiyo ya kawaida huku nikikumbuka alivyokuwa mkubwa na wakutisha, ambapo upana wake ulikuwa kama unene wa mti wa mbuyu, gafla nikajikuta nimetoka yale maeneo na sasa niko chumbani kwangu, ghafla damu zikaanza kutoka puani mpaka zikajaa chumba kizima, majirani na ndugu wakawa wanashangaa wingi wa damu ile wakalia sana, na mimi nikasema Mungu naomba unisaidie, nikashtuka toka katika maono yale, baada ya kushtuka nikamwambia Mungu sitaki kuumwa tena kada kipindi kilichopita nisaidie Mungu wangu. Haikupita hata siku tatu Ghafla Siku moja kulikuwa na mkutano wa injili kanisani kwetu tena ilikuwa siku ya mwisho ya mkutano huku nimekaa ndani ya kanisa nikifanya maombi kwaajili ya mkutano kabla ya saa za mkutano. Nilisikia kama napaliwa na kitu kooni kwa nguvu nikatoka nje kwenda kutema mara nikakuta nid damu nyingi mbichi imatoka kooni nikashangaa sana, ikatoka kama muda wa dakika kumi ili kwa wingi sana na ilikuwa ikiruka kama bomba kutoka kooni kuja mdomoni. Kwa haraka nilijaribu kuwashirikisha watumishi wawili watatu wakaniombea kisha baada ya mkutano kuisha nikarejea nyumbani, damu ikaendelea kutoka kidogo kidogo ikabidi kesho yake niende hospital Amana kwaajili ya vipimo maana hakuna aliyeweza kujua damu zile zilikuwa zikitokea wapi. Walinipima kipimo cha O.G.D Kuangalia mfumo wa chakula kama either kuna vidonda vya tumbo lakini hakukuwa na vidonda vyovyote vilivyooneka ila waliona makovu ya vidonda yaliyopona ni jambo la kushangaza sana Mungu kaponya tena vidonda ambavyo sijawahi kujua kana ninavyo, nimeshikwa vidonda nipona pasipo kujua huu nao ni muujiza, na kwa haraka haraka nikasema moyoni huenda yale maombi ya kufunga siku nyingi yanaleta uponyaji, ndugu msomaji hebu jifunze kufanya maombi ya kufunga ,funga inaleta uponyaji. Pia kipimo kikaonyesha utumbo wangu umepanda juu na kujitundika na kusababisha ugonjwa unaitwa hernia sliding lakini katika ugonjwa huo hausababishi damu kutoka, huwa mgonjwa anapewa masharti ya kulala, na kula then ile sehemu au ule utumbo hurudi mahali pake. Madr. Wakaanza kuumiza vichwa ni ni kinasababisha damu kutoka, wakanipeleka hospital ya regency kwaajili ya .C T scan baada ya kufanya wakagundua pia nina tatizo kwenye mapafu yangu hivyo wakahisi damu inatokea kwenye mapafu na kupita njia ya hewa kuja mdomoni. Wakasema itabidi nipelekwe muhimbili ili wakafanye pia kipimo cha njia ya hewa kuanzia puani hadi kwenye mapafu. Baada ya kufanya kipimo kile wakagundua njia ya hewa haina tatizo lolote, wakacheck damu, pressure,x-ray, na vingine vingi hakuna tatizo lililoonekana. Wakasema inabidi kipelekwe . India kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kifua. Tulipatwa sana na mshtuko kama familia watu walilia kutwa kucha kama msiba, baadae profesa mmoja pale muhimbili akasema hakuna haja ya kwenda india oparation watafanya wao pale pale muhimbili wakaniambia nijiandae kwaajili ya upasuaji ambao kwa mujibu wa maelezo ya daktari. Walisema ni oparation ngumu sana, itafanyika takribani sa nne mpaka tano, nakukaa hospitalini wiki mbili, wiki moja nitawekwa medical i.c.u baada ya upasuaji huku.
Nikipumulia mashine, kwa kweli nilishtuka sana, lakini bado niliendelea kumwamini Mungu kwa uponyaji na bado hata kama ataruhusu oparation bado yeye Mungu hata katika hilo atajitukuza. Nilijaribu kushirikisha watu mbalimbali kuomba pamoja.
Siku moja wakati naendelea kumwomba Mungu, nikaona katika maono usiku waziwazi mtu mmoja aliyevalia nguo nyeupe sana alinishika mkono wa kulia, mtu yule kama alikuwa Yesu sijui, na kama alikuwa malaika sijua maana alinizuia kumwona sura yake nikawa naona vazi lake refu lilikuwa likiburuza chini, tukawa tukitembea sambamba hatua zetu pasipokupishana, na wakati amenishika ule mkono nilisikia raha ya ajabu na amani ambayo sijawahi kuipata dunia hii. Ila kilichonishangaza ni vile tulivyokuwa tukitembea ni kama vile tulikuwa tukiteleza. Tulitembea kwa miguu kwa mwendo mrefu sana lakini hatukuchoka ni kama mwendo wa siku nzima, wakati tunatembea alikuwa akisema nami ila sikuelewa ile lugha aliyokuwa anaitumia sijawahi kusikia duniani, aliendelea kuzungumza huku tukitembea ghafla ulikuja mlima mrefu sana ukafunika barabara yote hakukuwa na sehemu ya kupita, na ule mkono alikuwa bado kaushikilia nikajaribu kujivuta nijitoe mikononi mwake nikashindwa maana nilitaka kukimbia baada ya kuona ule mlima. Pale pale akasema nami na sasa alitumia lugha ya kiswahili naye alisema maneno haya. "USIOGOPE MLIMA ULE ,ILI KUSHINDA UTATUMIA MBINU ZOTE NILIZOKUFUNDI AWALI WAKATI TUNAKUJA NJIANI" Lakini cha kushangaza anasema nitumie mbinu zote alizonifundisha awali kumbuka kwamba wakati tunakuja njiani alitumia lugha nisiyoifahamu. Alipokwisha kusema maneno yale ule mlima ukatoweka mara tukajikuta tuko hospitali kubwa ambayo sikufahamu ni hospitali gani, akaanza kunitembeza hospitali yote huku akiendelea kusema nami kwa ile lugha nisiyo ifahamu na mkono akiwa ameendelea kuushikilia. Ghafla baada ya kumaliza maeneo yote ya hospitali tukawa tunaelekea kwenye geti la kutokea, pale getini tulimkuta daktari. Ambaye kazi yake ilikuwa nikuhakikisha anapima watu wote wanaotoka ndani ya hospitali ile nilisikia akitueleza tulimpomkaribia, ghafla yule mtu aliniachia mkono kwaajili ya kupimwa. Daktari akachukua kipimo akawa anapima kifua na kipimo kile kilikuwa na maumivu sana, alipomaliza anataka kutupa majibu tu yule mtu akatoweka na mimi nikashtuka toka kwenye maono yale. Niliposhtuka nifikiri sana juu ya maono yale nikajisikia furaha na kujua Yesu yuko nami kila mahali. Ukweli tuliendelea na maombi yetu pamoja na watumishi wa Mungu na nikapata uponyaji wangu nilipoenda kwenye vipimo nikaonekana sina tatizo lolote mpaka hapa nilipo ni mzima sina tatizo lolote. Hakika Mungu hafananishwi, wala halinganishwi na chochote uweza wake ni mkuu sana, una jambo gani linakusumbua, ni jaribu unalo ambalo Mungu haliwezi, tazama maisha yangu na majaribu yangu ndipo utakapoona uweza wake, Mungu ni halisi na yupo kwa wote wanaomtafuta, Okoka leo umpokee aanze kufanya kazi ndani yako asanteni sana kwa kuufatilia ushuhuda huu Mungu awabariki sana.
Hapa ndio mwisho wa ushuhuda wangu ntakutumia picha ya tangu nilipokuwa mgonjwa na sasa.
namba yangu ya simu.
0753-083230
MUNGU wa mbinguni akubariki sana.
Nakuomba songa mbele na BWANA YESU maana nje na BWANA YESU hakuna uzima wa milele.
Ni mimi Oliver Zakaria.
Comments
nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Nimeguswa sana na shuhuda zako ninaomba tuwasiliane na. yangu ni 0713 311 876
ninaomba yeyote atakayeona ujumbe huu anayemjua Oliver Zakaria amfikishie na yangu ya simu ili tuwasiliane.
Mungu awabariki sana
Mildred J. Kisamo