MAMBO SABA YANAYOMTHIBITISHA MTU KWAMBA ANAMPENDA MUNGU.

Na Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
"Nawapenda wale wanipendao "
Sio neno langu hilo Ila nimenukuu MUNGU akisema kupitiaa Neno lake Biblia.
Mithali 8:17 '' Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.''

Kumbe kuna watu wanaompenda MUNGU na wengine hawampendi MUNGU, ila wanaompenda MUNGU na MUNGU anawapenda sana, na amesema hao wakimtafuta hakika watamuona.
Kwa sababu sio wanadamu wote wanaompenda MUNGU, je wewe ndugu uko upande gani?
Je unampenda MUNGU hata ukimtafuta kwa maombi umuone?
Je unampenda MUNGU katika kiwango akitakacho hata uwe na kibali cha kumtafuta na kumuona kupitia maombi yako?

Je Kumpenda MUNGU ni kufanyaje?
Je kumpenda MUNGU ni kutamka tu kwa mdomo kwamba unampenda?
Kuna watu hawampendi MUNGU kabisa japokuwa kwa vinywa vyao watakuambia kwamba wanampenda MUNGU.
MUNGU anasema juu yao kwamba '' Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.-Mathayo 15:8''

  Je, unampenda MUNGU hata na wewe uwe na sifa ya kupendwa na yeye?
Ni ka tafakari kagumu kidogo lakini napenda ujue kwamba.
Kumpenda MUNGU ni jambo muhimu sana kwa kila mtu.
Kuna mambo mengi yanayoweza kumthibitisha mtu kwamba huyo anampenda MUNGU.
Hapa nimekuandalia mambo 7 yanayomthibitisha mtu kwamba huyo anampenda MUNGU.

MAMBO SABA YANAYOMTHIBITISHA MTU KWAMBA ANAMPENDA MUNGU WA MBINGUNI.

1. Kutii Neno la MUNGU na sauti ya MUNGU.
Neno la MUNGU ni Neno maalumu sana na la kipekee.
Biblia inasema hivi '' Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.-Zaburi 12:6'' -Anayempenda MUNGU ni lazima awe ni mtii kwa Neno la MUNGU.
  Isaya 1:19-20 ''Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya''

-Anayempenda MUNGU ni lazima awe anaitii sauti ya MUNGU.
Sauti ya MUNGU ni Neno la MUNGU.

 

2.   Ni kumtumikia KRISTO katika kweli.
Zaburi 2:11-12 ''Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia''
-Kumtumikia MUNGU ni mpango wake kabisa na sio matakwa yetu sisi wanadamu.
Kila mteule wa KRISTO humtumikia KRISTO.
Maisha ya Wokovu ni maisha ya utumishi.
Kuna ambao BWANA amewapa kazi maalumu katika utumishi.
Kuna ambao wamepewa vitengo vyao katika utumishi.
Kuna ambao wamepewa huduma na kwa kupitia huduma hizo wanamtumikia BWANA.
Kuna ambao kumwabudu tu BWANA YESU huo ni utumishi mkuu zaidi.
1 Samweli 12:14-15 '' Kama mkimcha BWANA, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya BWANA, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata BWANA, MUNGU wenu, vema! Bali msipoisikia sauti ya BWANA, mkiiasi amri ya BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.'' 

-Mtu anayempenda MUNGU ni lazima amtumikie.
Kumtumikia MUNGU ni kumwabudu katika roho na kweli.


3.   Ni kuacha dhambi.
Mithali 28:13 ''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.'' 

-Dhambi ni uasi kwa MUNGU.
-Dhambi huwatenga wanadamu na MUNGU wao.
-Dhambi ni machukizo yote kwa MUNGU.
-Mtu ambaye anampenda MUNGU ni lazima akubali kuacha dhambi.
-Mtu ambaye anampenda MUNGU Ni lazima aachane na dhambi zote.
-Mtu ambaye anampenda MUNGU Ni lazima aitubie dhambi na kujitenga na dhambi zote.
Warumi 6:23 ''3 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU  Bwana wetu.''

4.  Ni kuenenda kwa ROHO.
Wagalatia 5:16 '' Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.'' 

ROHO MTAKATIFU ndio msimamizi wa kanisa la KRISTO.
ROHO MTAKATIFU ndiye ambaye humshuhudia KRISTO katika mioyo yetu.
ROHO MTAKATIFU kama tukimtii hakika huko ndiko kumpenda MUNGU.
Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU ndiko kumpendeza MUNGU, na kumpendeza MUNGU ndiko kumpenda MUNGU.
Wanaompenda MUNGU ni lazima waenende kwa ROHO MTAKATIFU.
ni lazima wamtii ROHO MTAKATIFU.
NI lazima wakubali kushauriwa na ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU anajua yote; yaliyopo, yaliyopita na yajayo yote hivyo tukimtii ROHO MTAKATIFU tunakuwa tunampendeza MUNGU muumba wetu.
MUNGU BABA anasema ''Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.-Mithali 1:23 ''

5.  Ni kuokoka Na kuishi maisha ya wokovu.

Yohana 3:17-18 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.'' 

 Kuokoka ndio mwanzo wa kumpenda MUNGU.
Maisha ya wokovu ndio kuokoka.
Kuokoka ni kuutii mpango wa MUNGU wa wokovu kwa wanadamu.
Kuokoka ndio kuishi maisha ya ushindi .
Kuokoka ndio kumpenda MUNGU na mpango wake wa uzima kwa wanadamu.

Waefeso 2:8 '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;''

6. Ni kumkimbia shetani na kazi zake zote.
1 Yohana 3:8 '' atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi''

Kumkimbia shetani ni kuacha dhambi.
Kumkimbia shetani ni kuanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kumkimbia shetani ndio kuamua kuokoka.
Kumkimbia shetani ni kumkimbilia BWANA YESU.
Mwanadamu anayempenda MUNGU ni yule aliyemkimbia shetani na mambo yake yote.
Ili umpendeze MUNGU ni lazima ujitenga na dhambi na kila jambo la kishetani.
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
 
7. Ni kumtii YESU KRISTO.
Warumi 8:10 '' Na KRISTO akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.'' 

Kumtii KRISTO ni kuutii mpango wa MUNGU wa uzima wa milele.
Kumtii KRISTO ni kumtii MUNGU .
Kumtii KRISTO ndiko kumpendeza MUNGU.
Ili MUNGU ajue unampenda unatakiwa kwanza umtii YESU KRISTO maana kwa huyo ndimo ukamilifu wa MUNGU unakaa kwa jinsi ya mwili.

Wakolosai 3:24 ''mkijua ya kuwa mtapokea kwa BWANA ujira wa urithi. Mnamtumikia BWANA KRISTO.''

Kwa ufupi sana hivyo ni baadhi tu ya vigezo vinavyoweza kukuonyesha wewe kama kweli unampenda YAHWEH MUNGU wa uzima.
Lakini mwisho kabisa naomba utambue kwamba Kumpenda MUNGU haiko katika kutamka kinywani tu Bali maana halisi ya kumpenda MUNGU iko katika matendo yako.
Je, unampenda MUNGU?

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula,
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU. 
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments