MUNGU ANATAKA UFANIKIWE.

Na Mwl. Christopher Mwakasege.
Bwana Yesu asifiwe!
Nataka ujue ya kuwa Mungu anataka ufanikiwe, na anataka ashiriki katika kufanikiwa kwako huko; Lakini kwa kutumia mpango wake, alionao kwa ajili yako! Ndiyo maana anasema: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini, siku zenu za mwisho” (Yeremia 29:11).
Mstari huu kwa tafsiri ya kiingereza ya “New International Version” (NIV) unasomeka hivi: “For I know the plans I have for you, declares the Lord, plans to prosper you and not to harm you, plans to give you hope and a future”.
Kwa kusoma tafsiri hizi mbili – tunapata kufahamu ya kuwa neno hili “mawazo” lilivyotumika katika mstari huu, lina maana ya “plans” au “mipango”. Na neno hili “amani” lilivyotumika katika mstari huu lina maana ya “to prosper you” au “kukufanikisha”.
Tena, nataka uone ya kuwa hakusema anajua “wazo”, bali alisema anayajua “mawazo”. Hii ikiwa na maana ya kwamba mipango aliyonayo kwa ajili ya kukufanikisha:


1. Inahusisha wazo lake zaidi ya moja. Kwa hiyo mipango yake juu yako ni mkusanyiko wa mawazo aliyonayo juu yako, ili akupe, na yakusaidie kupangilia maisha yako, na kukuwezesha kufanikiwa;
2. Inahusisha “njia” za Ki – Mungu za wewe kuzitumia ili uweze kufanikiwa. Na kufuatana na Isaya 55:8,9, njia hizi zipo katika mawazo yake aliyoyaandaa yawe mipango yake kwa ajili yako.
3. Inahusisha “neno” lake lililomo katika biblia, ambalo linapohuishwa na Roho Mtakatifu, yaani “pumzi” yake – linahuishwa na kugeuka kuwa maelekezo binafsi kwa ajili yako! Hii ni kufuatana na maneno yaliyopo katika Isaya 55:10,11.
Kuanzia mfululizo ujao, nitakuwa nakushirikisha aina mbalimbali za mawazo ya Mungu aliyokusudia kuyaweka moyoni mwako, ili yaweze kukujulisha na kukuongoza katika mipango yake itakayofanikisha maisha yako.
Mungu aendelee kukutunza! Mshirikishe na mwingine kuwepo kwa mfululizo juu ya somo hili muhimu! Ikiwa ni muhimu kwa serikali na makampuni kuwa na mipango ili ifanikiwe, si zaidi sana kwa mtu binafsi naye anatakiwa awe na mipango ya kumsaidia ili afanikiwe?
Na kama Mungu tuliyenaye, na tunayemwabudu katika Kristo Yesu anasema anaijua mipango hiyo, ina maana pia anajua namna ya kutushirikisha ili tuijue mipango hiyo na tuitekeleze! 


 Nataka liingie hili ndani ya moyo wako ya kuwa Mungu anapenda ufanikiwe, na anapenda na Yeye ashiriki katika kufanikiwa kwako huko; lakini kutumia mpango wake, alionao kwa ajili yako!
Mtazamo huu na msimamo huu wa Mungu, tunauona tunaposoma mstari wa Yeremia 29:11 usemao: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Zipo aina nyingi za mawazo ya Mungu, zinazounda mipango aliyonayo kwa ajili yako, ili uweze kufanikiwa. Tuangalie aina ya 1 ya wazo mojawapo la Mungu, alilolikusudia kuliweka moyoni mwako, ili liweze kukujulisha na kukuongoza katika mpango wake, utakaofanikisha maisha yako.
Wazo hilo ni hili: “Ombea kwa Bwana mji unaohusika na maisha yako!”
Wazo hili linatokana na agizo la Mungu kwa wana wa Israeli alipowaambia ya kwamba: “Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani” (Yeremia 29:7).
Neno hili “amani” lililoandikwa mara tatu katika mstari huu wa Yeremia 29:7 lina maana ile ile ya neno “amani”, lililotumika katika mstari ule wa Yeremia 29:11. Neno hili “amani” lilivyotumika katika mistari hii miwili lina maana ya “mafanikio”
Ndani ya agizo lililomo katika mstari huu wa Yeremia 29:7 nataka ujifunze na kutilia maanani yafuatayo:
1. Kwamba; Kufanikiwa kwako katika kitu unachokifanya, kumeunganishwa na kufanikiwa kwa mji unaokaa au unaoishi. Mji ukifanikiwa kimaendeleo na wewe unatakiwa ufanikiwe vile vile! Mji ukifanikiwa kimaendeleo, wakati wewe mkaazi wake umekwama kimaendeleo, ina maana umeshindwa kupata mbinu za kujiunganisha katika mafanikio ya mji huo! “Kwa maana katika amani (mafanikio) yake mji huo ninyi mtapata amani (mafanikio)”! Haya ndiyo ambayo Mungu aliwaambia wana wa Israeli – na anakuambia na wewe pia leo!
2. Kwamba; Ili mji unaokaa ufanikiwe kimaendeleo, unahitaji pia maombi yako. Biblia inasema: “Kautakieni amani (mafanikio) mji …mkauombee kwa Bwana” (Yeremia 29:7). Kuuombea mji kunamwonyesha Mungu haja uliyonayo moyoni mwako, ya kutaka msaada wake, ili aweze kukupa mbinu zitakazokuunganisha na mafanikio ya mji huo, ili na wewe ufanikiwe!
3. Kwamba; Maombi unayoombea mji, yanatoa nafasi kwa Mungu “kufuatilia” aina ya maendeleo yanayoufanya mji ufanikiwe! Hii ni kwa sababu si kila mafanikio unayoyaona katika mji yanakufaa na wewe pia! Biblia inasema: “Kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza” (Mithali 1:32)! Na Mungu asingetaka ujiunganishe na mbinu zilizopo katika mji zinazowaangamiza wanaozitumia kufanikiwa! Mbinu za mafanikio kama hizo, ndizo zinazofanya “mji” ukifanikiwa – unajikuta hautaki kumsikiliza Mungu…na wakaazi wake wanakuwa hawataki pia kumsikiliza Mungu! Mungu anasema: “Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema sitaki kusikia …” (Yeremia 22:21). Mafanikio yanayokufanya usimsikilize Mungu hayakufai.
4. Kwamba; Ukilitazama kwa mtazamo huu suala la kuombea mji ili ufanikiwe, utajikuta unaombea mji zaidi ya mmoja! Wana wa Israeli walipopewa agizo la kuombea mji wa Babeli walikuwa mbali na kwao. Na walipokuwa huko uhamishoni walijikuta wanauombea pia mji wa Yerusalemu ambako ndio kwao! Kwa hiyo ukiombea “Babeli” yako, usisahau kuombea na “Yerusalemu” yako, maana maombi ya miji inayotumika kukupa kipato chako, yanaunganisha mafanikio ya miji hiyo na kule kufanikiwa kwako!
5. Kwamba: Hata kama mji huupendi, wewe uombee, ili kuonyesha utii wako kwa Mungu, ili akufanikishe katika kipindi ulichomo katika mji huo! Nina uhakika wana wa Israeli hawakuupenda mji wa Babeli, lakini bado walitakiwa wauombee katika kipindi walichokuwa huko!
Mbarikiwe!!

Comments

Petrus Ntevi said…
samahan nimekosea tuma comments..nilikusudia ituma kwenye post yenye NILIMLISHA MUME WA MTU LIMBWATA NA si katika somo la mwl mwakasege