MAOMBI YA KUOMBA NGUVU ROHONI NA MWILINI ILI ZIONGEZEKE.


Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe
Karibu tujifunze kisha tuombe maombi ya ushindi kupitia jina la YESU KRISTO.
Inawezekana kabisa nguvu zako za kuvumilia katika hali uliyopo imepungua japokuwa ushindi wako uko karibu sana kuja.
Inawezekana kabisa nguvu za kusonga mbele ukiwa yatima zimepungua japokuwa ukivumilia huku ukiomba na utakatifu utastawishwa sana na BWANA YESU.
Labda wewe ni mjane na hujui utaishije baada ya kuondokewa na mpendwa wako, iko nguvu ndani ya damu ya YESU na jina la YESU KRISTO inaweze kukuletea ushindi mpya.
Inawezekana kabisa nguvu za rohoni kwa sasa kwako zimepungua na hujui kwanini zimepungua, hujatenda dhambi wala hujaacha kuomba lakini unajiona unapwaya tu.
Leo naomba tuombe ili tuongezewe nguvu na MUNGU wa mbinguni.
Neno la MUNGU linasema kwamba MUNGU ''Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Isaya 40:29 ''

Kwa sababu BWANA huwapa nguvu wazimiao basi leo omba nguvu za kushinda.
Omba upate nguvu za kumtumikia.
Omba upate nguvu za kuwakabili watesi wako.
Omba upate nguvu za kusonga mbele katika wokovu wa BWANA YESU.
Inawezekana kabisa unajiona huna uwezo wa kuwakabili hao wanakuharibia ndoa yako lakini kwa maombi ya leo BWANA YESU akupe ushindi.
Inawezekana kabisa wachumba kwako hupeperuka kama karatasi, kila ukipata mchumba anakukataa tu ghafla bila sababu za msingi, leo omba nguvu za kushinda.
Kama huna nguvu ni ngumu kumshinda adui mwenye nguvu, chanzo cha nguvu zako ni BWANA YESU hivyo mwite akushindie leo.
Biblia hapo juu inasema kwamba MUNGU huwaongezea nguvu hao wazimiao.
kama unazimia kutokana na hali unayopitia nakuomba leo upate nguvu za kushinda kwa jina la YESU KRISTO.
BWANA atalituma Neno lake ili likuponye.
Neno atakalolituma BWANA ni nile Neno la maombi utakalonitamka kwa imani baada ya kuomba toba.
Neno hilo ni matamshi utakayokuwa unayatamka wewe kupitia maombi yako leo maana YAHWEH ''Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Zaburi 107:20''

Kuomba sawasawa na mapenzi ya MUNGU ni kulipokea Neno lililobeba ushindi wako.
Maombi ni silaha muhimu kuliko zote ya kumshinda adui yako.
Maombi ni mkono mrefu zaidi wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
Jina la YESU KRISTO lipo na damu ya YESU KRISTO ipo hivyo kazi iliyobaki kwako ni kuomba tu kwa imani iliyojaa utakatifu wa kweli.

MUNGU wa mbinguni anasema ''Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini.-Malaki 4:2''
Ni wakati wako wa kuchezacheza kama ndama baada ya ushindi kwenye hitaji lako.
Muhimu tu hakikisha unaishi maisha matakatifu huku ukiomba maana maombi bila utakatifu ni kelele tu mbele za MUNGU.
Maombi bila imani ni kubahatisha.
Hapa hatutaki kubahatisha bali kupokea.
Omba leo BWANA YESU akupe nguvu za kushinda, jinyenyekeshe chini ya Mkono wa BWANA ulio hodari hakika unaenda kupokea.
Ombi langu BWANA YESU akuongezee nguvu na kukushindia leo.
Yale ya baraka ambayo hayajawahi kuwezekana kwako yakawezekane sasa kwa jina la YESU KRISTO.

Maombi haya chini naomba yamsaidie muombaji mchanga ili ajue kuomba na ajue kuliendea hitaji lake kupitia maombi atakayoomba mwenyewe.

MAOMBI YA KUOMBA KUONGEZEWA NGUVU.

JEHOVAH MUNGU wetu uhimidiwe na uabudiwe milele.
Nakushukuru muumba wangu kwa uzima na ulinzi katika maisha yangu.
Ninaishi kwa sababu wewe MUNGU wangu umetaka niishi.
Nitashinda magumu yote kwa sababu wewe BWANA utanishindia.
Katika jina la YESU naamini umo ushindi wangu.
Nakuamini BWANA YESU na naziamini kazi zako.
Naomba MUNGU wangu ulipe nguvu za kusonga mbele.
Nipe kukuangalia wewe tu na kukutegemea wewe tu mfalme wa uzima. nipe nguvu za rohoni na mwilini ili niwe mshindi katika maisha yangu.
Nakataa kila mipango ya kipepo inayoondoa nguvu zangu za kiroho.
Nafuta kila maneno mabaya yaliyotamkwa na maadui zangu ili kunifanya niwe mnyonge.
Kuanzia sasa nashinda kwa jina la YESU KRISTO.
kwa sasa ninapokea nguvu za MUNGU na hakuna adui yangu atakayesimama katika maisha yangu.
Wanaoifuatilia ndoa yangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wanaofuatilia uchumi wangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wanaofuatilia wazazi wangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wanaofuatilia kazi yangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wanofuatilia uchumba wangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wanaofuatilia mali zangu nawaharibu na kuwashinda leo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila anayefuatilia kitu changu namharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mimi ni mshindi kuanzia leo kwa jina la YESU KRISTO.
Asante BABA wa mbinguni kwa kunishindia.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea.
Amen Amen.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments