UFUNUO WA MUNGU KWA WANADAMU.

Na Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Biblia ni ufunuo wa MUNGU kwa wanadamu.
Neno ''Ufunuo'' lina maana ya kuondoa kilichofunika au kilichozibwa ili sasa kionekane au kijulikane kwa usahihi.

Kuna mambo mengi ambayo Biblia kama ufunuo wa MUNGU imeweza kuyaweka wazi hata kila mtu akajua.


2 Petro 1:20-21 '' Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa MUNGU, wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU.''


Biblia ndio pekee inayojulisha kila kitu kuhusu uumbaji na muumbaji.


=Ni Biblia pekee inayotujulisha kuhusu MUNGU wa kweli na muumbaji wa kila kitu.

Isaya 45:18 '' Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni MUNGU; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.''.

Hakika JEHOVAH ni MUNGU, Zaidi yake hakuna MUNGU mwingine  ila miungu tu na hiyo ni machukizo. Inapoandikwa kwenye Biblia Neno ''BWANA'' kwa herufi kubwa maana yake ni JEHOVAH au YAHWEH. Yeye ndiye MUNGU aliyeumba mbingu na dunia na kila kilichomo. Biblia iko wazi sana ikiongezea kusema kwamba ''Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.-Zaburi 83:18'' 

=Ni Biblia pekee inayotujulisha kwamba uzima wa milele upo na uzima huo ni katika KRISTO YESU pekee.

1 Yohana 5:11-13 ''Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe(YESU). Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.''

Huo ndio ufunuo wa MUNGU kwa wanadamu.
Alilolipanga MUNGU hakuna hata mmoja anaweza kulipinga.
ukimkataa YESU KRISTO moja kwa moja unakuwa umeikataa mbingu. Ukimkataa KRISTO moja kwa moja unakuwa umeipenda jehanamu. Biblia iko wazi sana ikisema '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.-Yohana 3:16-18''
 
=Ni Biblia pekee inatujulisha mwanzo wa kila kitu na mwisho wa dunia.

Mwanzo 1:1 ''Hapo mwanzo MUNGU aliziumba mbingu na nchi.''
Huo ni mwanzo wa uumbaji wa MUNGU kwa dunia,  lakini sio mwanzo wa viumbe walioko mbinguni.  huo Mwanzo unaozungumzwa kwenye hilo andiko ni Mwanzo wa viumbe wa duniani na sio uumbaji wa malaika wala viumbe wengine wa mbinguni, maana hao waliumbwa  kabla ya mwanadamu.

Miaka kadhaa baada ya mwanadamu kuumbwa aliasi.
Mwanadamu  aliasi baada ya kukubali uongo wa shetani.
Kwa Neema ya MUNGU  iliyo kuu sana MUNGU alileta Wokovu Kupitia YESU KRISTO.
Muda huu ni wakati wa kila mwanadamu anayeutaka uzima wa milele basi ampe YESU maisha yake, kisha aishi maisha matakatifu.
Kwa upendo wa MUNGU wa ajabu sana MUNGU aliamua kufunua hata mwisho wa watenda dhambi utakuwaje na mwanzo wa maisha ya uzima wa milele utaanzaje.
Biblia iko wazi sana ikisema ''Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.-Marko 13:26-27''
 
=Ni Biblia pekee inayotujulisha kwamba tunatakiwa tuishi kwa kumpendeza MUNGU aliyetuumbia matendo mema, ambayo MUNGU anataka wanadamu wote tuyaishi, na maagizo yake yote yako pekee katika Biblia.

Zaburi 34:14-16 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.''

Kumbukumbu la watenda mabaya(dhambi) litaondolewa kwa sababu hawatakuwa na sehemu katika uzima wa milele, kwa sababu watatupwa katika ziwa la moto. 
Ni heri sana kumtii MUNGU leo kwa kumpokea KRISTO Mwokozi.
Ni heri sana kuufuata mpango wa MUNGU wa wokovu.

=Ni Biblia pekee inayotujilisha kwamba tufanyeje ili tuwe wenye haki mbele za MUNGU Muumba wetu.

Warumi 10;9-11 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.''
 
=Ni Biblia pekee inayotufundisha maisha ya kila mwanadamu baada ya kuondoka duniani. kuna watakaoenda uzimani na kuna watakaoenda jehanamu.

Mathayo 25:46 ''Na hao(Waovu) watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.'' 

Biblia ndio ina mpango mzima wa wokovu wa MUNGU kwa mwanadamu.
Kama kuna kitabu kingine chochote kinachojaribu kuelezea matukio ya kuanza kwa ulimwengu na mwisho wake ni kwa kuiiga tu Biblia maana Biblia ipo miaka 2000 Kabla ya kitabu kingine chochote kuwepo duniani. hivyo vitabu vilivyofuata baadae chanzo chake ni kukopi baadhi ya mambo ya ndani ya Biblia na kuyapindisha ili watu wamkatae KRISTO mwenye uzima pekee wa milele kwa watakaomwendea
 Ukitaka kujifunza Biblia na kuielewa inabidi pia ukubali kufundishwa na watumishi wa MUNGU.
Pia maombi yanawezeza kukufanya uelewe vizuri Biblia baada ya fundisho.
Mfano kuna siku mchana nilikuwa nasoma Biblia  kitabu cha Isaya  Sura ya 42 na  na Sura ya 43 ni unabii unaohusu mambo mengi na Kwa ufupi ni:
Kuuandaa ulimwengu Kwa ajili ya Wokovu Wa BWANA YESU.
Ni taarifa ya ujio Wa Mkombozi YESU ambaye atatokea Israel.
Ni taarifa ya kurudishwa waisrael katika taifa lao la asili baada ya kuwa uhamishoni Kwa miaka mingi sana.
Maandiko haya pia yanatukumbusha kwamba kama mwanadamu ataacha mabaya hakika MUNGU atakuwa naye na kumbariki.
Maandiko hayo pia yanaonyesha mamlaka ya MUNGU ni ya mwisho na hakuna anayeweza kwenda kinyume na matakwa ya Mwenyezi.
Maandiko hayo pia yanaonyesha kwamba hakuna MUNGU mwingine Wa kweli ila ni JEHOVAH na hakuna Wa kuabudiwa ila yeye.
Hapo ni Kwa ufupi katika nilichojifunza.
Maandiko haya pia ni lugha ya kinabii ndio maana wakati mwingine kuna baadhi ya mistari tunashindwa kuielewa Kwa akili zetu hadi tufunuliwe kujua na ROHO wa MUNGU.
Unabii kama huu huwa unawakilisha matukio matatu Kwa wakati mmoja.
Kwanza ni unabii Wa wakati unatolewa na Kwa watu Wa wakati huo.
Pili ni unabii Wa wakati Wa kuja Kwa Yohana mbatizaji na BWANA YESU mwenyewe.

Tatu ni unabii Wa kukusanywa Kwa waisraeli miaka 1900 baada ya KRISTO kuzaliwa.

Hiyo ni sehemu tu ndoto ya Biblia ambayo ni Ufunuo wa MUNGU kwa wanadamu. 
Isaya 51:6 '' Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka. ''
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments