VIKAO VYA UHARIBIFU

Na Mchungaji Adriano Makazi, Ufufuo na uzima.



Hakuna jambo lolote linaloweza kutokea au kuendelea mbele bila watu kukaa vikao, wanaweza wakawa watu wawili au zaidi ili jambo hilo lifanikiwe kwa uzuri ama kwa ubaya. Vyanzo vingi vya matatizo ya watu wengi leo hii duniani limeanzia kwenye kikao. Haibishaniwi kwamba mambo mengi yanayotokea yameanzia kwenye vikao/mashauriano. Inaweza ikawa kupandishwa kazi au kupatwa na mabaya.
Mithali 20: 18 “Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita.”
Tunaona kumbe kuna mambo mengi hutokea au huthibitika kutokana na mashauri ya watu au vikao vya watu. Baada ya mashauri utekelezaji hutokea. Kila kusudi liwe baya au zuri huwa linathibitika mara baada ya kulikalia kikao.
2 Samweli 15:31 “Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili.”
Mfalme Daudi alipinduliwa na mwanaye Absalom . Ahithofeli alikuwa mshauri wa Daudi ambaye alimsaliti na kwenda kuungana na mwanaye ili wampindue. Kila mfalme au mfanya biashara huwa na mshauri wake ambaye anaweza kuonekana au asionekane lakini sisi mshauri wetu ni Roho mtakatifu ambaye hutushauri mambo ya ajabu ya Ufalme wa Mungu.

Wanaokukalia vikao ni wale wanaokufahamu vizuri.
Mathayo 10: 36 “Na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.”
Adui zako huwa hawatoki mbali na wewe bali ni wale wanatoka nyumbani mwako, anaweza kuwa ndugu yako au mfanyakazi mwenzako au rafiki yako. Ahithoferi alitoka kwa Mfalme Daudi akenda kumshauri Absalom ili aende Daudi. Unapokaa na mtumishi wa Mungu unaweza kutoka na laana au Baraka sababu unaweza kuona mapungufu ya kuhani wa Bwana na ukaanza kumdharau jambo ambalo linaweza kukuletea laana.
Elisha alikuwa chini ya Eliya ambaye alikaa vizuri na Eliya akapata upako mara mbili, Elisha aliishi na mtumishi wake Gehaz ambaye alikuja kupaka ukoma sababu hakujua jinsi ya kukaa na mtumishi wa Mungu vizuri.

Tumeona Ahithofeli alikuwa amajua Daudi. Watu hufanya vikao vya uharibifu na watu sababu huogopa kwamba kwa spidi wanayokwenda nayo wanaweza kupitwa hivyo huamua kufanya vita nao.
Daudi alipopakwa mafuta na mtumishi wa Mungu ili awe mfalme, mfalme wa Israeli alikuwa Sauli. Ilitokea vita kati ya Israeli na Wafilisti ambao walimtoa mtu mmoja aitwaye Goriathi na Israeli nao hawakumtoa mtu mpaka Daudi alipokwenda kuwatembelea ndugu zake alipomkuta Goriath akiwatukana Israeli. Goriath alikuwa akiwatukana wana wa Israeli asubuhi na jioni kila. Daudi alimpiga shujaa wa wafilisti na wale wafilisti walipoona shujaa wao amepigwa walikimbia wote. Hivyo hivyo itakavyokuwa kwa adui zako waliopanga vita juu yako watakimbia mbele yako kwa jina la Yesu.
Baada ya Daudi kumpiga Yule mnefili watu walitoka wakaanza kumwimba Daudi kiasi cha kusababisha Mfalme Sauli kuudhika Sababu yeye ndiye aliyekuwa Mfalme aliyestahili kupewa sifa. Tunajifunza kwamba unaweza ukawa unafanya kazi kubwa nzuri na mtu mwingine akaudhika na kufanya vita nawe.
1Samweli18: 1 “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe.Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”
Tangu siku ile ulipopata promotion Sauli wa maisha yako alikuonea wivu, tangu siku ile ulipovishwa pete Sauli alikuonea wivu, tangu siku ile uliposafiri nje ya nchi kibiashara Sauli alikuonea wivu. Kuna mtu hapendi mafanikio yako naye ndiye aliyeanza kukufanyia vita. Imeandikwa akugusaye wewe anagusa mboni ya jicho la Bwana Usiogope. Tangu siku ile Daudi alipofanikiwa ndipo alipoanza kupatwa na misukosuko kwenye maisha yake.
Majibu yote yapo ndani ya Biblia.

2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;”
“Vikao kwenye Biblia”
Mungu alikaa kikao mbinguni ili kumtengeneza mwanadamu, Kikao kile kilikuwa kitakatifu kwaajili ya kumuumba mtu kwa mfano wao na sura yake. “Tunalinda na Nguvu za Mungu kwa njia ya Imani” usiwaogope.

Mungu hajaruhusu tuone mabaya yanayotumwa kwetu. Inawezekana kuna vikao huwa Mungu anaviteketeza visifanikiwe ili makusudi yao yasitokee kwetu.
2. Kikao walichokaa ndugu zake Yusufu.
Mwanzo 37: 4 "Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.”

Ndugu zake Yusufu walikaa kikao wakamjadili Yusufu jinsi watavyompoteza. Jambo lililowafanya ndugu zake Yusufu wamchukie lilikuwa ni ndoto alizoziota. Tunaona hawa ni ndugu lakini walichukizwa na ndoto yake. Yusufu alipatwa na mabaya ya kusingiziwa kubaka sababu aliuzwa na ndugu zake akaingia gerezani.
3. Kikao kilichofanyika Babeli, Danieli alikuwa akifanya kazi na watu ambapo alikuwa akikaa karibu na Mfalme”
Daniel 6: 1 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku. Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.”

Danieli alikua akifanya kazi na watu wa idara moja ya kumtumikia Mfalme na utendaji wake ulikua unaonekana mbele ya Mfalme mpaka akabahatika kuwekwa kuwa msimamizi mkuu wa viongozi wote. Maandiko yanasema ukiwa mwaminifu kwa mambo madogo Mungu atakupa mambo makubwa, ukiwa mwaminifu kwa mali ya mtu mwingine Mungu atakufanikisha kwa mali kubwa. Daudi alifanya uaminifu kwenye kazi aliyopewa akapata kibali cha kusimamia wenzake.
Danieli alifanyiwa kikao cha uharibifu na wafanyakazi wenzake kwasababu walikuwa wanamwonea wivu wa mafanikio yake.
Biblia inasema mawaziri, madiwani na wengine wengi walikaa kikao ili kumshtaki Danieli kwa makosa yake wakakosa sababu ya kumshtakia, Danieli alikuwa msafi hana hatia wakaamua kumkamata kwa mambo ya Mungu wake sababu alikuwa anampenda wakatengeneza waraka wakampelekea Mfalme kwamba wamekubaliana watenge siku thelathini watu wote wamwabudu Mfalme peke yake yaani Ibada apewe Mfalme asipewe Mungu na mtu atakayekiuka sharia ile atupwe kwenye tundu la Simba.

Biblia imetuonyesha mpango wao ulikuwa kuwaondoa watu wanaomwabudu Mungu na kutenda haki waondolewe. Biblia inasema Danieli aliposikia mpango huo alifahamu umemlenga yeye ndipo akaamua kuingia nyumbani kwake na kufungulia madirisha yote na milango akamua kumwabudu Mungu wake asubuhi mchana na jioni.
Daniel alikuwa hawezi kumwabudu mfalme sababu alifahamu wakuabudiwa ni Mungu muumba mbingu na nchi pekee.
4. vikao vya uharibifu juu ya Shedrak, Meshak na Abednego.
Shadrak, meshak na Abednego walikataa kumwabudu mungu sanamu sababu hawakuwa tayari kumwabudu mungu asiye Mungu wa Israeli. Biblia inasema baada ya kukata kupomoka mbele ya Yule mungu Mfalme alibadilika sura akaamuru watupwe kwenye moto uliowashwa kwaajili yao, lakini wakina shadrak meshak na Abednego hawakuogopa sababu waliamini Mungu wanayemwabudu asipowaokoa basi wako tayari kufa.

Danieli 3:19 “Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. 22 Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego.23 Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto.26 Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.”
Maandiko yanasema aliyeta mtego utamnasa mwenyewe na aliyechimba shimo atatumbukia mwenyewe. Hata wewe wale waliopanga vikao vya uharibufu ili wakukamate uharibikiwe na kuangamia wao wao ndio watakao hangamia kwa jina la Yesu. Hakuna jambo gumu asiloliweza Bwana. Kuna watu wanaoshindana na kesho yako kwasababu umeanza kufanikiwa na unaelekea mbali.
Usiwaogope watu wanaokuwinda na kukutengenezea moto na kukuchimbia mashimo sababu mabaya yao hayatakupata hata moja. Ukiwa ndani ya Yesu hakuna mabaya yatakayokupata .
Ayubu 5: 12 “Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.”

Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”
“Katika jina la Yesu ninavisambaratisha vikao vyote vya uharibifu vilivyopangwa juu yangu. Vikao juu ya afya yangu, vikao juu ya biashara yangu, vikao juu ya elimu yangu ninavisambaratisha kwa jina la Yesu, zile ajenda za vikao vya uharibifu ninazilaani kwa jina la Yesu, wasimamizi wa ajenda za vikao vya siri na madhabahu zao na viongozi wa vikao vya uharibifu juu yangu na familia yangu ninawashinda kwa damu ya Yesu, naviharibu vikao vyote vya uharibifu dhidi yangu kwa jina la Yesu.

Comments