VIZUIZI VYA KICHAWI

NA MCHUNGAJI ADRIANO MAKAZI, UFUFUO NA UZIMA


Wachawi ni Binadamu walioamua kuweka mkataba wa kumtumikia na shetani. Wachawi wanaweza kumzuia mtu kiuchumi, wanaweza kuzuia mafanikio ya mtu ni adui wa binadamu wenzao. Wasoma nyota, wapiga ramli, wasihiri, freemasonry na wengine wote hawa ni wachawi, ni mawakala wa shetani wanaofanya mapenzi ya shetani duniani. Maandiko yanasema adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Mtu wa karibu yako anaweza kukufanyia mambo mabaya sababu anakufahamu fika.
Wachawi hawa kuna wengine wanakwenda mpaka kuzimu kuonana na shetani ana kwa ana ili waweze kuiba nyota za watu na vibali vyao. Lakini Mungu ni Roho na ndiomaana aliamua kuuvaa mwili ili aje atuokoe kwa damu yake kama kafara(damu ya Yesu). Watumishi wa Mungu nao ni mawakala wa Mungu ambao wanafanya mapenzi ya Mungu kuziokoa roho za watu zilizoibiwa na kutekwa na hawa mawakala wa shetani. "Mungu ameiweka Ufufuo na Uzima kama chombo cha kurudisha vyote vilivyoibiwa na shetani na mawakala wake kwa mamlaka ya jina la Yesu Kristo."
1Wafalme 17:1 "Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu."
Yakobo 5:17 "Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake."
Eliya alikuwa ni Binadamu ambaye anayo mamlaka ya rohoni(ya Mungu) na aliweza kuzuia jambo lisifanyike kwa muda wa miaka mitatu. Hapa tunajifunza kuna binadamu mwenye mamlaka ya rohoni anayeweza kuzuia jambo lisitokee kwa muda fulani na ikawa. Vivyo hivyo kwenye upande wa giza Kuna watu wamezuiliwa wasifanikiwe kwa muda mrefu kwa nguvu za kichawi/kishetani lakini ipo Nguvu ya Mungu ambayo imeachiliwa ili kuondoa vizuizi walivyowafanyiwa watu wasiondoke kwenda kwenye mafanikio yao kwa jina la Yesu.
Eliya aliongea maneno ya kuizuia mvua na umande visitokee juu ya nchi kirahisi bila kuwa na historia ya kuwahi kufanya hivyo na ilitokea kwasababu alikuwa na mamlaka ya Mungu.
Wachawi nao wanaouwezo kwa nguvu za giza kuzuia ubaki palepale hata unapojaribu kuweka mguu unashindwa, unapojaribu kutoka kibiashara unashindwa kwasababu kuna mchawi yupo mahali fulani amesema fulani hatafanikiwa amekunenea maneno yenye nguvu za kishetani nyuma yake na unajikuta hufanikiwi kweli.
Yoshua 13:22 "Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua."
Wachawi ndio wanaowazuia watu wasifanikiwe kwenye maisha yao, Mungu ametoa sheria ya kuwa usimwache mwanamke mchawi kuishi. lakini kipindi kile huyu baalam mwana wa peori mchawi alikuwa mmoja wa wachawi waliouliwa kwa upanga. Sisi nyakati hizi tunao upanga wa roho ambao ni Neno la Bwana ndio tunaoutumia kuwaangamiza wachawi na kazi zao zote kwa damu ya Yesu.
Hesabu 22: 1 "Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa."
Ukiwa na wingi wa mafanikio watu wanafadhaika, ukifanikiwa sehemu fulani wapo wanaofadhaika na kuchukua hatua ya kukuharibia kwa siri. Wamoabu waliamua kuwaendea wazee wakatengeneza na hoja ili kuwazuia wana wa Israeli, waliamua kumwendea Baalam mchawi ambaye waliamini kila atakaye mlaani atalaaniwa na kila atakaye mbariki atabarikiwa kwa kinywa chake, hivyo wakawambia atamke maneno ambayo yana nguvu kwenye ulimwengu wa roho ili wana wa Israeli wasifanikiwe kwenye vita yao.
wachawi wanauwezo wa kuzuia kila mtu hata ambaye amezaliwa mara ya pili(ameokoka), kama umeokoka ukisinzia utashindwa kwenye vita na hawa wachawi watakushinda, unatakiwa uwe mpiganaji wakati wote muda wote ukiishi maisha matakatifu ili nguvu za Mungu na neema yake zikulinde na kukushindia vita yako. Ukiwa umezaliwa mara ya pili ukaishi maisha matakatifu na kupigana vita vya rohoni hakika utawashinda wote waliofanya vita dhidi yako na kufanikiwa kila uendako kwa jina la Yesu.
1 Wathesalonike 2:18 "Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia."
Paulo hapa anasema alizuiwa na shetani na huyu ndiye aliyesema tuzidi kuwa hodari katika Bwana lakini alikuwa anajua kushindana kwetu kunafaida ya kushinda pale tunapozuiwa. Paulo ametukumbusha kwenye.

2 Timotheo 4:7 "Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda"
Mtume Paulo lifanikiwa sana kwenye huduma yake sababu alikuwa anajua siri kuu ni kupigana vita vya rohoni. Kushindana kwetu ni siri kuu ambayo inatupeleka kwenye mafanikio kwa damu ya Yesu.
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
shetani anaweza kumzuia mtu asiende na bila kupigana huwezi kwenda mpaka pale utakapo amua kufungua njia kwa kushindana kwa jina la Yesu.

TAFSIRI YA NENO SHETANI
Neno shetani maana yake ni adui au mpinzani na kazi yake ni kuleta vizuizi kwa watu wa Mungu, analeta vizuizi vya kuolewa, vizuizi kwenye biashara, vizuizi pande zote ili kwamba mtu asiende kwenye kusudi alilopewa na Mungu kwenye maisha yake. Kila mtu hapa Duniani analokusudi la kufanya alilopewa na Mungu.
Yohana1:6 "Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.".
Unapoona wewe ni mgonjwa si bahati mbaya, unapoona huwezi kufanya jambo fulani si bahati mbaya bali yupo aliye kuzuia ambaye amejificha mahali fulani ambaye unaweza kumshnda kwa kupigana vita vya rohoni. Pale ulipo haupo kwa bahati mbaya kuna kusudi lililokufanya ukawa hivyo. Kila mtu unayemwona anakusudi na anayopitia yale ni kwasababu ya lile kusudi lililo ndani yake.
Yeremia1: 5 "Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa."
Kwenye maandiko utamwona hana amekaa muda mrefu kwenye ndoa hakushika mimba mpaka akatungiwa nyimbo za kudhihaki na Penina naye alikuwa mwenzake naye akawa anaongea maneno ya kumwuudhi baada ya kuona hashiki mimba. lakini ndani ya tumbo lake hana Mungu alikuwa anampango wa kumleta Samweli.
Ukiangalia na Musa naye alikuja kwa namna ya tofauti akazaliwa wakati wa amri ya kuuwawa kwa watoto wa kiume akafikia kuwaokoa wana wa Israeli.
kila mtu ni mtu watofauti, kila mtu ameitwa kwaajili ya kusudi fulani hapa duniani kuna wengine wamekuja duniani kuongea na wafalme,wengine wamekuja kuongea na wafanya biashara, wengine wamekuja kama Yehu wamepewa vinywa vyenye mamlaka hawaongei mara mbili wakitoa amri au ushauri, wanatekeleza amri ya Mungu, wakisema ufe unakufa au uishi unaishi.
Isaya alikuwa na wito na kizuizi chake kikuu kilikuwa ni mfalme huzia lakini Isaya alisimama mpaka mfalme huzia akafa. Alivyokufa mfalme huzia ndipo Isaya akaanza kumwona Bwana kwenye maisha yake na kuisikia sauti yake na kuiona hatima yake. inamaana hata wewe huzia wako anatakiwa aondoke maana yeye ndiye anayekuzuia usimiliki na kuifikia hatima yako.
2 Wathesalonike 2:6 "Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake"
Yupo anayezuia amekaa mahali fulani amejenga madhabahu yake ili kuzuia. tumeona Isaya amezuiliwa na mfalme huzia na baada ya kufa ndipo Isaya akaanza kufanikiwa.
shetani anazuia kwa kukaa ndani ya mtu au nje ya mtu.
Luka 22: 3 "Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano."

shetani alimwingia Yuda na akapewa fedha ili amsaliti Yesu. Yuda alimsaliti Yesu pale shetani alipomwingia. Unaweza kumwona mtu anakusumbua wakati mwingine si yeye ni shetani aliyemwingia ndiye anayefanya vita na wewe simama umshughulikie kwa jina la Yesu atakaa sawa na kukutii.
Sasa na Mtume Paulo amesema naye alitaka kwendalakini shetani alimzuia:- maana yake ni hii 'mfano unataka kuchukua Vissa kwenda nje ya nchi na yule anayetakiwa kukupa Vissa anakuangalia anakataa kukupa Vissa kwasababu unaonekana hutarudi' maana yake kuna pepo amemwingia mtu yule anayetoa vassa ili akuzuie usifanikiwe kama wengine na wewe kama hujui unafikiria ni hali ya kawaida sio bahati yako kumbe ni shetani amekuzuia kupitia mtoa vissa lakini kama una maarifa ya Mungu ukiamua kumshughulikia utapenya na atakupa vissa bila shida yeyote.
kuna watu wengine ni viti vya enzi yaani shetani anaingia ndani yake kufanya kazi na kutoka, maana yake yeye akili yake haiongozwi na yeye maana kila anachokifanya anaongozwa na shetani aliye ndani yake. Kuna watu wanakasirika bila ya sababu pale wanapokutana na wewe fahamu wanatenda vile shetani anavyowapelekesha hata wao hawajui. kuna watu wanaenda vile wasivyotaka wao kimawazo, kiakili, kitabia sababu wanamilikiwa na shetani.
"Baba Mungu katika jina la Yesu kristo imeandikwa "Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke" kwa mamlaka ya Jina la Yesu ninavunja kila kizuizi cha kichawi kilichowekwa kwenye maisha yangu kunizuia kwenye kazi, kwenye biashara, kwenye ndoa, kwenye elimu, kwenye promotion ninaviondoa kwa damu ya Yesu, kila silaha iliyofanyika na itakayofanyika juu yangu haitafanikiwa kwa jina la Yesu ninavivunja viti vya enzi vilivyonizunguka ili kushindana na mimi kwa jina la Yesu, ninawafyeka mawakala wa shetani wote ambao ni viti vya enzi kwa jina la Yesu, ninawaangamiza kwa jina la Yesu, kwa damu ya Yesu nikateketeza kila shetani aliyendani ya Mtu ili kunizuia kwa jina la Yesu. Amen
Fanya vita vya rohoni kama Mtume Paulo kwa jina la Yesu na hakika utapenya na kufanikiwa

Comments