JE UNAITII SAUTI YA MUNGU ILIYOSEMA NA WEWE?

Na Mtumishi Peter Mabula

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze  Neno la MUNGU.
MUNGU husema na watu wake.
MUNGU husema na wateule wake.

Amosi 3:7 Biblia inasema ''Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.'' 

MUNGU amejiwekea utaratibu wa kuongea na watu wake.
Zamani MUNGU alikuwa anaongea na manabii tu ambao ni watu wachache aliowateua ili kufikisha kusudi la MUNGU kupitia kile walichoambiwa na MUNGU, Lakini  baada pazia la hekalu kupasuka siku ile BWANA YESU anaukamilisha wokovu kwa sasa kila Mteule wa KRISTO ni kuhani kwa MUNGU na MUNGU anaweza kusema nae jambo lolote, liwe la kanisa au liwe la jamii au liwe la kwake binafsi. Kizuri zaidi ni pale ROHO MTAKATIFU alipoanza rasmi kuishi ndani ya wateule wa KRISTO maana yeye ndio ukamilisho wote.
Watu wa MUNGU leo huisikia sauti ya MUNGU, Huelewa kile MUNGU anasema.
Kuna namna nyingi ambazo MUNGU anaweza kuongea na mwanadamu. Kuna njia ya ndoto, kuna njia ya Neno, Kuna njia ya maono, Kuna njia ya watumishi wake, kuna njia ya mazingira, kuna njia ya Malaika N.k.

Kumb 4:35-36 ''Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye MUNGU, hapana mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto. '' 
 
Je, wewe MUNGU amewahi kuzungumza na wewe kwa njia gani?
Je, huwa unaitunza sauti ya MUNGU inaposema na wewe?
Kuna watu hutunza sauti tu zile za baraka lakini sauti ya maonyo huipotezea.
Inawezekana kuna wakati MUNGU alikuwa anasema na wewe kila mara lakini baadae kwa sababu ambazo wewe huzijui sauti ile ikakoma kabisa.
Mimi kwa ufunuo ninasema kwamba ile sauti kuirudisha ni kwa njia ya toba tu.
Mfano kuna vitu MUNGU akikuambia ni kwa sababu anataka wewe uombe na sio utangaze kwa watu, sasa kama utaendelea kutokuwa muelewa basi MUNGU ataacha kusema na wewe. 


Najua utajiuliza sana ''kwanini kwa sasa MUNGU hasemi na mimi?'' jibu ni kwamba unatakiwa utubu ndipo sauti ile itarudi tena.
Kuna vitu MUNGU akikuambia ni kwa ajili yako binafsi tu.
Kuna vitu MUNGU akikuambia labda ni kuhusu mtu fulani, wewe unatakiwa umfuate huyo mtu na kumsaidia vile ulivyoelekezwa kwa sauti ile ya MUNGU. Sasa wengine akiambiwa tu na MUNGU kuhusu mtu fulani basi kazi yake itakuwa kuwatangazia mtaa mzima, kufanya hivyo kwa muda mrefu kunaweza kuiondoa sauti ya MUNGU kwako.

MUNGU huwa hasemi uongo hata siku moja na MUNGU huwa hasemi jambo la kukufanya uingie katika dhambi hivyo uwe makini katika kuisikiliza sauti ya MUNGU.

Hesabu 23:19 ''MUNGU si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?''


MUNGU alisema na Mfalme Hezekia kupitia Nabii Isaya, kwa utii ule wa sauti ya MUNGU ugonjwa ukaondoka kwa Mfale Hezekia, tena kwa utii huo wa sauti ya MUNGU akaongezewa miaka ya kuishi na mji wake ukaokolewa.
Ibrahim aliitwa atoke katika nchi yake ya Uru ambako watu wa kule walikuwa wanaabudu miungu.
Kutii kwa Ibrahimu kulileta baraka kuu hata leo.
Ibrahimu kwa kuitii sauti ya MUNGU leo ndiye baba wa imani, leo Ibrahimu ndiye Chimbuko la Taifa la Israeli.
Je wewe huwa unaitii sauti ya MUNGU?
Inawezekana kabisa MUNGU husema na wewe kila mara kupitia Mchungaji wako lakini wewe umeshupaza shingo ndio maana hufanikiwi.
Inawezekana kabisa MUNGU husema na wewe kupitia watumishi wake kwa njia nyingi kama hivi leo lakini hujawahi kumtii KRISTO kupitia ujumbe huo unaofundishwa.
Hata kwa ujumbe huu MUNGU anaweza kuwa anakusemesha kitu hivyo ni wajibu wako kumtii MUNGU kupitia Neno lake.
Manoa yeye alitokewa na Malaika wa MUNGU na kumweleza ujumbe wa MUNGU.
Yusufu yeye aliambiwa na MUNGU kutitia ndoto  na ndoto hiyo ikaja kutimia.
Yahazieli yeye alisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU ndani yake akawaambia Waisraeli na mfalme Yehoshafati kwamba vita wala sio yao ila ni ya MUNGU hivyo MUNGU atawaokoa kutoka kwa maadui wabaya. Ni kweli MUNGU akawaokoa kiajabu sana na wakamtukuza MUNGU.
Je MUNGU husema na wewe kwa njia gani?
Je unaitii sauti ya MUNGU?
Jambo la kukumbuka ni kwamba sio kila sauti unayoisikia ni ya MUNGU.
Sio kila unachokiona katika maono au ndoto ni sauti ya MUNGU.
ROHO MTAKATIFU anahitajika ndani yako ndipo utaweza kujua kama ni MUNGU anasema na wewe. lakini MUNGU husema sana na watu wake hivyo usipuuzie ila mwiite ROHO wa KRISTO akujulishe.

Matendo 15:17-18 ''Ili wanadamu waliosalia wamtafute BWANA, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; Asema BWANA, ajulishaye hayo tangu milele.'' 

 MUNGU husema na watu wake na hujulisha.
Wakati mwingine MUNGU hawezi kusema na mtu jambo ambalo mwanadmu huyo sio zaidi yake.
Kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu imani nayo ni muhimu sana.
Kuna watu kama wakiambiwa kwamba mpendwa wao ambaye amelazwa hospitalini hatapona wanaweza wakafa wao kwa presha kabla hata ya huyo mgonjwa kufariki.
Kuna watu wana wachumba waliojichagulia wenyewe lakini sauti ya MUNGU ikija na kusema kwamba ''Huyo hutamuoa/hatakuoa'' wanaweza kufunga hata siku 10 ili tu kukemea jambo hilo wakidhani labda sio MUNGU aliyesema.
Hayo yaliwahi kunikuta hata mimi kabla sijaoa.
MUNGU alikuwa anasema na mimi lakini sikuamini kama ni MUNGU hadi yalipokuja kutokea ndipo nikajua. nikagundua kwamba  nilitumia nguvu nyingi sana ambazo ni heri ningeitii ile sauti ya MUNGU iliyosema nami.
Kuna watu hawawezi kuambiwa vitu ambavyo sio saizi yao hivyo wanatakiwa waongeze imani zao kwa kuomba sana, kusoma Biblia na kuitafakari sana pamoja na utakatifu sana.
Ndugu mmoja kutokea Ukanda wa ziwa Victoria aliniambia habari za ugonjwa wa Babu yake. Katika maombi niliona kwamba yule Babu hatarudi bali ataondoka, maana yake atafariki. Nilichokifanya sikumwambia mtu yeyote ila nilimwambia ndugu mmoja aende akamuongoze sala ya toba yule babu na kumfundisha habari za uzima wa milele katika KRISTO. Yule ndugu akumuongoza sala ya toba na baada ya siku chini ya 7 Yule Babu akafariki.
Katika kuizungumzia sauti ya MUNGU hapo ningemwambia yule babu kwamba atakufa ningeharibu.
Ningewatangazia watoto wake yule Babu kwamba atakufa wangenishangaa sana.
Ningetangaza kwa marafiki na watu wote ninaofahamiana nao juu ya kifo cha yule Babu hakika ningegeuka kituko kikubwa na kwa MUNGU ingekuwa ni makosa. Ndio maana nakuambia kwamba sio kila kitu ambacho MUNGU anasema na wewe unatakiwa kukitangaza.





1 Wafalme 17:2-6 ''Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema BWANA; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.''




Eliya hapa aliisikia sauti ya MUNGU ikimuelekeza jambo la kufanya. ilikuwa ni kipindi cha njaa katika Israeli. Kama angewatangazia watu na hakika wangemtangulia kule alikoambiwa na MUNGU aende.
Wangemkamata maana alikuwa anatafutwa na mkuu wa nchi.
Wangekuwa karibu na alipo ili kila kunguru wakileta chakula wanawafukuza.
Ni muhimu sana kuitunza sauti ya MUNGU na kuitii.
Ni muhimu sana kujua ni nani wa kumweleza kile ambacho MUNGU amesema na wewe.
Jambo la kujua jingine ni kwamba MUNGU hasemi jambo lililo kinyume na Neno lake Biblia takatifu.
Kujua jambo ambalo limetoka kwa shetani ni rahisi sana maana jambo hilo litakuwa linapingana na Biblia.
mengine shetani hujaribu kuwahadaa watu kwa kuchanganya uongo na ukweli lakini ROHO MTAKATIFU hujulisha hivyo baada ya kuokoka unatakiwa umuhitaji sana ROHO MTAKATIFU.
Sio kila unachoambiwa na MUNGU lazima usiseme. Uwe makini maana mengine kusema kwako ndio kupona kwako.

Mimi nakushauri MUNGU akisema na wewe jambo mtu sahihi wa kumweleza mweleze Mchungaji wako maana atakusaidia, Kama ROHO wa MUNGU anakutataza kumwambia acha maana sio yote ya kumwambia yeyote, Mengine unafanya tu kama Eliya kwa kutembea kwenye sauti ya MUNGU uliyoisikia.
Kuna watu wengine ukiwaambia kile ambacho MUNGU amesema na wewe watakuja kinyume chako na kukuharibia baraka yako.
Mfano binti au kijana baada ya maombi kwa ufunuo umehakikisha kwamba wewe utamuoa/kuolewa na fulani, baada ya hapo wewe badala ya kuomba na kukaa kimya ndio unaanza kumtangazia kila mtu kiasi kwamba unaweza kuja kuona yule yule ambaye alipaswa kuwa wako, utamuona anaolewa au kuoa mwingine kwa sababu hukujua ufanyeje baada ya MUNGU kusema na wewe.

Usikubali kutafuta sifa katika kile ambacho MUNGU amesema na wewe.
MUNGU akisema na wewe Mshukuru na kitendee kazi kitu hicho.
Tendea kazi kwa maombi na kama kinaruhusika kuomba ushauri basi watafute watumishi wa BWANA YESU wakusaidie
Kama kitu hicho kinakutaka ubadili tabia hakika badili tabia maana usipobadili tabia itakuwa hatari kwako.
Kuna watu sauti ya MUNGU ya kuwaonya huja kwao lakini wao hushupaza shingo na kumbe mwisho wao umefika hivyo wanapishana na uzima wa milele.


Yakobo 4:7 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.'' 

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments