MADHARA YA DHAMBI YA MTU KWENYE MAISHA YAKE.

Na Peter M Mabula, Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe mpendwa wangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo nazungumzia madhara ya dhambi katika maisha ya mtu, lakini mwanzo kabisa naomba kila mtu ajue kwamba madhara mabaya zaidi ya dhambi ni ziwa la moto, ndio maana MUNGU kila Leo anawaonya wanadamu ili waache dhambi, MUNGU anasema:
 '' Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.-Ezekieli 18:4 ''

Madhara mengine ya dhambi ni  kifo cha mapema.
1kor 10:1-10 ''Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni KRISTO.  Lakini wengi sana katika wao, MUNGU hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.
Wala tusimjaribu BWANA, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.''


-Wanaozungumzwa katika maandiko hapo juu ni wana wa Israeli ambao MUNGU aliwatoa katika nchi ya Utumwa Misri ili kuwapeleka Kaanani nchi ya ahadi.
MUNGU alipanga watu hawa wote wafike Kaanani lakini dhambi zao ziliwafanya waisraeli hao wafike Kaanani watu wawili tu kati ya wale watu zaidi ya Milioni mbili. Waliofika Kaanani ni Yoshua na Kalebu tu maana hao walimtii MUNGU na kumwamini hadi Mwisho, wengine waliofika pamoja na akina Yoshua ni Waisraeli watoto ambao walizaliwa jangwani katika kipindi cha safari ya kutoka Misri kwenda Kaanani.
Dhambi za watu hawa zilifupisha maisha yao.
Madhara mojawapo ya dhambi ni kifo cha mapema kama ilivyotokea kwa waisraeli wakati wakitoka Misri.
Biblia hapo juu inasema walitamani mabaya ndio maana wakafa kifo cha mapema.
Waliabudu sanamu ndio maana wakafa kifo cha mapema.
Walifanya uasherati na kupelekea kifo cha mapema. Hii ilitokea kwao kwa sababu ya uovu wa uasherati na siku hiyo moja walikufa watu ishirini na tatu elfu  kwa kifo cha mapema ambacho chanzo chake ni dhambi.
Wengine walitenda dhambi ya kumjaribu MUNGU wakaumwa na nyoka na kufa wengi sana kwa kifo cha mapema.
Wengine walifanya dhambi ya kumnung'unikia MUNGU wakafa kifo cha mapema.
Leo tuko katika kipindi cha Neema lakini hiyo haiondoi moja kwa moja kwamba dhambi haiwezi kuleta kifo cha mapema kwa mtu.
Kuna watu leo hufa kifo cha mapema kwa sababu ya dhambi ya uzinzi kisha ukimwi.
Kuna watu leo hufa kifo cha mapema kwa sababu ya  kufumaniwa na wake za watu kisha kuuawa.
Kuna watu leo hufa kifo cha mapema kwa sababu ya kuiba kisha kukamatwa kisha  kuchomwa moto N.k
Kifo cha mapema kipo kwa sababu ya dhambi.
Dhambi ni mbaya sana na inatakiwa kukimbiwa na kila mtu. Ndugu ikimbie dhambi na achana na dhambi zote.

 
Madhara mengine ya dhambi ni  kwamba Dhambi huwatenda wanadamu na MUNGU wao.


Isaya 59:1- 4 ''Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;  lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya. Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.'' 


-Dhambi huwatenga wanadamu na MUNGU wao.
-Kuna MUNGU hawezi kukuokoa kwa sababu tu ya dhambi zako.
-MUNGU anaweza asisikilize hitaji lako kwa sababu tu ya dhambi zako.
-Dhambi zako zinaweza kuuficha uso wa MUNGU hata asikusikilize wala kukujibu.
Ndugu ni muhimu sana kuacha dhambi.
Acha uzinzi, acha uongo, acha kutoa mimba, acha kuua, acha wizi, acha kuabudu shetani, acha kuroga na acha kila uovu unaokuhusu maana dhambi ni mbaya na ina madhara makubwa sana.



Ukipanda dhambi utavuna uharibifu.
Dhambi ni mbaya sana lakini MUNGU kupitia YESU KRISTO hutuita ili tuwe watakatifu na hatutakiwi kurudi tena dhambini.
Waefeso 1:3-5 ''Atukuzwe MUNGU, BABA wa Bwana wetu YESU KRISTO, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake KRISTO; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.''
 
Jambo jingine naomba ujue kwamba Kutubu kwa Hezekia kuliondoa kifo cha mapema.

Hata kwako kifo cha mapema kinaweza kikaondolewa kama ukitubu na kuacha dhambi.
2 Wafalme 20:1-6 '' Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA akasema, Nakusihi, BWANA, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la BWANA likamjia, kusema,  Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, BWANA, MUNGU wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa BWANA. Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.''



Ndugu yangu, Kuficha dhambi zako ni kuyaficha pia mafanikio yako ya kiroho na kimwili
Mithali 28:13 '' Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.''
 
Kung'ang'ania dhambi ni kujipeleka kwenye ziwa la moto huku ukiliona kabisa likikusogelea.
Kushabikia dhambi ni kumpa zawadi shetani.
Kushabikia dhambi ni kumtia moyo shetani ili aongeze zaidi kuleta uovu.
dhambi ni mbaya na inatakiwa ikemewe na kila mtu na kila mtumishi.

 Popote unapokuwa, iwe Guest House, Chumbani, kwenye vichochoro, hata iwe usiku wa giza  nene, chochote unachofanya, Kamera ya Mbinguni inakumulika na kuchukuwa Picha, jicho la BWANA liko kila mahali likichunguza kila tendo.
Mithali 15:3 ''Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.'' 

 Mtu ukiwa na pesa unaweza kupata chochote cha hapa Duniani, lakini huwezi kupata vitu vya rohoni kwa njia ya pesa, vitu vya rohoni unaweza kuvipata kwa njia ya maombi pekee yake
'' Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa BWANA; Hakika, hatakosa adhabu. - Mithali 16:5''

 Dhambi ni mbaya, ndugu usiwe kama kupe ambaye muda mwingi yuko katika ng'ombe, siku akianguka ukimuuliza nani kukuleta, atasema nimeletwa na ng'ombe. na ndivyo ilivyo kwa watu wengi wanatembea na mapepo ambayo yanawaongoza, na ukimuliza nani kakuleta bar/gesti atasema shetani. Lakini naomba tujue kwamba mwanzo wa mapepo kuingia ndani ya mtu ni kwa sababu ya dhambi au kuwa mbali na MUNGU.

 dhambi ina madhara makubwa.
Dhambi ndizo zilizosababisha waisrael wasafiri miaka 40 kutoka misri kwenda kaanani badala ya wiki 1.
=Hiyo inatufundisha sisi kwamba dhambi inaweza ikachelewesha Baraka yako.

Hata viongozi wakuu ni muhimu kuwa makini sana. Musa alifanya makosa  yaliyofanya akose kuingia kanaani. yanatufundisha nini??
Kule Meriba Musa aliambiwa auambie mwamba utoe maji yeye akaupiga mwamba Mara 2 huku akijipa heshima yeye Kwa kusema "je tuwatokezee maji katika mwamba huu?"
Ni kosa maana hakuambiwa hivyo soma Hesabu 20:7-12 ili uone kosa la Musa. Ila alitubu kama ukisoma kumbukumbu La torati.  Musa alichukuliwa baada ya kufa maana alitubu na wakati Wa kufa kwake alikuwa mtakatifu.
Tukio La Musa linatufundisha kwamba tusiongeze katika tulichopewa na MUNGU, pia dhambi ina madhara makubwa.
Ukipewa kutoa ujumbe wa MUNGU usiupindishe Kwa malengo yako, maana huko ni kuchuma dhambi.

 Dhambi ni mbaya na ina madhara makubwa.
Kugawanyika Wa Israel na kuwa mataifa 2 kulitokana na dhambi ya Suleiman, Hayo ni madhara ya dhambi.
Hivyo ndio mwanzo Wa taifa la  yuda.
Lakini baada ya miaka mingi Israel wakarudi kuwa taifa moja Tena.

Nini tunajifunza kuhusu madhara ya dhambi?
=Dhambi zako zinaweza zikukuathiri na kukuvuruga katika maisha yako.
=Makosa ya viongozi wakuu yanaweza kuliathiri kanisa hata taifa.

Mithali 14:34 '' Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.''
 Ndugu jioke na kizazi hiki chenye ukaidi.
BWANA YESU anakungoja sasa ili uamue vyema leo.


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula, Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments