HUDUMA NA WEWE

na Frank P. Seth

“11Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 12kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe” (Waefeso 4:11 & 12).
Nimetazama katika maandiko ili kutafuta tofauti ya HUDUMA au KARAMA walizonazo watu, na MAJINA au MAHALI wanakotumika na kuona mambo yafuatayo:
i. Hawa wenye huduma hizi: mitume, manabii, wachungaji, waalimu, wainjilisti, nk. waliitwa kuwa hivyo. Ni habari ya WITO, na “wakatolewa” kwa ajili ya hiyo huduma.
ii. Nimejiuliza sana ni kwanini MAHALI mtu afanyapo huduma ni muhimu kumthibitisha (qualify) huyo mtu kuwa na hiyo HUDUMA yake?

Sasa angalia, katika maandiko kuna watu waliitwa majina kwa sababu ya KAZI zao, kwa mfano nabii Elia, Mtume Paulo, Yohana Mbatizaji, nk. Ukiangalia WASIFU wa hawa watu, hawakuanza na JINA bali KAZI zao. Yale mambo waliyofanya ndio yaliwapa majina. Kwa mfano, pamoja na kwamba Yohana Mbatizaji aliamua kujiita “suti ya mtu aliaye nyikani”, kwa sababu alibatiza watu akaitwa “mbatizaji”, na kwa sababu ya utaratibu wa maisha yake, wakamwita nabii, tena wakimfananisha na nabii Elia. Je! Si kazi zake zilimpa majina yake, naam, na cheo pia?
Kwa habari ya MAHALI, nikaona shida hii juu ya nchi, asiye na kanisa sio mchungaji kwa maana hana JENGO au MAHALI ambapo watu wanakusanyika chini yake! Je! Umejiuliza kwamba Yesu aliitwa Mchungaji ila hakuwa na jengo, chumba cha darasa au mti fulani maalumu wa kuendeshea ibada? Angalia mitume na watumishi wengine wa zamani, MAHALI haikuwa KIGEZO muhimu na cha pekee cha kuwa na huduma fulani ila KAZI zao walizotenda.
Nikiandika waraka huu, nazungumza na wengi “waliotolewa” kwa ajili ya huduma fulani lakini HAWATAMBULIKI wala HAWANA nafasi popote walipo. Nakupa shauri, fanya kazi ya HUDUMA kama ulivyoitwa kwa maana ipo siku ya kutoa hesabu. Sio kazi yako kujiita majina, lakini watu wakiona kazi zako watakupa jina lako stahili.
Angalia, mahali ni muhimu sana na ukubali kuwa chini ya mchungaji wako kwa maana mpo wengi humo wenye huduma nzuri na nzito tu; fanya kazi yako kwa bidii, acha wengine nao wafanye kazi zao. Usitafute NAFASI ukidhani ili kutumika hiyo nafasi ni kitu cha muhimu sana. Mjue Mungu ili uwe na amani na kufanikiwa kwako kutakujilia na kukupata. Kuzaa matunda ni kitu cha kipaumbele sana bila kujali jina, cheo wala mahali ulipo.
Umewahi kuona shida hii, wapo wenye majina pasipo kazi na wenye kazi pasipo majina? Na, umeona wenye mahali (nafasi) bila kazi na wenye kazi bila mahali? Ndipo mtumishi mmoja wa Mungu (jina limehifadhiwa) akasema, “ukiona baba ni askofu, mama ni mchungaji kiongozi na watoto ni wachungaji wasaidizi, jua hapo ni biashara ya familia”. Najua wanaweza kuitwa kama Mungu apendavyo, je! Ni Mungu?
Tazama jambo hili, makanisa ni taasisi kama zilivyo taasisi zozote zilizoundwa kisheria. Majina yasikusumbue, huku kwenye taasisi zingine wanaitwa wakurugenzi, kanisani wanaitwa maaskofu; huku wanaitwa mameneja, kanisani wanaitwa wachungaji; huku wanaitwa wahudumu, kanisani wanaitwa mashemasi, nk. hii ni mifumo tu, isikupe shida. Cha muhimu, je! Unafanya kazi ya huduma? Jina na cheo unaweza kupewa na taasisi au kanisa lako, je! Unafanya kazi sawa na hilo jina? Je! Umeitiwa hiyo nafasi na jina husika?
Frank P. Seth

Comments