SILAHA YA MSAADA

Na Frank P. Seth

"Lakini lisikieni neno la BWANA, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia. Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu" (Yeremia 9:20,21).
Nilipokuwa mdogo, mama yangu mjane kule kijijini, hakunifundisha sana jinsi ya kupata pesa, wala hakunionesha mambo mengi yanipasayo kujua ili nifanikiwe kimaisha, ila alinifundisha KUOMBA Mungu. 

Sikujua kwamba nilijifunza jambo moja la muhimu kuliko mambo yote hadi nilipofika mahali na kujua kwamba katika mambo muhimu sana ambayo ni lazima UWEZE ni kuomba Mungu vizuri*.
Pesa au watu wana KIKOMO cha kukusaidia. Awezaye kuomba hana kikomo. Milango mingi sana iliyofungwa inafunguliwa kwa maombi. Ajuaye KUOMBA na mwenye bidii katika hayo maombi na KAZI, huyo sio mwenzako; atavuka vikwazo na vizingiti vingi sana na wala hamtakuwa ngazi moja, japo ni mwanadamu tu kama wewe. Nguvu ya MWOMBAJI ni zaidi ya mwenye PESA na AKILI, japo sipuuzi umuhimu wa kuwa na MAARIFA na kukaa vizuri na watu.

Maombi ni jambo la KIROHO linalofanyika kwa kutumia MWILI na AKILI, kwahiyo KUJIFUNZA na MAZOEZI ni muhimu ili kumfanya mtu awe mwombaji. Kama wewe ni mzazi, anza kuwapa watoto wako mazoezi ya kuomba. Hakikisha vipindi vya sala nyumbani watoto wanaZAMU za kuomba, na kusoma Neno. Kama ikiwezekana, kila siki wote wasome na kuomba (2-5Mins each).
Uzoefu unaonesha, kwa wastani watoto hawawezi kuomba zaidi ya dakika 5. Kama una watoto 3 inamaana dakika 15 zitakuwa za watoto kuomba kwa kupokezana. Kwa ujumla, dakika 20-30 zitatosha kufanya sala ya nyumbani. Baada ya muda wa mwaka mmoja utakuwa umejitengenezea JESHI la kukusaidia kupigana vita vya kiroho kwenye familia yako. 

Hata ukiwaachia watoto kwenda shule (boarding school - form one) unakuwa na amani kwamba watoto wako wanajua kukabiliana na mwaswala kimwili na kiroho. Usidanganywe, mwenye mazoezi ya muda mrefu ya KUOMBA ataweza kufanya vizuri zaidi ijapo wakati wa kushindana. Je! Hujui kwamba mashindano katika ulimwengu wa roho hayana kikomo? Wanao unawaachaje bila kuwapa huu ujuzi muhimu?
Frank P. Seth

Comments