Askofu Dr. John Kanoni Nkola ajiandaa kustaafu

Askofu Dr. John Kanoni Nkola wa Dayosisi ya Shinyanga AICT na Mkewe
Askofu Dr. John Kanoni Nkola wa Dayosisi ya Shinyanga, AICT, ametangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa mwaka mmoja wa kustaafu uongozi. Tamko hilo alitoa kwenye ibada maalum ya kuuzindua mchakato huo iliyofanyika Jumapili ya tarehe 5 Juni, 2016 katika kanisa kuu la Kambalage mjini Shinyanga. Akitangaza kuanza kwa mchakato huo, Askofu Dr. Nkola alisema, “Miaka 23 iliyopita, Bwana, kupitia uongozi wa kanisa, alinipatia jukumu la kuongoza Dayosisi hii. Na kazi hiyo nimeifanya kwa kumtii na kumwogopa Mungu.” 

Aliwashukuru wakristo wote, hususani wa kanisa kuu, kwa ushirikiano mzuri na mkubwa waliompatia katika kipindi chote hicho. Aliongeza, “Busara yenu na upendo wenu hakika vilinifanya niifurahie kazi hii.” 

 Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Silas Kezakubi ndiye alikuwa mhubiri katika ibada hiyo. Katika mahubiri yake, Askofu Kezakubi aliwahimiza wakristo wote kushrikiana na uongozi wa kanisa hilo katika kuweka njia madhubuti za kuwatunza watumishi wa kanisa hapo wanapostaafu. “Mungu hafurahii kuona watu waliotoa maisha yao kumtumikia Yeye, na wakatumika hadi kuishiwa nguvu, baadaye wanapostaafu wanaishi kwa machozi.” Aliongeza kuwa utaratibu uliopo kwa sasa ni wastaafu hao kutunzwa na Pastorate au Doyosisi wanamoishi. Alibainisha kuwa, “utaratibu huo umeshindwa kwani pastorate nyingi hazina uwezo wa kumtunza mtumishi anayezihudumia na pia kumtunza mstaafu”. Alieleza kuwa njia nzuri ilikuwa kuwekeza katika majengo kwenye viwanja vyetu na kuweka kando sehemu ya mapato ya majengo hayo kwa kuwatunza wastaafu. 

Awali, Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Jacob Pambana alitoa ufafanuzi juu ya namna kanisa litakavyomuaga wakati wa kustaafu. Akimkaribisha Askofu Dkt Nkola ili azungumze na wakristo waliokuwa wamefurika katika viwanja vya kanisa Kuu, Katibu Mkuu Pambana alisema, “Baba Askofu Dkt Nkola atastaafu kwa heshima tarehe 24 Oktoba, 2017 kipindi ambapo kanisa la Mungu AICT Dayosisi ya Shinyanga tutafanya Mkutano Mkuu wa Injili na sherehe za kustaafu kwake”. 

Wachungaji zaidi ya hamsini kutoka pande zote za Dayosisi hiyo walifika kuhudhuria ibada hiyo Waumini wa kanisa hilo walifurika mapema kwenye viwanja vya kanisa Kuu wakiwa na shauku kubwa kuwaona na kuwasikia viongozi wao wa kiroho. Vikundi mbali mbali vya kwaya vilitumbuiza kwenye sherehe hiyo, kikiwemo kikundi cha wapiga tarumpeta. 

Baada ya ibada, wakati wa jioni, kwaya ziliendelea kutumbuiza na hatimaye sherehe hiyo ilikamilirishwa kwa walimu wa kwaya wote waliokuwepo kuanzisha umoja wao. Huu ndiyo umoja wa kwanza kabisa kuundwa na waalimu wa kwaya katika kanisa la AICT. Askofu Dkt Nkola, ambaye ndiye aliyesimamia uanzishwaji huo alieleza matumaini yake kuwa waalimu wengine wa kwaya watajiunga na umoja huo. Waalimu wa kwaya wamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza katika kanisa la AICT.

Comments