SIFA SABA(7) ZA WACHUMBA WA AINA YA DELILA.

Na Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze.
Leo nazungumzia mchumba aina ya Delila.

Waamuzi 16:4 '' Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.'' 

Samson alimpenda Delila.
Delila alikuwa mwanamke kama alivyo mwanamke yoyote leo, lakini mchumba wa aina ya Delila hubeba mambo mengi sana ya kuumiza kwa mwenzi wake.
Akina Delila sio lazima wawe wa kike tu, tabia za mchumba aina ya Delila hata wanaume wengi tu wanazo. Tena inawezekana kabisa mikakati ya Delila katika uchumba wake na Samsoni, Mikakati kama hiyo wanaume wengi zaidi wanayo pengine kuliko hata wanawake.
Namzungumzia Delila leo sio jinsia yake ila kusudi lake katika uhusiano wake na Samsoni, kwa hiyo nikizungumzia tabia ya wachumba wanaume aina ya Delila ni kwa sababu ya kusudi la Mchumba huyo aina ya Delila.
Ngoja nianze somo kwa kukuuliza wewe mwenye mchumba au unayetarajia kumpata mchumba.
 
Je Unapendwa Na Mchumba Wako Au Unajipendekeza Kwa Mchumba Wako?
 Swali Hilo Ni Muhimu Kujiuliza Ili Uje Uwe Katika Ndoa Nzuri. Nimewahi Kuona Wanandoa Fulani Wakiambiana Vitu Ambavyo Niligundua Kwamba Kuna Mmoja Kati Yao Hakupendwa Ila Alijipendekeza Tu Kwa Mwenzake Wakati Wa Uchumba. Mwanaume Kwa Hasira Alimwambia Mkewe Kwamba "Nilikuoa Tu Ili Kukusaidia Maana Ulikuwa Unatia Huruma Kwa Umaskini Wenu" 
 Mwanamke Naye Kwa Hasira Akajibu "Niliolewa Na Wewe Kwa Bahati Mbaya Tu Maana Mchumba Wangu Halisi Alikuwa Nje Ya Nchi"
Vitisho Hivyo Viko Katika Ndoa Nyingi Kwa Sababu Tu Ya Mmoja Kati Ya Wanandoa Wakati Wa Uchumba Alijipendekeza Badala Ya Kupendwa. 
Ndugu Ambaye Uko Katika Uchumba Hakikisha Unapendwa Na Sio Wewe Kujipendekeza. 
Kama Hakupendi Huyo Mchumba Wako Heri Kuachana Nae Ili Usije Baadae Ukaonekana Ulijipendekeza Kwake Na Sio Kupendwa Kwa Upendo Wa Dhati. 
Kila Mmoja Ni Muhimu Sana Kumcha MUNGU Na Kuwa Na Hofu Ya MUNGU.
Uongo katika uchumba ni ugonjwa hatari sana unaoweza kuja kuwasumbua katika ndoa.

Mithali 12:19 ''Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.''

 Katika uchumba na mchumba asiye sahihi ulimi wa uongo hutumika sana.
Mchumba aina ya kina delila ni mchumba muongo mwenye nia mbaya na wewe.
Mchumba aina ya kina delila hutumia uongo kama silaha yake ya kukuteka wewe.
Uwe makini sana katika uchumba.
Mtegemee MUNGU ili usije kulia baadae wakati wa ndoa.
Mchumba Wako Kukutaka Mfanye Mapenzi Kabla Ya Ndoa Ni Dalili Muhimu Kwamba Hakupendi Bali Anataka Tu Kukutumia Kama Ka Chombo Kake Ka Starehe Kasiko Na Akili Wala Pumzi. Kuwa Makini Na Mche BWANA YESU Mwenye Uzima Wako Wa Milele.
Yeremia 23:10 ''Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.''
-Hakika nchi imejaa wazinzi na waongo.
-Jieupushe na mchumba mwasherati maana huyo hakupendi.
Shetani wakati mwingine hutumia  uchumba kuwaharibia kila kitu vijana.

 Ndugu, Naomba ujue kwamba Ni Mara Chache Sana Kukutana Na Uchumba Mbaya. Mara Nyingi Sana Uchumba Huwa Mtamu Sana Tena Mzuri Sana Lakini Ikifika Hatua Ya Ndoa Mambo Hubadilika Hasa Kama Mlitamaniana Tu Bila Kupendana. 
 Kuna Watu Walitamaniana Tu Ikapelekea Kuchumbiana Lakini Walipofunga Ndoa Vita Vikaanza, Matukano Kila Siku Kwa Sababu Walitamaniana Tu Hawakupendana. Japokuwa Wakati Wa Uchumba Kila Kitu Kilikuwa Furaha, Ahadi Zilitekelezeka, Baby Ilikuwa Mtoto Mzuri, Honey Ilikuwa Asali Tamu Lakini Wakati Wa Ndoa Vinafutika Vyote Inabaki Tu Kukosoana Na Kulaumiana. Ndugu, Enenda Kwa ROHO Wala Usitegemee Akili Zako katika kuchagua mchumba wako. Mtii BWANA YESU Utaishi katika uchumba wako utakuwa unafanya vyema sana.

 Mithali 21:2 ''Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo.''
MUNGU huipima mioyo hivyo ukimuomba hakika atakuonyesha mtu sahihi na atakufunulia siri ya waongo wanaotaka kukulaghai.
Muhimu ni lazima tu uwe na uhusiano mzuri na MUNGU.
Kuwa na uhusiano mzuri na MUNGU kunaanzia kuokoka kisha kuishi maisha matakatifu.
Binti; huyo kijana aliyekuja kukuchumbia hakikisha kabla ya kumkubali au kumkataa kwanza mpeleke kwenye mizani ya MUNGU ambaye hupima mioyo na kubaini moyo mwenye hila.
Kijana; kabla hujamkubalia huyo binti nakuomba  mpeleke kwanza kwenye mizani ya MUNGU kwa njia ya maombi ili ubaini kama ni mcha MUNGU au ni msanii tu.

Zaburi 118:8 '' Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu.''
 
Wapo pia vijana walioachwa na wachumba zao.
Naomba uyajue haya;
Kama Umeachwa Na Mchumba Wako Ni Muhimu Pia Kujiuliza Kwanini Umeachwa?. 
Je Ulikuwa Unamuomba Hela Mchumba Wako Kila Siku?.
 Je Gharama Zako Zilizidi Sana Kwake?. 
Je Uliacha Maombi Na Ibada Kwa Sababu Ya Uhusiano?.
 Je Uliacha Utakatifu Baada Ya Kumpata Mchumba?. 
Je Mlifanya Uasherati Na Mchumba Wako?.
 Je Wewe Ni Mchafu Ndio Maana Umeachawa?.
 Je Ndugu Zako Wamesababisha Umeachwa?. 
 Ndugu, Siku Nyingine Mche MUNGU Hata Ukiwa Na Mchumba. -Ishi Maisha Matakatifu Hata Kama Umepata Mchumba.
- Baki Kwenye Tumaini La Uzima Wa BWANA YESU Hata Kama Uko Katika Uchumba. 
 MUNGU Atakupa Mchumba Mwingine Ila Jitahidi Sana Katika Uchumba Mpya Mche MUNGU BABA Na Fuata Utaratibu Wa Kikanisa Na Utakatifu.
 Kumbuka Kama Ulimpata Mchumba Wako Kwa Maombi Na Ulinzi Wa Uchumba Huyo Utategemea Maombi Na Utakatifu.

SIFA ZA WACHUMBA WA AINA YA DELILA.

1. Kukudanganya.
Waamuzi 16:15 '' Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi.''
-Kwenye andiko hilo ni kama Delila alikuwa na upendo kwa Samsoni lakini alikuwa amejaa uongo mkuu ndani yake, alipenda kifo cha Samsoni na sio kumpenda Samsoni.
-Leo unaweza kumpata mchumba anakuambia hana mtoto kumpe ana watoto watano(5)
-Unaweza ukampata mchumba anakuambia hiyo ndio rangi yake kumpe amejichubua.
-Unaweza ukampata mchumba kumbe ni jambazi wala sio mcha MUNGU kama unavyomuona nje.

 
2.Kupenda vitu na sio mtu.
Waamuzi 16:19  ''Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. '' 
-Ukikitafuta kitu ambacho Delila alikipenda kwa Samsoni unaweza ukakikosa, ila mimi naona alipenda kifo cha samsoni na sio kumpenda Samsoni, alipenda kuzikata nywele za Samsoni na sio kumpenda Samsoni.
maana hiyo ina maana kwamba huyu Mchumba hakumpenda Mchumba wake, ila alipenda kitu kwa mchumba wake.
-Hata leo kuna wachumba hupenda  pesa na sio mchumba.
Kuna ambao hupenda Elimu ya mchumba na sio mchumba mwenyewe.
Kuna ambao hupenda kazi na sio mchumba husika.
 
3. Kuwa na hila ndani yao.

Waamuzi 16:6 ''Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe.'' 
-Delila alikuwa na hila ndani yake.
Hila yake aliitumia kuonyesha upendo ndipo lengo la hila yake likatimia.
Hila ya Delila ilikuwa ni kumkabidhi Samsoni kwa wafilisti akiwa hana nguvu zake.
Alitumia hila hiyo na alifanikiwa.
Hata leo kuna wachumba wana hila ndani yao ndio maana huleta maumivu wakati wa ndoa.
-Rafiki yangu mmoja ambaye tumewahi kuishi pamoja miaka ya nyuma alikuwa ameokoka na ni mtumishi mzuri kanisani, akampenda binti fulani kanisani kwao ambapo binti huyo alikuwa mtumishi kabisa wa kanisani. Kijana yule baada tu ya kumuoa yule binti alianza kunywa pombe na kumpiga mke wake. Nilipoambiwa niliumia sana lakini baada ya kumpata rafiki yangu yeye alidai simu yake iliibiwa ndio maana hakupatikana kwenye simu, akawa mjanja mjanja akinitoroka kimaongezi kila mara. Binti yule hata kwenye huduma akaanza kuyumba. Kumbe rafiki yangu alikuwa na hila ndani yake.
Mfano kama angeanza pombe wakati wa uchumba hakika yule binti asingemkubali. Wachumba aina ya Delila ni wengi na wanatesa wengi.
 

4. Kutumika kipepo dhidi yako.
Waamuzi 16:5 ''Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja.''
-Delila alikuwa ni mchumba wa Samsoni lakini alikuwa anatumika kipepo.
Alikuwa anatumiwa kipepo na wakuu wa wafilisti ambao walimweleza hadi mambo ya kufanya ili kumnasa Samsoni.
Hata leo kuna vijana huenda kwa waganga ili kuwapata mabinti au  vijana fulani wachumbiane, huko ni kutumika  kipepo na siku zote uchumba wa hivyo tarajia uharibifu baadae.
 
5.Wasaliti.

Waamuzi 16:18 '' Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.''
-Delila alimsaliti Samsoni ili apate Pesa, ndio maana hapo kwenye andiko unaona wafilisti wakija nyumbani kwa samsoni wakiwa na fedha, tayari kumlipa Delila baada ya usaliti alioufanya.
Hakuna mchumba mbaya kama msaliti.
Msaliti anaweza kukuua ili apate pesa  maana hakupendi wewe kama mchumba.
Ndio maana kila siku nawaonya watu kwamba usikubali kutafuta mchumba nje na kanisa la MUNGU.
Muombe MUNGU ili kukupa mtu sahihi lakini mtu huyo yuko ndani ya kanisa la KRISTO na sio nje ya KRISTO.
Nje ya kanisa kuna wasaliti tu na wenye hila.
 
 
6.Wanaishi maisha ya maigizo ili kukunasa.

Waamuzi 16:16 '' Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. ''
-Delila kila siku alikuwa anajiliza mbele ya Samsoni ili Samsoni amweleze ukweli kuhusu asili ya nguvu zake.
Huyu Delila alikuwa anaishi maisha ya maigizo katika uhusiano wake na  Samsoni.
-Hata leo wachumba aina ya Delila wamejaa.
Unatakiwa uwe makini sana ndugu yangu unayetegemea kupata Mchumba.
Nimewahi kuandaa masomo mengi sana kuhusu uchumba na ndoa unaweza ukayatafuta ndani ya blog ya Maisha ya ushindi ili kuongeza ufahamu juu ya masuala ya uchumba na ndoa.
 

7.Kutumia udhaifu wako ili kujinufaisha wao.


Waamuzi 16:17 '' Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.''

-Samsoni alionyesha udhaifu mkubwa baada ya kumweleza Delila siri zake.
Mchumba aina ya Delila ukimweleza siri zako anaweza kukuharibia na kukuachia machungu makuu na kilio cha mara kwa mara.
Mimi sitaki ujue useme ''nimesamehe ila sitasahau'' bali nakuomba kabla ya yote mhusishe MUNGU katika uamuzi wako juu ya mchumba huyo, pia wahusishe baba zako wa kiroho au viongozi wako wa kiroho wakusaidie katika kuamua vyema.
Jambo jingine  baya ambalo hufanywa wachumba wa aina hiyo ni Mapambo mengi yasiyo na maana ambapo mapambo hayo huondoa uhalisia wa mtu. Siku asipojipamba unaweza ukakimbia maana ndipo utamuona yeye halisi.

na pia wachumba wa aina hii hupenda kuvaa kikahaba.
Unakuta mchumba wa mtu lakini kila siku mitaani anavaa vimini tu, huyo havai.
Unakuta mchumba kila siku anavaa nusu uchi, matiti nje, huyo havai.
Je, una mchumba wa aina ya Delila?

 Haitoshi Tu Mtu mtu Kuwa Na Jina La Kikristo Bali Inatakiwa Utakatifu Na Kupanda Kiwango Cha Kiroho.
 Ndugu jioke na kizazi hiki chenye ukaidi.
BWANA YESU anakungoja sasa ili uamue vyema leo.
Ubarikiwe sana.Nakuomba pia nisaidie kuwasambazia na wengine ujumbe huu.
Ni mimi ndugu yako Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Mabula1986@gmail.com
+255714252292.

Comments