DHAMBI INAKUTAMANI WEWE, WALAKINI YAKUPASA UISHINDE.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu, tena karibu sana tujifunze Neno hai la MUNGU aliye hai.

Mwanzo 4:7 '' Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. ''

Usipotenda vyema yaani usipotenda kwa utakatifu dhambi inakuotea.
Usipotenda kwa kufuata Neno la MUNGU iko dhambi inakuotea.
Usipolitii Neno la MUNGU katika matendo yako, iko dhambi inakuotea.
Kwenye andiko hapo juu tunamuona mtoto wa mzee Adamu aitwae Kaini, dhambi ikimtamani na kumshinda.
Hata leo dhambi haijakoma kukutamani wewe, walakini yakupasa uishinde.
Kijana, hiyo tamaa ya ngono inayokusumbua ni dhambi inayokutamani ili ufe mapema kwa ukimwi. Ni dhambi inayokutamani ili kukutenga wewe na uzima wa milele. Ni dhambi inayokutamani wewe ili kukuletea laana katika maisha yako, Walakini Neno la MUNGU linasema kwamba yakupasa uishinde maana ikikushinda ni hatari.

Binti, hiyo tamaa ya ngono inayokutesa ni pando la shetani, ni dhambi inayokutamani, walakini yakupasa uishinde maana usipoishinda ni hatari kwako.
Dhambi inakutamani ili kama ukiitii basi jina lako litaondolewa kwenye kitabu cha uzima.
Dhambi inakutamani ili tu ukiitii ujue ulinzi wa MUNGU juu ya baraka zako unaondoka mara moja, ndio maana hiyo dhambi inatokutamani yakupasa uishinde maana usipoishinda ni hatari kwako.
Vijana wenzako wanapokushauri utende uovu, hiyo ni dhambi inakutamani, walakini yakupasa uishinde.
Wamama wenzako wanapokushauri kwenda kwa mganga, hiyo ni dhambi inakutamani na yakupasa sana uishinde maana usipoishinda ni hatari kwako.
Wababa wenzako wanapokuchukua kwenda bar, hiyo ni dhambi inakutamani, walakini yakupasa uishinde maana usipoishinda ni hatari kwako.
 
Mambo mengi ya kidunia yaliyo chukizo kwa MUNGU ndiyo hayo yanayoongoza kuwatamanisha wanadamu ili wayafanye, hiyo ni dhambi inawatamani na yawapasa waishinde maana wasipoishinda ni hatari kwao.
Marafiki zako wanaweza kuwa sehemu ya dhambi kukutamani wewe ili utende dhambi.
Ndio maana Biblia inasema;
'' Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. -Zaburi 1:1''

Kwenye shauri la watu wasio haki huko kuna dhambi inayokutamani wewe, walakini yakupasa uishinde maana ikikushinda hiyo dhambi ni hatari kwako.
Ukijiunga na njia ya wakosaji yaani wasiomhitaji YESU ili awaokoe, hiyo ni dhambi inakautamani, walakini yakupasa uishinde maana ikikushinda ni hatari kwako.
Marafiki zako wanaweza kuwa baraza la wenye mizaha kama ushauri wao kwako ni wa kukutaka tu ufanye dhambi, hiyo ni dhambi inakuotea, walakini yakupasa uishinde.
Jitenge na marafiki wabaya maana hiyo ni dhambi inakutamani, walakini yakupasa uishinde.
Ishinde dhambi kwa kuamua vyema.
Ishinde dhambi kwa kuokoka na kuishi maisha matakatifu.
Ishinde dhambi kwa kujiunga na kanisa.
Ishinde dhambi kwa kwenda ibadani.
Ishinde dhambi kwa kujiunga na kundi la maombi.
Ishinde dhambi kwa kuliishi Neno la MUNGU na kulitafakari kila mara.
Ishinde dhambi kwa kuondoka katika eneo ambalo litakushawishi kutenda dhambi.
Ishinde dhambi kwa kutohudhuria disko, bar, kwenye kumbi za starehe na kwenye matamasha ya nyimbo za kidunia.
Ishinde dhambi kwa kuamua kuishi maisha matakatifu ndani ya KRISTO YESU Mfalme wa uzima.
Ishinde dhambi kwa kuondoka eneo ambalo mko wawili tu wa jinsia tofauti.
Ishinde dhambi kwa kuikataa dhambi na vishawishi vyake vyote.

Ayubu 2:9 '' Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru MUNGU, ukafe. ''

Ayubu dhambi ilimtamani kupitia mke wake ili amkufuru MUNGU, lakini Ayubu aliishinda dhambi hiyo iliyokuwa inamtamani.
Hata wewe ndugu, nakusihi sana ishinde hiyo dhambi leo inayokutesa na kukukosesha amani.
Ishinde dhambi kwa kukataa ushawishi wa watu wasio na nia njema na wewe.
Ishinde dhambi kwa Kufuta picha zote za ngono na video zote za ngono kwenye simu yako.
Ishinde dhambi kwa Kuacha punyeto.
Ishinde dhambi kwa Kacha kujichua.
Ishinde dhambi kwa Kuacha kuwachungulia wanandoa waliolala usiku kwenye nyumba zao.
Kuatamani kufanya uovu hiyo ni dhambi inakutamani, walakini yakupasa uishinde.


Dhambi ya uasherati ilikuwa inamtamani sana Yusufu kupitia mke wa bosi wake, lakini Yusufu aliishinda.

Mwanzo 39:7-12 ''Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu.Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose MUNGU?
Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. ''
 
Ndugu, dhambi inakutamani, walakini yakupasa uishinde.
Dhambi ya uongo ilimtamani Anania na mkewe Safira, walakini walitakiwa waishinde lakini ilipowashinda dhambi hiyo walikuwa, hiyo iko Matendo 5:1-11.

Ndugu Dhambi inayokutamani ina madhara makubwa sana kwako, walakini yakupasa uishinde.

Dhambi ya tamaa ya pesa na usaliti ilimtamani Yuda Iskarioti hadi ikapelekea kujinyonga, Hiyo Iko Mathayo 27: 3-5.
Ndugu Dhambi inayokutamani ina madhara makubwa sana kwako, walakini yakupasa uishinde.

Eva, Dhambi ilimtamani kupitia Tunda la mti, ilipomshinda dhambi hiyo ikapelekea kifo kwa Eva NA uzao wake wote, uzao wa Eva ni wanadamu wote.
Mwanzo 3:6 ''Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.''

Eva ushawishi wa dhambi ulimzidi hata akasau akigo la MUNGU waliloambiwa;
 ''BWANA MUNGU akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. -Mwanzo 2:16-17''

Ndugu Dhambi inayokutamani ina madhara makubwa sana kwako, walakini yakupasa uishinde.
Dhambi huwa ina tabia ya kuwatamni wanadamu siku zote, walakini MUNGU siku zote anatutaka tuishinde dhambi.

Kwa msaada zaidi naomba nikuambia njia saba za kuishinda dhambi na siku moja nitazifafanua hizo njia saba za kuishinda dhambi.

NJIA SABA ZA KUZISHINDA DHAMBI..

1. Kumtii MUNGU kupitia Neno lake Biblia.
2. Kuishi maisha mataktifu.
3. Kuokoka.
4. Kujitenga na dhambi.
5. Kuutumia muda wako wote vizuri na kwa malengo mema.
6. Kufunga na kuomba.
7. Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments