UTOKAPO KWENDA VITANI


KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MBEYA SNP: EDWIN URIO

Kwa nini tupigane vita?
2 KOR 10:3 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ymwili;”
Neno linaonesha kuwa tunafanya vita, yaani duniani tumo vitani.
Maana ya vita
WAEFESO 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”
Vita ni mapigano. Ili kuwe na vita, lazima kuwe na pande mbili tofauti. Hivyo vita ni pande mbili zinazoshindana na kila upande ukiwa na nia ya kushinda. Pasipo vita hakuna kumiliki. Ukitaka kufanikiwa maishani lazima upigane.
UFUNUO 12:7-12 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Ili msalaba uonekane, lazima vita ipiganwe. Tumekuja au tuko Mbeya kupigana.
Leo tunampiga Lusifa na mahali pake hapataonekana. Tukipiga vita shida yako haitaonekana, itapotea. Kama vita ilipigwa mbinguni, kwa nini vita isipigwe Mbeya, Kyela, Mbarali. Lazima vita ipigwe. Watu wengi hawapendi vita. Kama hautapigana vita hautamiliki. Yaani hautakuwa na afya njema, fedha, elimu, biashara nzuri, mafanikio. Tumekuja kuijaza Mbeya na Ufufuo na Uzima. Tunataka kila ukipita kila mahali tusikie majeshi, majeshi na utukufu, utukufu. Bila hivyo hatutaenea mkoa wa Mbeya mzima.
Baada ya shetani yule joka na malaika zake kupigwa wakatupwa chini na mbinguni kukawa wokovu. Maana yake shetani alipokuwa huko mbinguni hakukuwa na wokovu, kwa vile kulikuwa na mbaya shetani. Ili Ufalme wa mbinguni uje, lazima vita ipigwe hapa duniani. Tukapewa ole ya nchi na bahari. Ole kwa vile alitupwa na kushuka akiwa na ghadhabu. Wakati mbinguni wakishangilia kuwa mbaya shetani ametoka na mahali pake pakaondolewa, hivyo hawezi kurudi huko, dunia,nchi na bahari ole wao. Kwa hiyo lazima kupigana.
Vita usipojipanga utashindwa. Vita ina gharama ya kifo/vifo. Unayemvizia kumpiga vitani naye amejipanga. Usipokuwa makini, yaani hujajipanga vizuri unaweza kupoteza ndoa, watoto, biashara, afya njema.
Kanuni za vita
Kwanza, kabla hujaenda vitani lazima umuulize Bwana.
YOSHUA 7:2-5 “Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu. Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji.”
Kabla ya vita Yoshua alituma watu wawili mji wa Ai, ili ajue adui zake wamejipangaje na wana nguvu kiasi gani, wakarudi wakisema ushindi ni wa uhakika kwa hiyo litumwe jeshi dogo. Kwa vile Mungu alipokuwa anamkabidhi uongozi alimweleza kuwa “kila mahali zitakapokanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa” na pia “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako”. Na kwa vile Yeriko alitumia mbinu hiyo hiyo ya kutuma watu wawili kupeleleza na akashinda vita, basi alitegemea kushinda Ai. Lakini hakuongea na Bwana kama alivyofanya Yeriko, wakapigwa huko Ai maana mmoja wao aitwaye Akani aliiba huko. Angemuuliza Bwana kabla ya vita, Bwana angeshiriki hiyo vita na wangeshinda. Lakini pia hapa tunajifunza kuwa ukiwa na maovu usipigane vita. Kwa ufupi usiwe na mazagazaga uendapo vitani.
Daudi alishinda Amaleki wakati wa mfalme Sauli kwa vile alimuuliza/alizungumza na Bwana. Hizi zilikuwa vita za mwilini, lakini vita yetu ni ya rohoni na mbinu ni hizi hizi.
KUMBUKUMBU LA TORATI 20:1 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.”
Cha kwanza “utokapo” maana yake ni mmoja, “adui zako” maana yake ni wengi. Na maneno ‘Utokapo kwenda vitani” maana yake uendapo kupigana. Tambua kuwa ukienda kupigana na mchawi mmoja, nyuma yake wapo 50 nk. Lakini hata wawe wengi kiasi gani, ukitangulia kumuuliza Bwana utashinda.
ZABURI 56:1-3 “Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita. Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;”
Nia ya adui kufanya vita dhidi yako ni kutaka kukumeza, lakini ameongozana na wenzake wengi ambao watashiriki kukumeza. Lakini wewe mtumaini Bwana, maana mwenye mwili hatakuweza. Adui wanataka kumeza biashara yako, ndoa yako, kazi yako, elimu yako, utendaji wako kanisani, kumeza kanisa lako. Kataa kumezwa kwa jina la Yesu. Kumbuka uendapo vitani lazima ujipange na lazima umuulize Bwana. Imeandikwa katika Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?”
Tukirudi Kumbukumbu ya Torati mlango wa 20 inaonyesha adui watakuwa wengi wakiwa na farasi na magari. Unaambiwa usiogope, maana Mungu yu pamoja nawe. Katika vita yetu adui yetu ana fedha nyingi au ni tajiri sana, au ni kiongozi mkubwa sana, au polisi wa cheo cha juu au jambazi; usiogope. Mstari wa 2 hadi wa 4 tunaambiwa acha hofu, usiteteme, usizimie moyo. Usifanye hivyo vitani maana ukiwa na hayo yatakurudisha nyuma na lazima utashindwa. Hata wawe wengi kiasi gani, Bwana ataandamana nasi vitani. Bwana anaungana nawe ukiwa njiani kwenda vitani na ndani ya vita.
YOSHUA 10:1-11 “Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyoushika mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya vivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao; ndipo wakacha mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa. Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia, Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli. Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na jeshi zao zote, na kupanga marago yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita. Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali maragoni, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; uje kwetu kwa upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu. Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote. Bwana akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.”
Kwanza Bwana alimhakikishia Yoshua ushindi (mstari wa 8) na wengi walikufa kwa mawe ya barafu ya Bwana kuliko waliouawa na wana wa Israeli. Ina maana Yoshua na jeshi lake wanapiga, Mungu anapiga zaidi, wanapiga na Mungu anapiga zaidi. Ukimuuliza Bwana kabla ya vita, atakuwepo kwenye vita yako katika ulimwengu wa roho. Imeandikwa Kutoka 15:1-3 “Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake.” Unapoanza kupigana, Bwana anatelemka kuungana nawe. Mnakutana vitani na Bwana. Sio rehema tu, baraka tu bali hata risasi, mawe, mishale, moto, nk. vinaweza kutoka kwa Bwana kupiga adui.
YOSHUA 10:14 “Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye Bwana kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa Bwana alipiga vita kwa ajili ya Israeli.”
Bwana atapiga vita kwa ajili yako. Bwana atapigana vita ya ndoa yako, biashara yako, madeni yako, kudhulumiwa kwako. Leo nakuambia adui yako hautamuona tena. Usiogope, ukishamweleza tu Bwana nenda vitani, Bwana yuko upande wako. We jitakase tu, kisha muulize Bwana, anza kupiga vita. Ukienda bila kujitakasa utapigwa.
2 Samweli 18:8 “Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga.” Ukitoka kwenda kupigana, Bwana huungana nawe. Bwana atajua. 2 Samweli 17:14 “Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.” Katika vita yako Bwana anaweza kuvunja jambo ambalo ni jema ili wewe ushinde.
1 WAKORINTHO 2:4-5 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.”
Katika vita yako, ifuate imani yako sio hekima za binadamu. Usishangae adui yako anakufuata kanisani, kwani huyo uliyeungana naye kwa ajili yako, yaani Mungu, anajua huyo anayekufuatilia atafanya nini. Usiogope kuwa wanakuja. We mwambie Bwana fungua njia. Tembea mbele. Hujiulizi kuwa hapa ilikuwa bahari, sasa pakavu. Badala ya kufurahia utukufu wa Bwana kwa aliyokutendea, unahofu wanaokufuata na unaangalia nyuma. Angalia ukubwa wa Bwana na uwezo wa Bwana. Usitazame binadamu wala usitazame hekima uliyonayo, tazama uwezo wa Mungu. We nenda mbele. Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.” Katika shida zako wakati ukipigana Bwana atakupigania. Utokapo kwenda vitani usiogope, usiyeyuke. Mfuate adui yako mpige. Usingojee akushambulie kwanza ndiyo upige. Awe shangazi, mama, mtoto, jirani, bosi kazini, rafiki, we piga tu. Unapoanza kupigana vita, Bwana mtu wa vita anashuka. Ngome za adui zako zitaanguka zote. Bwana atafungua njia zako na anayekuloga ataanguka, anayekutesa ataanguka, anayekudharau atakuheshimu na kila akutendeae mabaya ataanguka. Wewe songa mbele usigeuke nyuma. Mungu hapendi michanganyo, mara kwenye sherehe au mikutano ya kimila ya ukoo au jamii na mara uko kanisani. Mara uko kanisa hili lenye kuamini kupata chumvi, maji au mafuta toka kwa Askofu au mchungaji mara unakuja Ufufuo na Uzima. Mfuate yeye Mungu tu, utaishinda vita, Bwana atakupigania kwenye maisha yako.


UKIRI
Baba katika jina la Yesu. Naomba unisamehe makosa yangu, unitakase kwa makosa niliyofanya. Ninajitenga na mizimu ya ukoo. Naomba rehema zako. Imeandikwa Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Pia imeandikwa ole ya nchi na bahari. Adui ananikabili pamoja na wenzi wake. Najua natakiwa nijipange pamoja na kukuuliza wewe. Umesema Bwana hutaniacha, maana imeandikwa yu pamoja nawe. Pia imeandikwa Bwana ni mtu wa vita. Nami naenda vitani nikiomba iwe kama ulivyosema hapo zamani. Vita yangu ni katika ulimwengu wa roho. Nakumbuka katika ulimwengu wa mwili uliua watu wengi kuliko waliopigwa na upanga wa jeshi la Yoshua na pia wengi walioliwa na msitu kuliko waliouawa na jeshi la Daudi. Wewe ulisema usiogope. Nami sasa siogopi. Ninawaendea maadui katika vita hii kwa jina la Yesu. Ninasambaratisha ngome za hao wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota na washirikina. Awe baba yangu, mjomba wangu, rafiki yangu, mkuu mwenye cheo chochote ninampiga kwa jina la Yesu.Wale wanaomeza afya yangu, biashara yangu, mafanikio yangu ninawafyeka katika jina la Yesu. Imeandikwa nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo. Nami kwa damu ya mwanakondoo ninawapiga wote na kutangaza ushindi. Amen

Comments