MWISHO UPO NA UTAFIKA SIKU MOJA.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Mwanadamu yeyote anapozaliwa huwa kuna furaha kuu katika familia hiyo, lakini wakati wa kufariki huwa huzuni na vilio vingi vinatawala. hakuna mwanadamu anayependa kifo japokuwa kifo kipo kwa kila mtu.

 Ayubu 14:1-2 ''Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.''

Huo ndio ukweli kwamba siku za kuishi mwanadamu sio nyingi  ukilinganisha na milele ijayo.
Japokuwa kuna mwisho wa kuishi mwanadamu duniani lakini pia kuna siku ya mwisho ambayo ndio kila mtu atahukumiwa sawasawa na matendo yake aliyokuwa akiyatenda alipokuwa akiishi duniani.


Kwa wateule wa MUNGU jambo muhimu kujua sio kwamba anakufaje bali muhimu ni kwamba anamalizaje mwendo.
Je anamaliza mwendo na wokovu?
Je unamaliza mwendo na utakatifu
Je umevumilia mpaka mwisho maana atakayevumilia katika YESU hata mwisho ndio atakayeokoka.

Mathayo 10:22 ''Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. ''

Mwisho huwa haujulikani utakuja lini ndio maana kuna wanaofariki wakiwa watoto, wengine wakiwa wazee na wengine wakiwa vijana.
Muhimu ni kuishi maisha matakatifu ya wokovu siku zote za kuishi duniani.
Kama umekuwa mtu wa kuanguka na kuinuka hakikisha unainuka na kutokubali kuanguka dhambini tena.
Mwisho upo na utafika siku moja.

1 Thesalonike 4:16-17 '' Kwa sababu BWANA mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.'' 

Huo ndio mwisho yaani BWANA YESU kuja na kuhukumu wazima na wafu ili kila mwanadamu avune alichopanda alipokuwa akiishi duniani.
Kama kuna jambo muhimu sasa kwa kila mwanadamu ni kumpokea BWANA YESU kama BWANA na Mkombozi wake.
Kama kuna jambo muhimu sasa kwa kila mteule wa KRISTO ni kuishi maisha matakatifu.
Kama kuna jambo muhimu sana ni kujitenga na dhambi na kila uovu.
Ni muda special  kutoka kwa MUNGU kuja kwetu kwamba tuishi maisha matakatifu.
 Utakatifu Hautegemei Sura Ya Mtu Au Ukimya Wa Mtu. Utakatifu Hautegemei Mtu Kuomba Kwa Sauti Kubwa Wala Kuomba Kimya Kimya. 
Utakatifu Hautegemei Kuitwa Mchungaji Au Kuitwa Muumini. Utakatifu Hutegemea Mtu Kuacha Dhambi Na Kuanza Kuishi Maisha Mema, Utakatifu Hutegemea ROHO MTAKATIFU Kuwa Kiongozi Wa Maisha Ya Mtu Huku Mtu Huyo Akimtii ROHO MTAKATIFU. Utakatifu Ni Kumcha BWANA YESU Katika Yote.

Yoshua 24:14 '' Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA. ''

Wisraeli walionywa kwamba wamche MUNGU kwa unyoofu wa mioyo na kweli. Waliambiwa waiweke mbali miungu walioitumikia wazazi wao na sasa wamtumikie BWANA peke yake.
Hata leo Neno la MUNGU hilo linamtaka kila mwanadamu amche BWANA siku zote za maisha yake.
Kila mmoja wetu anatakiwa amche MUNGU katika hali zote za maisha.
Kumcha MUNGU maana yake ni Kumpenda MUNGU na kumwogopa ili usimkosee.
Huu ni wakati wa kuachana na miungu ya kabila au ukoo ili uliishi Neno la MUNGU katika KRISTO.
Huu ni wakti wa kujitenga na mizimu ya ukoo.
Ni wakati wa kujitenda na kila matambiko ya mababu.
Ni wakati wa kumcha MUNGU aliye hai.
Kama unaabudu miti acha.
Kama unaabudu pesa au watu acha.
Ni wakati wa Kumwabudu MUNGU wa mbinguni kupitia YESU KRISTO mfalme wa uzima wa milele.
 Hizi ni siku za mwisho zenye mambo mengi mabaya sana.
Lakini parapanda italia na wafu watafufuka, hukumu itatolewa na waongo waliomkataa YESU KRISTO wataabika.
wahubiri wanaodanganya watu kwa kuwatoa kwa YESU siku hiyo wataabika.
Hizi ni siku za mwisho za kila mmoja kuwa makini maana Biblia ilikwisha onya mapema sana.
Siku Za Mwisho Wataibuka Matapeli Watakaojiita Kristo Na Katika Siku Hizo Za Mwisho Watatokea Matapeli Wengi Ambao Biblia Inawaita Manabii Wa Uongo.
Biblia inasema '' kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule. Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele. -Marko 13:22-23''

 Hao ni Mawakala Wa Shetani Kwa Lengo La Kuwatoa Watu Kwenye Wokovu Wa BWANA YESU. 
Mteule Nakusihi Uwe Macho Maana Nje Ya Wokovu Wa KRISTO Kuna Mawakala Wa Shetani, Nje Ya KRISTO Kuna Shetani. Ukimdharau YESU KRISTO Na Neno Lake Hakika Utadharauliwa Siku Ya Mwisho. Okoka Na Ishi Maisha Matakatifu Siku Zote.

Mwisho upo na utakuja siku moja.
Kuna maisha baada ya kufa.
=Waliokufa bila dhambi huenda mbinguni sehemu ya kungojea siku ya mwisho maana hao ni watakatifu.
=Na watenda dhambi wasiookoka huenda kuzimu kama sehemu ya kungojea siku ya mwisho.

Watakatifu mbinguni huonana na kumwabudu MUNGU Kwa furaha kuu ila mbinguni hakuna mwanaume wala mwanamke Bali huishi kama malaika

Mwisho upo na siku moja utafika.
ukisoma 1 Thessalonike 4:13-14 inaonyesha kwamba wateule walio hai duniani hawatamtangulia mteule aliyekufa hata mmoja katika kumlaki BWANA YESU.
Unajua kwanini?
Ni kwa sababu mteule anapokufa huenda mbinguni katika eneo la mangojezi ya siku ya mwisho baada ya siku ya mwisho kinafuata kuvikwa taji tu na kuingia Uzima Wa milele.

Lakini watenda dhambi wakifa huenda kuzimu kwenye mangojezi tu wakisubiri kwenda ziwa la moto.
Ufunuo 20:6 inasema  ''..... Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. '' 

heri mtakatifu aliye na Ufufuo baada ya mauti ya kwanza maana mauti ya Pili haitamhusu.
Mauti ya pili ndilo ziwa la moto ambalo litawahusu tu waovu.
Ndugu yangu usijisahau katika maisha haya.
Kazi yako isikusahaulishe hata ukamsahau BWANA YESU mwenye uzima wako.
Uchumi wako usikuondoe kwenye wokovu wa BWANA YESU.
Kutaka kuolewa au kuoa kusikufanya umwache BWANA YESU.
Mwisho upo na utakuja siku moja.
 Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia''.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.


Comments