NINI KINAONGOZA MAISHA YAKO?

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Je nini kinaongoza maisha yako?
Ongoza maana yake ni kitu au mtu kuwa mbele yako ili kukuongoza njia au kukuongoza jambo la kufanya.
 Inawezekana kabisa kitu hicho hakikuongozi tu bali unaongozana nacho kabisa, yaani unafuatana nacho kikiwa ndio msaada wako.

Mathayo 15:14 ''Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.''

Kipofu akiomuongoza kipofu mwenzake hakika wote wawili watatumbukia shimoni.
Kipofu anaweza kuwa mtu, lakini pia kipofu ni kitu chochote kinachomuongoza mtu ambacho kitu hicho sio sahihi.
Dhambi ikikuongoza, huyo ni kipofu aitwaye dhambi na kama ukikubali akuongoze siku zote za maisha yako hakika mtajikuta wote mko ziwa la moto.
Pesa ni kipofu mwingine ambaye akikuongoza anavyotaka yeye unaweza kujikuta huhusiki na mbingu bali jehanamu.
Wanaoongozwa na pesa ni kwao ni sahihi hata kuua ili aongeze pesa.
Mambo ambayo ni Vipofu ni mengi sana na hao vipofu hawatakiwi kuwaongoza watu.
Mpendwa, nakusihi hakikisha huongozwi na kipofu.

 Nini huongoza maisha yako?
-Meli huongozwa na usukani, kama uko ndani ya meli utafuata usukani ulikoelekezwa hata kama hutaki kwenda huko.
-Kuna watu huongozwa na watu wengine, kama hao waongozaji ni vipofu hakika hata waongozwaji watapotea.
-Kuna watu huongozwa na hatia hata hawajiamini tena kama wamesamehewa baada ya kutubu na kumpokea BWANA YESU..
-Kuna watu huongozwa na dhamiri na sio Neno la MUNGU, ni hatari.



Matendo 8:30-31 ''Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.'

Nitawezeaje kuelewa, mtu asiponiongoza?
Hili ni swali ambalo ndugu mmoja mwafrika wa Ethiopia alimuuliza Mtumishi wa MUNGU Filipo.
Ilibidi Filipo amuongoze kulijua Neno la MUNGU hatimaye akabatizwa na kuokoka.
Mtu kama filipo anahitajika katika jamii leo ili awahubirie watu Neno la MUNGU ili waijue kweli ya MUNGU. Maana kuna watu hawajui lolote hadi aje Filipo kuwasaidia kujua mpango wa MUNGU juu ya maisha yao.
Filipo aliongozwa na ROHO wa MUNGU ndio maana ikawa rahisi kwake kulifikisha kusudi la MUNGU kwa Mwethiopia yule.

Wewe ni nini huongoza maisha yako?
-Kuna watu huongozwa na hasira tu.
-Kuna watu huongozwa na uoga wa kipepo.
-Kuna watu huongozwa na mali zao.


Zaburi 139:23 ''Ee MUNGU, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;''

Je, leo MUNGU akichunguza moyo wako atakuta unaongozwa na nini?
Inawezekana kabisa kinywa chako kila mara kinamtaja MUNGU kwamba ndio anayeongoza maisha yako, lakini matendo yako hayaonyeshi kwamba unaongozwa na MUNGU.
Inawezekana kabisa wewe huonyesha kila jumapili unaongozwa na MUNGU,  Maana unahudhuria kanisani, lakini siku zingine za juma unaongozwa na nini?
  Wewe nini kinaongoza maisha yako?
-Kuna watu huongozwa na Biblia ambalo ni Neno la MUNGU(Hawa wanaitwa heri)
Zaburi 119:105-106 '' Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.''
-Kuna watu huongozwa na ROHO wa MUNGU(Hawa ni washindi daima)

Warumi 8:14-17 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, BABA. ROHO mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa MUNGU; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa MUNGU, warithio pamoja na KRISTO; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.''
 
-Kuna watu huongozwa na Neno la KRISTO(Hawa ni majasiri wenye uzima wa milele ndani yao)

Wakolosai 3:16-17 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.'' 

 Watu  wanaoongozwa na Neno la MUNGU kisha wakati huo huo ROHO wa MUNGU anawaongoza maana neno la MUNGU pia ni lake, na wakati huo huo Neno la KRISTO ambalo ndio Biblia yote wanaitii hakika hao ni heri.
Kama umeongozwa na vitu ambavyo havifai mimi Peter Nakushauri anza kuanzia leo kuongozwa na Biblia pamoja na ROHO MTAKATIFU.

Kuna watu maisha yao huongozwa na pesa.
Ndugu, nakuomba mali yako au pesa yako isikuongoze katika maisha yako maana baada ya kuondoka duniani pesa yako haitakuwa na msaada kwako hata mmoja.
pesa uliikuta na utaiacha, hutaondoka na pesa bali utaondoka peke yako.


Ndugu, nakuombaongozwa na Neno ala MUNGU ambalo ndilo Neno la KRISTO pia, Ongozwa na ROHO wa MUNGU. Kuongozwa na Neno la MUNGU na kuongozwa na ROHO wa MUNGU ni jambo moja, ni kitu kimoja na ndio mpango wa MUNGU kwetu.
BWANA YESU anayaweka yote pamoja wakati akimzungumzia ROHO MTAKATIFU aliposema;
 ''Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza MIMI, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo BABA ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.   -Yohana 16:13-15''

ROHO atatuongoza kweli kweli yote.
ROHO atanena ya YESU KRISTO.
Ya MUNGU BABA yote ni ya YESU.
Kumbe ndugu zangu ni muhimu sana tuongozwe na Neno la MUNGU na tuongozwe na ROHO MTAKATIFU.
Ndugu, ongozwa kuanzia leo na Neno la MUNGU na ROHO wa MUNGU.

Sio lazima mawazo yako ya jana yawe ndio mawazo yako ya leo.
Kama jana uliwaza dhambi naomba leo uwaze kuokoka na utakatifu.

Kama jana dawa ya mganga ndio ilikuwa kiongozi wako, nakuomba leo utakatifu ndio ukuongoze.
Kuendeleza mawazo ya jana yasiyokusaidia ni kujipoteza huku unajiona.


 Sheria Ya Kiroho Ni Tofauti Na Sheria Za Kimwili. Sheria Ya Kiroho Humfanya Mtu Awe Wa Kiroho Na Kumpendeza MUNGU. Sheria Za Kimwili Ni Kwa Ajili Ya Manufaa Ya Mwili Na Jamii Na Sio roho. 
Sheria Ya Kiroho Ni Biblia Na Sheria Ya Kimwili Ni Taratibu ulizojiwekea ili zikuongoze.
Taratibu ulizojiwekea zinaweza kuusaidia mwili wako lakini sio roho yako.
Nakuomba uifuate sheria ya kiroho ambayo ni Neno la MUNGU.

1 Petro 1:25 ''Bali Neno la BWANA hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu. ''

 BWANA YESU Amekaribia Kurudi. Je, Umejiandaaje? 
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
 Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
 Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha. 
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka. 
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
 Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments