YA KALE LAZIMA YAPITE ILI MAPYA YACHUKUE NAFASI.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
 Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
ROHO wa MUNGU aliniambia kuhusu ujumbe huu ambao leo nakuletea.
2 Kor 5:17 ''Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''

Mtu akiwa ndani ya KRISTO lazima awe kiumbe wa tofauti.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO lazima amtii KRISTO.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO huyo amefanyika mtoto wa MUNGU.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO katiba yake inakuwa Biblia.
Neno katiba maana yake ni sheria mama ya nchi lakini kwa Mkristo ambaye katiba yake ni Biblia, inatakiwa, Biblia ndio iwe muongozo wake wa maisha yake yote.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO ni mtu wa thamani sana.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO inabidi ya kale yapite na yasirudie tena.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO ya kale anatakiwa ayaache na sasa afuate mapya yanayofundishwa na Biblia.

Waefeso 5:3-5 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU.''

Kama uko ndani ya KRISTO hakikisha unayaacha ya kale yote.
Ya kale ni uongo, wizi na kuwa changudoa
Ya kale ni kwenda kwa waganga wa kienyeji na kuroga.
Ya kale ni kutambika na kutumainia mizimu.
Ya kale ni usengenyaji na uzinzi.
Ya kale ni kuabudu sanamu na kusujudia mawe au miti.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO lazima aachane na ya kale yote na sasa ayafuate mapya ambayo ni utakatifu, maombi na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.

Zaburi 34:13-14 '' Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.'' 

Ndugu hakikisha unaachana na ya kale yote.
Ya kale ni kwenda Disko na ulevi.
Ya kale ni kusikiliza nyimbo za kidunia.
Ya kale ni usaliti katika ndoa yako na kuzini wakati wa uchumba.

Waefeso 3:9-10 '' Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.'' 

Ya kale ni tamaa mbaya na udokozi.
Ya kale ni lazima yapite ili yaje mapya ambayo ni Ucha MUNGU na hekima ya ki-MUNGU maana ndio matokeo ya mtu aliyeamua kuwa ndani ya KRISTO.
Kama hujayaacha mambo ya kale hakikisha unayaacha leo maana ukiendelea na ya kale utaikosa mbingu.
Acha ya kale maana hayana faida kwako hata moja.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya, ya kale yanapita na tazama yanakuwa mapya.

 ''tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za BWANA tu, ila na mbele ya wanadamu.-2Kor8:21'' 

Kama hujawahi kuwa kiumbe kipya hakikisha leo unakuwa kiumbe kipya.
Viumbe wapya hawasemi uongo wala sio waasherati.
Viumbe wapya ni watiifu na wanyenyekevu kwa KRISTO.
Viumbe wapya huishi maisha matakatifu.
Viumbe wapya hawavai mavazi ya kikahaba.
Viumbe wapya hawavai mitepesho.
Viumbe wapya hawavuti sigara wala bangi.
Viumbe wapya hawatumii madawa ya kulevya.
Kama umeamua kuwa kiumbe kipya hakikisha unayaacha ya kale yote, ya kale lazima yapite ili mapya yachukue nafasi.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO lazima awe kiumbe kipya.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO lazima abadili mfumo wake wa maisha kutoka maisha ya dhambi na kuanza kuishi maisha matakatifu.

 ''mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli.-Waefeso 4:22-24''

Ni muhimu sana kuacha ya kale na kuanza kuishi katika mapya ambayo ni kutii Neno la MUNGU.
MUNGU anapomuokoa mtu humpa mfumo mzima wa kuishi ambao ni maelekezo ya Biblia.
Mtu akiokoka anatakiwa kuwa kiumbe kipya na ni lazima ya kale yapite  ili mapya yachukue nafasi.
Ya kale ni kuuza pombe.
Ya kale kumiliki bar au kuwa mhudumu wa bar.
Kama umeamua kuufuata uzima wa milele ni lazima uachane na biashara yako hiyo ya dhambi.
Uzima wa milele unawangojea walio ndani ya KRISTO na wameacha ya kale yote na sasa wanayaishi mapya.
Kutoa mimba ni ya kale.
Kuchanjwa chale ni ya kale.
usoma nyota ni ya kale.
Kuwa na nyota yako hayo ni ya kale .
Viumbe vipya hawavai nguo za kuacha matiti nje.
Kama hujaacha ya kale nakusihi uyaache leo.
Jitenge na ya kale yote.
Acha  dhambi, ogopa dhambi, ikimbie dhambi na usifanye dhambi tena maana dhambi ni ya kale ambayo sharti yaondoke kwa watu wa MUNGU.
Ndugu, ishinde dhambi  leo kwa kuamua kuishi maisha matakatifu kama neno la MUNGU linavyokutaka.
Mpende MUNGU na achana na ya shetani yote.

Yakobo 4:7 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments