VITA DHIDI YA UFISADI

Na Frank P. Seth

"Enyi hayawani wote wa nyikani, njoni, Mle, enyi hayawani wote wa mwituni. Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi. Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote. Husema, Njoni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi" (Isaya 56:9-12).

Mara nyingi nimetafakari sana juu ya hii vita dhidi ya UFISADI na imenisumbua sana kwa maana hakuna namna FISI atalinda MZOGA bila kuula yeye mwenyewe kwa visingizio mbali mbali. Je! Ni nani aliye juu yetu kutuongoza?

Umewahi kujiuliza huu mfumo wa serikali nyingi duniani umetoka wapi? Yaani watu kupenda kujinufaisha kwa sababu wao ni WATAWALA na wanaUWEZO wa MAAMUZI? Usiangalie Africa tu, dunia imekubwa na ugonjwa huu wa kufisha.

Ukitaka kuangalia MFUMO wa serikali zinazopigiwa kelele sana duniani, angalia kwanza KANISA utaona kitu nasema. Kanisa kwa muktadha huu simaanishi mwili wa Kristo, ila MADHEHEBU na VIKUNDI vya huduma ambavyo ndani yake wamo Wakristo, au kanisa la Kristo. Nao wanatumia Jina la Kristo na Msalaba kufanya biashara zao japo wanahubiri Injili pia.

Angalia jinsi ambavyo Mungu anawaita WACHUNGAJI mbwa (Isaya 56:11); Kwa sababu ya CHOYO na KUTOKUSHIBA! Kila mmoja akigeuka UPANDE wake mwenyewe na kufuata njia zake kwa kutafuta FAIDA tena toka PANDE zote! Hao ni wachungaji! Yaani wanatafuta faida sio katika makundi yao tu, ila hata nje ya hayo, wakifanya hayo kwa MASILAHI BINAFSI huku wakisingizia kazi ya HUDUMA. 

Angalia neno hili, hukumu huanza kwenye nyumba ya Mungu kwa maana humo ndiko kuliko na CHUMVI na NURU ya ulimwengu. Kama chumvi imeharibika itafanywa nini hata ifae tena? Kama nuru imekuwa giza, giza litaondokaje? Na je! Kama misingi imeharibika, mwenye haki atafanya nini?

Kila nikitazama jinsi ambavyo MASKINI, YATIMA na WAJANE wamesahaulika KANISANI, naona sura ya SERIKALI nyingi sana duniani. Naona jinsi ambavyo mnyonge ananyongwa kwa sababu ya UMASIKINI wake, na wenyeNACHO wakifutiwa dhambi zoa kwa sababu ya mali na nafasi zao! Je! Kama haya yapo makanisani, kwanini tunyooshee kidole serikali zetu? Je! Tabibu akiwa mgoinjwa nani ataleta UPONYAJI kwa mwingine?

Tafakari jambo hili, ili tukatubu kwa ajili ya UOVU makanisani mwetu na kwa ajili ya VIONGOZI wetu humo, ili BWANA aturehemu na serikali zetu ZITAPONA pia. Maana maskini, yatima na mjane mahali pao pamefunikwa na dhuluma na upendeleo. RUSHWA na UFISADI vimeharibu matumaini yao hata watoto wao hawajui hatma zoa. Je! mataifa yetu yatapataje kupona? Ni nani basi anaona hili ili AOMBE na taifa likapate kupona?
Frank P. Seth

Comments