SOMO: Siri ya kifo cha ghafla (Mtu wa ndani "Roho")

Na ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA, Ufufuo na uzima


Sisi wito wetu ni kurudisha watu walioibiwa. Kwenye Biblia tumeona Elia alimfufua mtu, tumeona pia Elisha alimfufua mtoto, mifupa ya Elia ilimfufua mtu, Yesu Kristo mwenyewe Bwana wa wokovu wetu alimfufua binti Yairo,
Yairo alikuwa anamfuata Yesu siku nzima mpaka jioni, Bwana Yesu akamwambia Usiogope mwanao ataamka, tunajifunza kinyume cha Imani ni uoga, unapokuwa na uoga maana yake huna imani. Yesu alikuja duniani kufundisha wanafunzi wake ili watende kazi yake. Kijana kwenye lango la naimu aliyekuwa amebebwa kwenye jeneza alifufuliwa na Bwana Yesu. Siku moja Yesu alipelekewa taarifa kwamba Lazaro wa Bethania ni mgonjwa ila hakwenda bali alisubiria mpaka alipokufa akazikwa akakaa siku nne kaburini, watu walizomea sana wakacheka sana kwasababu Yesu alichelewa kufika lakini Yesu alikwenda akawaambia ndugu yao atafufuka na akawaambia wamwonyeshe walipomzika na waliondoe jiwe ndipo akamwita Lazaro njoo na hapo Lazaro akafufuka.
Yohana 5:25
Tunatakiwa tuingie kwenye ulimwengu wa rohoni kwa kushinda rohoni kwanza baadaye tushinde mwilini. kuna nguvu zinazofanya kazi rohoni unashindwa rohoni kwanza baadaye unashindwa mwilini, unapigwa rohoni kwanza baadaye unapigwa mwilini. Lakini Silaha za vita zetu zina uweza katika Mungu hata kuangusha ngome, ina maana zipo ngome kwenye familia zinazotakiwa kuangushwa, kuna ngome za laana, ngome za magonjwa, ngome za kushindwa zinazotakiwa kuangushwa kwa jina la Yesu.
Imeandikwa 2 Wakorintho 10: 3 "Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo"
Waefeso 6; 12-17 Imeandikwa: "Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya aman.Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu"
2 Wakorintho 4:9 Imeandikwa"Twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi"
Ulimwengu wa rohoni ni halisi kuliko ulimwengu wa mwilini mfano mzuri Kabla Yesu hajazaliwa alikuwepo katika ulimwengu wa rohoni na alikuwa anaitwa NENO, hata leo vyote vinafanyika kwa huyo na pasipo yeye hakuna kilichofanyika
Yohana 1;1-2 Imeandikwa: "Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu."

Isaya 41: 10 U"siogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."
kuna wanaoshindana nawewe lakini watakuwa si kitu na wataangamia, sababu Bwana atakusaidia watakuwa kama kitu kisicho kuwa. Unatakiwa ufahamu kuwa wapo walioshindana na Bwana lakini hawakufanikiwa, wapo wafalme walioshindana na Bwana lakini hawakufanikiwa na utambue pia yeye ashindananaye na Bwana atapondwa kabisa. Usiogope hali uliyonayo. shetani anaogopesha ila yeye anaogopa kitu kimoja tu ambacho ni Neno la Mungu.
Ufunuo 19:13 Imeandikwa: "Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu."
Kuna ulimwengu wa rohoni na ulimwengu wa mwilini. unaweza kuhubiri maneno mazuri kwenye ulimwengu wa mwilini lakini usipo ugusa ulimwengu wa rohoni unakuwa hujafanya kitu.
Kwenye ulimwengu wa rohoni kufa sio kupotea, kuyeyuka wala kuzimia, Kufa ni kutoka nje ya mwili. Mwili ni kama nyumba ya mtu, na mtu anapotoka nje ya mwili anaitwa amekufa. Hakuna mtu ambaye aliwahi kukuona sababu unaonekana mtu wa nje ambaye ana kikomo chake hapa duniani (Udongo). Unaweza kuwa nje ya mwili watu wakasema umefariki na unaweza kuwa ndani ya mwili ukawa unaishi kwenye ulimwengu wa mwili.
Ukiwa nje ya mwili unakuwa mtu yuleyule, Gari haliwezi kwenda bila injini, vivyo hivyo mwili wako hauwezi kuishi bila wewe (roho) kuwepo ndani yake.

Roho ya mtu inapokuwa nje ya mwili tunasema mtu huyo amekufa, lakini ikiwa ndani ya mwili tunasema mtu huyo ni mzima. Mtu akifa anaingia kwenye raha ya ajabu hawezi kurudi kwa mapenzi yake mwenyewe labda Mungu awe na makusudi na mtu huyu kama hajamalizia kazi yake duniani.
Yohana 6:63 Imeandikwa "Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima."
2 wakorintho 12:2-5 Imeandikwa: "Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene. Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu."
Kile ambacho Biblia inasema kuhusu wewe ni ukweli kuhusu wewe lakini kile watu wasemacho kuhusu wewe sio ukweli kuhusu wewe, usiogope bali jiandae kwa mambo makubwa yajayo ambayo Mungu amekuandalia na usiogope kwa yanayokupata sasa hivi.
1 Yohana 4:2 Imeandikwa: "Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu"
Yesu kristo ni Mungu aliyekuja duniani akavaa mwili akaishi kwetu kama mwanadamu akapigwa kama mwanadamu.
Stori kubwa kuliko zote duniani ni Mungu kuvaa mwili akawa kama mwanadamu.
2 Yohana 1: 7Imeandikwa: "Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo."
Mathayo 27:50 Imeandikwa: "Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake."
Yesu aliamua kutoka ndani ya mwili wake akaenda chini kuzimu kule zilipokuwa roho za watu waliokufa kabla Yesu hajazaliwa. alipofika huko awatangazia kuwa yule waliyemsikia zamani kwamba ni nyoka wa shaba ndiye mimi, yule mliyekuwa mnamsiburia kwa hamu ndiye mimi nimekuja kuwachukua, na zamani kuzimu kulikuwa na sehemu mbili; za waliokufa watakatifu na wenye dhambi.
1Petro 3: 18 Imeandikwa: "Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri"
Mchawi ni nani?
Mchawi ni mtu yoyote (mtoto au mtu mzima) ambaye roho ya uchawi au jini wa uchawi linakaa ndani yake. Mchawi anapolala usiku, huamshwa na filimbi za kichawi ufikapo muda fulani maana wachawi nao wana filimbi zao "kama vile sisi tuliookoka tutakavyosikia parapanda ya Bwana Yesu atakapokuja kutuchukua" nao huamshwa kwa filimbi zao wanazozijua. Mtu huyu anapoamka Roho yake inatoka ndani ya mwili wake kwenda kuwanga/kuloga huku mwili wake unabaki nyumbani kwake ukiwa umelala.
kuna aina tofauti za uchawi
1. Kuna uchawi wa kurithishwa ambao mtu anaweza akawa ana roho ya uchawi amerithishwa lakini hajawahi kuutumia ama anautumia,
2. Kuna uchawi wa kununua ambao unanunuliwa kwa pesa nyingi.

Ayubu 4: 15 Imeandikwa: "Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama."
Kama ukifika mahali ukasikia nywele zinasimama fahamu mahali hapo kuna uchawi na mashetani na si uoga wa kawaida. Kama una nguvu za kushindana shindana nao lakini kama huna nguvu ondoka mahali hapo haraka, wachawi wapo na mchawi anaweza akawa mtu yeyote unayemtegemea na usiyemtegemea.
Wanyama wanaweza kuona "malaika" na wachawi.
Hesabu 22:23 Imeandikwa: "Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani."
Mungu anawapenda wanadamu wote.
Maombolezo 3:31 Imeandikwa: "Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele."
Mungu hatesi Wanadamu na ukiwa unateseka sio Mungu anayekutesa, ukiwa unaumia sio Mungu anayekuumiza bali wapo wanaokuumiza na hao ndio unatakiwa uwashambulie kwa jina la Yesu.
Kabla huja lala tamka maneno ya mamlaka juu ya wachawi na yatatokea vilevile kama ulivyotamka kwa jina la Yesu. usipende kulala kabla hujatamka maneno, jifunze kutamka maneno kwa imani na mamlaka na Mungu atayajibu.
Wachawi wanaweza kutoka wakaingia ndani ya mtu na kunasa, wakiwa wametoka ndani ya mwili wao, wanaacha roho ya kichawi ili iweze kubakia na mwili wa mtu.
Ukiri:
"Kwa jina La Yesu kuanzia sasa ndugu, rafiki , jamaa ambaye alikuja kuniloga na kubakia ndani yangu ninaamuru ondoka kwa damu ya Yesu.".... shambulia kwa mamlaka ya jina la Yesu wachawi na mashetani yanayokusumbua kwa damu ya Mwanakondo na utakuwa huru kwa jina la Yesu.

BAADHI YA SHUHUDA BAADA YA MAOMBI YA ASKOFU MKUU Dr JOSEPHAT GWAJIMA.
Binti mmoja amefunguliwa baada ya maombi. Anasema alikuwa amelala usiku akaota nyoka mkubwa amekuja kumshika mguu alipojaribu kumkung'uta hakuondoka na akashtuka usingizini na kulala tena, Askofu alimwombea ili amwone aliyejibadilisha na kuvaa umbo la nyoka aliyemwona, ndipo akamwona rafiki yake aitwaye Rehema ambaye walikaa pamoja na kulala pamoja. Mungu amemfungua uoga na magonjwa aliyokuwa nao na kuwa huru.
Binti mmoja ameeleza alipokuwa mdogo kuna mama aliyekuwa jirani yake alikuwa hawezi kuuza ice cream bila kumpa yeye aiuze ya kwanza, ameelezea siku moja alikataa kuuza hizo ice cream ndipo alipolala usiku akawaona wazee wawili nditoni wanamwambia lazima awafuate na baada ya hapo akawa anakula mkaa sana, alipojaribu kuja kanisani alijiskia kifua kinabana sana lakini akajitahidi kuja ndipo akaombewa na Askofu na kufunguliwa kwa jina la Yesu na yule pepo wa kula mkaa akamtoka kwa jina la Yesu.
Binti mmoja aitwaye upendo ameeleza kuwa wakati wa usiku alikua hawezi kulala sababu kuna bibi wa kijijini kwao huwa anamtokea na kumwambia lazima aende naye na siku nyingine anamjia kama bibi wawili na mtoto mmoja wa kike au anakuja kwa umbo la nyoka. Wakati mwingine huwa analala kanisani na harudi nyumbani sababu ya uwoga wa huyo bibi anayemtokea. Binti huyo amewekwa huru kwa Damu ya Bwana Yesu na kuwa mzima.
SHUHUDA NI NYINGI SANA NA ZOTE ZINAPATIKANA KWA MFUMO WA DVD KANISANI UFUFUO NA UZIMA__UBUNGO__DAR ES SALAAM__TANZANIA.

Comments