YESU KRISTO ndiye Mwokozi wetu.


Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Hii ni sababu muhimu sana na ya kwanza, yaani YESU KRISTO ni Mwokozi wetu.
Biblia inajulisha juu ya Mwokozi wa ulimwengu ambaye ni YESU KRISTO.


1 Yohana 4:14 '' Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu.'' 

Neno ''Mwokozi'' kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu maana yake ni ''mtu anayemtoa mwingine katika janga au hatari.''

Kwa maana hiyo , YESU KRISTO ni pekee aliyetoka mbinguni ili aje duniani ili kututoa sisi wanadamu katika janga liitwalo dhambi na amekuja kututoa katika hatari mbaya iitwayo ziwa la moto.
Mwokozi kazi yake ni kuokoa, KRISTO kazi yake ni kuokoa wanadamu wote wale wanaompokea na kutubu dhambi zao.

Mwokozi YESU ni Mwokozi wa ulimwengu wote, kama kuna mwokozi mwingine duniani hakika hata huyo anamhitaji Mwokozi YESU maana BWANA YESU ni Mwokozi wa waokozi wote
.
Jina lake tu ''YESU'' maana yake ''Mtu mwenye kuookoa.''
Jina YESU ni jina la kipekee kabisa likichaguliwa mbinguni, na aliyeleta jina hilo duniani ni malaika aliyetumwa na MUNGU.
Siku Malaika analeta jina hilo duniani alimwambia Mariamu kwamba 

''Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.-Mathayo 1:30-33

BWANA YESU alikuja na mamlaka ya milele.
BWANA YESU alikuja kumuokoa Mwanadamu.
BWANA YESU alifanyika Mwokozi kwa wanadamu wote watakaomtii.

Kazi ya wanadamu kuwaza uhuru kutoka nguvu za giza ikapata jibu baada ya Mwokozi wa ulimwengu kuja.

Kwa hiyo jina YESU maana yake ni mwenye kuokoa.
Siku Bwana YESU anazaliwa, Malaika wa MUNGU alitoa tangazo muhimu sana kwa wachungaji kondoo waliokuwa karibu na Eneo lile la Bethlehemu.
Malaika aliwaambia Wachungaji wale Neno hili;

'' Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, MWOKOZI, ndiye KRISTO Bwana.-Luka 2:10-11

Japokuwa BWANA YESU ni Mwokozi wa watu wote lakini hamuokoi mtu yeyote kwa kumlazimisha mtu huyo.
BWANA YESU anataka amwe Mwokozi na mfalme kwao tu walioamua kumtii kwa hiari yao wenyewe.

Zaburi 110:3-4 ''Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. BWANA ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.''
 
Watu wataamua kumfuata YESU kwa hiari yao.
YESU japokuwa ndiye aliywapenda kwanza wanadamu lakini hata hivyo hawalazimishi kumpokea kama Mwokozi wao, japokua hakuna mwokozi mwingine.
Mwanadamu ambaye anamkataa YESU maana yake anaukataa uzima wa milele.
Mwanadamu ambaye anamkataa YESU maana yake analitaka ziwa la moto.
Mwanadamu ambaye hamhitaji BWANA YESU maana yake huyo mtu hataki kuwa chini ya mpango wa MUNGU wa uzima wa milele.
Kwa wanaompokea YESU kama BWANA na Mwokozi wao Biblia iko wazi sana kuhusu wao ikisema;


'' kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.-Warumi 10:13''

Jina la YESU lipo na ni jina lenye uzima.
Kila mwanadamu atakayependa kuokolewa na Mwokozi hakika ataokolewa.
Wokovo ni mpango wa MUNGU kumtafuta mwanadamu ili huyo mwanadamu awe chini ya MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.
Wokovu una BWANA YESU pekee.
Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu wote.

Sababu muhimu sana ya kuamua kumpokea BWANA YESU ni kwa sababu BWANA YESU ni Mwokozi wa ulimwengu.


Yohana 3:17-18 '' Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments