Waziri mkuu wa Israeli awasili Uganda




Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.


Hali ya usalama imeimarishwa maradufu mjini Kampala na Entebbe Uganda baada ya kutua kwa ndege inayombeba Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.
Bw Netanyahu ambaye ameandamana na mkewe Sarah anaanzia ziara yake ya siku 5 barani Afrika nchini Uganda.
Netanyahu atazuru uwanja wa ndege wa Entebbe na kukagua gwaride la heshima litakaloandamana na makombora 19 kwa heshma yake.


Bw Netanyahu atahudhuria sherehe rasmi ya ukumbusho wa mika 40 tangu uvamizi wa uwanja wa ndege wa Entebbe na makomando wa kiyahudi kuwaokoa abiria wa ndege moja wayahudi waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo wa kipalestina .
Ndege hiyo ilikuwa imetoka Israeli ikielekea Ufaransa.
Kwa waziri Netanyahu, hii sio kumbukumbu rasmi ya kitaifa ila ina maana kwake binafsi kwani kakake Yoni, ni mmoja kati ya makomando wayahudi waliouawa katika operesheni hiyo ya kihistoria.

Ndege iliyotumika na makomando wa jeshi la Israeli kuwakomboa mateka wayahudi huko Entebbe Mwaka 1976.

Kwa Israeli ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano wa taifa hilo la kiyahudi.
Mwenyeji wake rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amewakaribisha marais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Paul Kagame wa Rwanda Salva Kiir Mayardit, wa Jamuhuri changa zaidi duniani ya Sudan Kusini Edgar Lungu wa Zambia waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, na waziri wa maswala ya Kigeni wa Tanzania Augustine Mahiga katika kikao cha faragha kinachotarajiwa kujadili maswala ya ugaidi na Usalama wa taifa ambayo Israeli imeahidi kuyasaidia kukabiliana nayo.


Duru kutoka Kampala zinaeleza kuwa makomando wa Israeli tayari wameshika doria kote mjini Kampala dakika chache tu kabla ya ndege iliyombeba Waziri Benjamin Netanyahuna ujumbe wake kutua.

Comments